• HABARI MPYA

  Sunday, March 13, 2016

  SIMBA SC KUENDELEZA UBABE LIGI KUU LEO?

  Na Adam Fungamwango, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC itajaribu kujiongezea pointi za kuwaweka mbali zaidi ya wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodcom Tanzania Bara, Azam na Yanga wakati itakapomenyana na Prisons Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.
  Simba inayoongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 51, itafikisha pointi 54 ikiifunga timu ya jeshi la Magereza na kuwazidi mabingwa watetezi, Yanga kwa pointi nne, ingawa Wekundu wa Msimbazi watakuwa wana mechi mbili zaidi za kucheza.
  Simba itaingia uwanjani ikiwa na wastani mzuri wa kushinda mechi zao kwenye Uwanja wa Taifa na haijafungwa na timu yoyote ile ya mkoani msimu huu.
  Timu hiyo imefungwa kwenye Uwanja huo mara mbili tu, tena zote na watani wao wa jadi, Yanga na imetoa sare moja tu dhidi ya Azam FC kwenye uwanja huo, huku mechi nyingine zote ikishinda.

  Pia itaingia ikiwa na mshambuliaji wao hatari, Mganda Hamisi Kiiza anayeongoza kwenye orodha ya wafungaji bora kwa magoli 18, atakayetaka kufunga magoli mengine ili azidi kumuacha Amissi Tambwe wa Yanga, anayemfuatia kwa karibu akiwa na magoli 17.
  Mara ya mwisho zilipokutana kwenye uwanja huo katika Ligi Kuu msimu uliopita mechi ya mzunguko wa pili, Simba iliiadhibu Prisons kwa kuifunga mabao 5-0, Ibrahim Hajib akipiga hat-trick, huku mabao mengine yakifungwa na wachezaji walioondoka, Mganda Emmanuel Okwi aliyehamia Denmark na winga Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyehamia Azam. 
  Hata hivyo, kiuhalisia haitokuwa mechi rahisi kwa Simba kwani itabidi itokwe machozi, jasho na damu kutokana na uwezo mkubwa wa Prisons inaounyesha msimu huu, hasa kwenye mechi za karibuni.
  Timu hiyo yenye maskani yake mkoani Mbeya imekuwa ikifanya vizuri kwenye mechi zake hivi karibuni kiasi cha kukamata tano kwa pointi 36 kabla ya mechi za jana za Ligi Kuu.
  Pia rekodi zinaonyesha kuwa mechi tatu ilizopoteza Simba ukiacha mbili ilizofungwa na Yanga, iliyobaki imefungwa na Prisons kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza msimu huu Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Ilikuwa ni Oktoba 21 mwaka jana, Prisons ilipoichapa Simba bao 1-0, lililofungwa na Mohamed Mkopi dakika ya 62.
  Kama kawaida, Mkopi anatarajia kuiongoza tena leo safu ya ushambuliaji wa timu hiyo akiwa na 'pacha' wake Jeremiaha Juma, mshambuliaji hatari aliyefikisha magoli 11 mpaka sasa kiasi cha kumfanya achaguliwe kwenye kikosi cha timu ya taifa Taifa Stars.
  Kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza Ligi Kuu msimu uliopita 2014/15 zilitoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, Okwi akifunga goli la mapema, lakini dakika moja kabla ya mechi kumalizika Hamisi Maingo alisawazisha. Mechi hiyo ilichezwa Oktoba 25, 2014.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUENDELEZA UBABE LIGI KUU LEO? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top