• HABARI MPYA

    Wednesday, April 06, 2016

    TFF IJIPANGE KULIPA MAKOCHA WA TIMU ZA TAIFA

    WIKI iliyopita Serikali ilitangaza rasmi kujitoa kwenye mpango wa kulipa mishahara ya makocha wa timu za taifa za soka za Tanzania.
    Waziri wa Michezo, Nape Nnauye wiki hii alikaririwa akisema kwamba, Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amesema Serikali yake haiwezi kusaidia mchezo mmoja pekee na kwa kuwa haiko tayari kwa sasa kusaidia michezo yote, bora iache kusaidia na soka pia ili ijione haipendelei.
    Miaka 10 iliyopita, Rais aliyemaliza muda wake, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete aliamua kuibebesha Serikali yake jukumu la kulipa mishahara ya makocha wa kigeni wa timu za taifa.

    Uamuzi huo wa Rais Kikwete ambaye kihistoria ni mpenzi wa michezo na shabiki mkubwa wa klabu kongwe nchini, Yanga hakika ulisaidia kwa kiasi fulani kurejesha hamasa ya wananchi kuipenda timu yao, Taifa Stars kuanzia enzi za Mbrazil, Marcio Maximo aliyefuatiwa na Wademark wawili mfululizo, Jan Borge Poulsen, Kim Poulsen, Mholanzi Mart Nooij na sasa mzalendo, Charles Boniface Mkwasa.
    Makocha wote wa kigeni walilipwa stahiki zao vizuri, lakini baada ya kuingia Mkwasa aliyerithi mikoba ya Nooij Juni mwaka jana ndipo mambo yameharibika na sasa inalezewa anadai zaidi ya Sh Milioni 200.
    Ukweli ni kwamba uamuzi huu ni pigo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na familia ya mchezo huo kwa ujumla, kwa sababu inafahamika bado bila mkono wa Serikali mambo hayawezi kwenda sawa.
    Lakini TFF hawana budi kuupokea na kukubaliana nao, kwa sababu ndiyo hali halisi – maana yake lazima wafikirie kuendesha soka ya nchi kwa ujumla kutokana na uwezo walionao.
    Binafasi, nimesikitishwa na uamuzi wa Serikali ya Dk. Magufuli kusitisha kuwalipa makocha wa Taifa Stars, lakini nawashauri TFF sasa wakae chini na kufikiria namna ya kuweza kuendesha soka ya nchi hii kwa uwezo wao.
    Taifa Stars inadhaminiwa na kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager, basi katika fungu la udhamini wa Stars lipatikane fungu la kulipa benchi la Ufundi la Stars.
    Na umefika wakati sasa tuache utaratibu wa kutumia watu bila mikataba.
    Lazima kuanzia mtunza vifaa na wengine wote wa benchi la Ufundi wawe na Mikataba.
    Kuhusu timu za vijana, TFF inapaswa kutafuta fungu la fedha la kuwalipa makocha wa timu za vijana ili operesheni za soka ya nchi hii ziendelee kwa ufanisi.
    Inafahamika nchi nyingi zinazofanya vizuri kisoka hapa Afrika zinapata msaada mkubwa kutoka kwa Serikali zao, lakini sisi hapa hatuwezi kushindwa kuendelea kucheza mpira kwa sababu Serikali imejitoa kulipa mishahara ya makocha.  
    TFF iendelee kuhangaikia maendeleo ya soka ya nchi hii na Serikali isubiri kuja kutoa pongezi siku moja mambo yakiwa mazuri. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF IJIPANGE KULIPA MAKOCHA WA TIMU ZA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top