• HABARI MPYA

    Sunday, March 13, 2016

    HONGERA YANGA NA AZAM, LAKINI SOMO LA MUFULIRA WANALIJUA?

    WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Afrika, Azam na Yanga jana wote wameshinda mechi za ugenini, huku JKU pekee ikipoteza.
    Azam FC imeanza vyema michuano ya Afrika kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya wenyeji Bidvest Wits jana usiku Uwanja wa Bidvest mjini Johannesburg, Afrika Kusini katika mchezo wa kwanza Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika.
    Maana yake Azam FC sasa itacheza bila presha mechi ya marudiano Dar es Salaam wiki ijayo, ikihitaji sare kusonga mbele.  

    Mabao ya Azam FC jana yalifungwa na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dakika ya 51, beki Shomary Kapombe dakika ya 56 na mshambuliaji na Nahodha John Bocco ‘Adebayor’ dakika ya 59. 
    Nao Yanga SC wamejiweka kwenye nafasi nzuri ya kuingia hatua ya mwisho ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji APR katika mchezo wa kwanza wa raundi ya Kwanza jana Uwanja wa Amahoro, Kigali, Rwanda.
    Asante kwa wafungaji wa mabao hayo, beki Juma Abdul Jaffar kipindi cha kwanza na kiungo Mzimbabwe Thabani Scara Kamusoko kipindi cha pili na Yanga sasa watahitaji hata sare mchezo wa marudiano ili kusonga mbele.
    Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na Duncan Lengani, aliyesaidiwa na washika vibendera Clemence Kanduku na Jonizio Luwizi wote wa Malawi, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Bao hilo lilifungwa na beki wa kulia aliye katika kiwango kizuri kwa sasa, Juma Abdul Jaffar dakika ya 20 kwa shuti la mpira wa adhabu ndogo umbali wa mita 30, baada ya Nahodha wa leo wa Yanga, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima kuangushwa.
    Yanga iliyokuja na mashabiki wapatao 100 kutoka Dar es Salaam walioongezewa nguvu na mamia ya mashabiki wa mahasimu wa APR, Rayon walitawala mchezo kipindi cha kwanza na ilikuwa vigumu kuamini kama APR walikuwa nyumbani.
    Kipindi cha pili, kidogo APR walikianza vizuri na kuonekana kama wangeweza kusawazisha, lakini bado nyota ya Wana Jangwani iliendelea kung’ara Kigali.
    Kiungo Thabani Scara Kamusoko akaifungia Yanga bao la pili dakika ya 74 akimalizia pasi ya Mzimbabwe mwenzake, mshambuliaji Donald Dombo Ngoma.
    Baada ya bao hilo, Yanga wakajiamini zaidi na kujikuta wanaizawadia bao rahisi APR dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za kawaida lililofungwa na Patrick Sibomana. 
    Mchezo wa marudiano utafanyika wiki moja baadaye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na utachezeshwa na marefa wa Shelisheli; katikati Bernard Camille na pemebeni watakuwapo Eldrick Adelaide na Gerard Pool. 
    Bahati mbaya, wawakilishi wengine wa Tanzania, JKU ya Zanzibar walifungwa mabao 4-0 na wenyeji SC Villa katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Mandela, Kampala, Uganda. 
    Mabao ya Jogoo Jogoo la Kampala yamefungwa na Mike Ndera, Mike Serumaga, Umar Kasumba na Godfrey Lwesibawa. Sasa JKU itabidi ishinde 5-0 wiki ijayo Uwanja wa Amaan, Zanzibar ili kusonga mbele.
    Matokeo haya yamepokewa kwa furaha na mashabiki kwanza wa timu hizo na pili Watanzania kwa ujumla wapenda michezo.
    Hakika ni jambo la kufurahisha sasa mashabiki wa nyumbani watakwenda kwa mbwembwe wikiendi ijayo kwenye viwanja vya Azam Complex, Chamazi na Taifa, Dar es Salaam kuzishangilia timu zao.
    Soka ni mchezo wa furaha, na hususan pale timu yako inapofanya vizuri – lakini hugeuka kuwa mchezo wa machungu pale timu yako inapogeuzwa kisusio.
    Pamoja na kuwapongeza Azam na Yanga kwa matokeo mazuri kwenye mechi za awali jana, nataka niwakumbushe kitu.
    Mwaka 1979, Simba ilifungwa mabao 4-0 na Mufulira Wanderers ya Zambia katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati huo ikijulikana kama Klabu Bingwa Afrika.
    Mufulira wakaona wamemaliza kazi Dar es Salaam na kuelekea mchezo wa marudiano wakabweteka, wakiamini 4-0 ni ushindi mkubwa Simba hawawezi kupindua matokeo.
    Wakati Mufulira wanarejea Zambia kusubiri mchezo wa marudiano, huku nyuma Simba wakajifungia kwenye kambi yao na kujiuliza, kisha kufanya mazoezi kwa bidii kujiandaa kwa mchezo wa marudiano.
    Mufulira hawakuamini macho yao siku ya mchezo wa marudiano pale Lusaka, walifungwa mabao 5-0, Thuwein Ally pekee akifunga matatu na kutolewa katika michuano.
    Bahati mbaya Simba nayo haikuvuka Raundi ya Pili, baada ya kutolewa na Racca Rovers kwa jumla ya mabao 2-0, ikilazimishwa sare ya 0-0 Dar es Salaam kabla ya kwenda kuadhibiwa ugenini.
    Na soka ndivyo ilivyo – pale unapofanya kosa tu, mpinzani wako anaweza kutumia vizuri na yakatokea matokeo ambayo kwako yatakuwa ajabu.
    Kwa nini nimewakumbusha hili Azam na Yanga – nataka wasibweteke baada ya matokeo mazuri ya awali, ili yasije yakawatokea kama ya Mufulira kwa Simba mwaka 1979 katika michuano kama hiyo ya Afrika. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HONGERA YANGA NA AZAM, LAKINI SOMO LA MUFULIRA WANALIJUA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top