• HABARI MPYA

    Wednesday, April 06, 2016

    KIIZA, JUUKO KIKAANGONI SIMBA SC

    Na Somoe Ng'itu, DAR ES SALAAM
    WACHEZAJI wawili wa kimataifa wa Simba kutoka Uganda, Hamisi Kiiza na Juuko Murshid, huenda wakakumbana na adhabu ya kusimamishwa kutokana na kuchelewa kurejea nchini kuungana na timu hiyo inayoongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.
    Kiiza na Murshid walipewa ruhusa ya siku tano kwenda Uganda kuitumikia timu yao ya Taifa lakini hadi jana wachezaji hao hawajarejea nchini.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema kwamba nyota hao walipewa ruhusa ya siku tano ambayo iliishia Jumamosi.
    Hamisi Kiiza anaweza kuadhibiwa Simba SC kwa utovu wa nidhamu

    Manara alisema kwamba tayari kocha mkuu wa timu hiyo, Jackson Mayanja, amewaondoa kwenye programu yake kwa ajili ya kuwakabili Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho utakaofanyika Aprili ya  11 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
    "Kwa kweli hatuna taarifa zao, walipaswa kurejea nyumbani tangu Jumamosi, lakini hawajarudi na wamekaa kimya, tayari mwalimu (Mayanja) ameshawaondoa kwenye mipango yake," alisema Manara.
    Aliongeza kuwa kikosi chao kinaendelea na mazoezi isipokuwa kiungo, Mwinyi Kazimoto ambaye ni majeruhi na amepewa mapumziko ya siku saba na daktari wa timu hiyo.
    Kiiza ndiye anayeongoza kwa kupachika mabao msimu huu akiwa amefikisha magoli 19 akifuatiwa na Amissi Tambwe wa Yanga aliyecheka na nyavu mara 18.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIIZA, JUUKO KIKAANGONI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top