• HABARI MPYA

  Sunday, April 10, 2016

  AZAM FANYA KWELI LEO, ESPERANCE KITU GANI!

  Na Adam Fungamwango, DAR ES SALAAM
  WAWAKILISHI wa Tanzania Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Azam FC, leo inatarajia kushuka kwenye uwanja wake wa nyumbani Azam Complex kupambana na Esperance ya Tunisia.
  Ni mechi ya raundi ya pili ya kombe hilo, Azam ilipoingia baada ya kuiondoa Bidvest Wits  ya Afrika Kusini kwa jumla ya magoli 7-3.
  Katika mechi ya kwanza ugenini ilishinda mabao 3-0, kabla ya kushinda kwa mbinde nyumbani kwa mabao 4-3.
  Kwa vyovyote vile mechi hiyo haitoikuwa rahisi kwa Azam, inabidi itokwe machozi jasho na damu ili kuweza kupata ushindi kutokana na kuwa Esperance ni moja kati ya timu kongwe na zenye uzoefu mkubwa na michuano mikubwa kama hii barani Afrika.

  Lakini pia historia inaibeba timu hiyo ya Tunisia kuwa si timu inayotolewa kirahisi kwenye hatua ya mtoano na badala yake nyingi hutinga kwenye makundi, iwe Ligi ya Mabingwa au Shirikisho.
  Kwa upande Azam timu hiyo ambayo inashiriki michuano ya kimataifa kwa mara ya nne sasa, haijawahi kutinga hatua ya makundi.
  Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2013 ilipotolewa kwenye raundi ya 16 bora Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya nchini Morocco.
  Katika mechi ya kwanza timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana Azam Complex kabla ya  mechi ya marudiano Azam kulala kwa mabao 2-1
  Mwaka 2014 Azam ilitolewa kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kuchapwa jumla ya mabao 2-1 dhidi ya Ferroviario Beira ya Msumbiji, baada ya kushinda mabao 1-0 nyumbani, lakini ikachapwa ugenini mabao 2-0.
  Mwaka jana 2015 ilitolewa na El Merreikh kwa jumla ya magoli 3-2 kwenye Ligi ya Mabingwa chini ya Mcameroon James Omog, iliposhinda mabao 2-0 nyumbani, lakini ikachapwa mabao 3-0 nchini Sudan.
  Katika mechi ya leo Azam itacheza bila mchezaji wake wa kutegemewa Shomari Kapombe.
  Kapombe ataukosa mchezo wa leo kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa Nimonia tangu wiki iliyopita, kitu ambacho kitakuwa pengo kubwa kutokana na umuhimu wa mchezaji huyo kwa siku za hivi karibuni.
  Kwa sasa mchezaji hiyo yupo nchini Afrika Kusini kwenye hospitali ya Morningside Mediclinic mjini Johannesburg akipatiwa matibabu.
  Kwa mujibu wa daktari wa timu hiyo Juma Mwimbe ni kwamba Kapombe hatacheza mechi zote mbili dhidi ya Esperance.
   Mbali na kuwa mhimili imara wa safu ya ulinzi, Kapombe pia amekuwa mpishi na mfungaji mzuri wa mabao ya timu msimu huu, hadi sasa akiwa amefunga mabao manane kwenye Ligi Kuu pekee.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FANYA KWELI LEO, ESPERANCE KITU GANI! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top