• HABARI MPYA

  Thursday, March 10, 2016

  MICHO: NI WAKATI WA MALIPO YANGA, WANA TIMU NZURI KWA LIGI YA MABINGWA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa timu ya taifa ya Uganda, Milutin Sredojevic ‘Micho’ (pichani kushoto) amesema kwamba umewadia wakati wa mashabiki wa Yanga kulipwa furaha kwa mapenzi yao makubwa kwa timu hiyo.
  Micho alikuwa anaizungumzia Yanga kuelekea mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, APR Jumamosi, Uwanja wa Amahoro mjini Kigali Rwanda. 
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE kwa simu leo kutoka Uganda, Micho amesema kwamba hii ni nafasi nzuri kubwa ya kwanza kwa Yanga kuwania kufika mbali kwenye michuano ya Afrika tangu mwaka 2007.
  Amesema mwaka 2007 alipokuwa kocha wa Yanga, walifanikiwa kuitoa Petro Atletico ya Angola katika Raundi ya Kwanza na kwenda hatua ya mwisho ya mchujo, ambako walitolewa na Esperance ya Tunisia, hivyo kucheza la El Merreikh ya Sudan kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako walitolewa pia.
  “Bahati nzuri ni kwamba sasa hivi Yanga ina wachezaji wazuri zaidi, ambao sikuwa nao wakati ule, lakini nilijitahidi kutengeneza timu nzuri kwa wachezaji wale wale na tukafika tulipoishia,”amesema Micho na kuongeza.
  “Yanga sasa ina wachezaji wazuri wenye uzoefu mkubwa wa kimataifa na labda sasa ni wakati ambao mashabiki watalipwa fadhila kwa mapenzi yao makubwa kwa timu,”amesema.
  Micho amesema Yanga kwa sasa ina kikosi bora kinachopaswa kuwalipa furaha mashabiki kwa mapenzi yao kwenye timu

  Micho amesema mechi baina ya timu hizo ambazo baada ya Jumamosi Amahoro, zitarudiana wiki moja baadaye Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam itakuwa ni vita kubwa kwa sababu inakutanisha timu zinazofahamiana.
  “Utakuwa mchezo wa ushindani mkubwa mwisho wa siku timu ambayo itakuwa imewekeza zaidi kwenye maandalizi mazuri kwa ujumla ndiyo itashinda,”amesema Micho.
  Kocha huyo Mserbia amesema kwamba akiwa amekwishafanya kazi Tanzania ambako alifundisha Yanga na Rwanda alikokuwa kocha wa timu ya taifa, hawezi kupendelea upande wowote katika maoni yake.
  “Nina furaha kwamba timu mbili kubwa zimesonga mbele, lakini bahati mbaya timu moja tu ndiyo itasonga mbele kwenda Raundi nyingine kuwania kucheza hatua ya makundi ya Ligi Mabingwa Afrika, ambako wakikosa watahamia kwenye mchujo wa kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho,”amesema Micho.
  Kocha huyo wa zamani wa SC Villa ya Uganda, amesema kwamba timu zote zimewekeza katika ujenzi wa vikosi imara, Yanga ikiundwa na mseto wa wachezaji wakiwemo wa kigeni, wakati APR ina wachezaji wengi wa nyumbani na ambao ni tegemeo la timu ya taifa ya Rwanda.
  “Wachezaji wa APR hivi karibuni walikuwa timu ya taifa ya Rwanda ambayo ilicheza michuano ya CHAN na kufika Robo Fainali, dhahiri watakuwa wamepata uzoefu mzuri utakaowasaidia kufanya vizuri kuisaidia klabu yao,”.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MICHO: NI WAKATI WA MALIPO YANGA, WANA TIMU NZURI KWA LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top