• HABARI MPYA

  Sunday, March 13, 2016

  MALINZI AUAMBIA MKUTANO MKUU TFF; "TUMEIWEKA PAZURI SOKA YA TANZANIA"

  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) jana limefanya mkutano wake mkuu katika hoteli ya Regal Naivera jijini Tanga, huku mkuu wa Mkoa wa Tanga Mwantumu Mahiza akiwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano huo utakaomalizika kesho kwa shughuli ya uwekaji jiwe la msingi katika eneo la kukuzia vipaji mjini humo.
  Ifuatayo ni Hotuba ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi
  Rais wa TFF, Jamal Malinzi (kushoto) akiwa na Rais wa FIFA, Gianni Infantino kulia

  "Ndugu Mweshimiwa mgeni rasmi, mh Mwantumu Mahiza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Ndugu wajumbe wenzangu wa Mkutano Mkuu. Ndugu wageni waalikwa.
  Salam aleikum, Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa ajili ya aliyotujalia na kutufanikisha kuwepo hapa leo. Ni kwa Rehema zake Mwenyezi Mungu tumeweza kujumuika hapa leo.
  Ninaomba nichukue fursa hii kuwaomba wote tusimame ili kuwarehemu waliotangulia mbele ya haki.
  Ndugu zangu, kama mnavyofahamu tarehe 25/10/2015 nchi yetu ilifanya Uchaguzi Mkuu. Nichukue fursa hii kumpongeza Rais wetu Mpendwa Dr John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wetu pamoja na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu. Pongezi za pekee ni kwa Mh. Nape Nnauye kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo na Mh Anastacia Wambura kuwa Naibu Wake.
  Pongezi za kipekee kwa wanafamilia ya mpira wa miguu Tanzania ambao wamepata nyadhifa kama ifuatazo:
  1.  Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa, ameshinda nafasi ya ubunge wa jimbo la Ruangwa na pia kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.
   2. Mstahiki  Paschal Kihanga, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Mkoa wa Morogoro, alishinda udiwani na pia amepata wadhifa wa Meya wa Manispaa ya Morogoro.
  3. Mh John Kadutu  mjumbe wa mkutano mkuu toka Mwanza,  ameshinda ubunge jimbo la Ulyankulu.
  4.  Mh. Maftah Nachuma Katibu wa Chama cha Mpira wa miguu Lindi vijijini ameshinda nafasi ya ubunge jimbo la Mtwara Mjini.
  5. Mh. Leonard Kiganga Bugimala, Mwenyekiti klabu ya Geita Gold Sport amechaguliwa kuwa Mwenyekiti Halmashauri ya mji wa Geita na Makamu wake Mh. Costantian Mdindi pia amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.
  6. Mh. Khalid Mohammed Abdallah Mjumbe  wa Kamati ya Utendaji TFF ameshinda nafasi ya udiwani.
  7. Mh  Yusuf  Kitumbo Mwenyekiti chama cha mpira mkoa wa Tabora, ameshinda udiwani.
  8.  Mh. Golden  Sanga, Mwenyekiti chama cha mpira mkoa wa Ruvuma, ameshinda udiwani.
  9. Mh. Bartholmeo Kimario,  Mwenyekiti chama cha mpira mkoa wa Singida, ameshinda udiwani.
  10. Mh. Omari Kinyento, mjumbe wa Mkutano Mkuu toka Singida ameshinda udiwani.
  11.  Mh. Omar Gindi, Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira Mkoa Kigoma ameshinda Udiwani.
  12.  Mstahiki James Bwire, Mshirika wa TFF, Mkurugenzi Alliance School kwa kuchaguliwa udiwani na umeya jijini Mwanza.
  Tunampongeza pia Makamu wa Rais wa TFF, Ndg Wallace Karia kwa kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba.
  Ushindi huu ni heshima kubwa kwa familia ya mpira wa miguu Tanzania na unaonyesha jinsi gani watanzania wanathamini na kuenzi mpira wa miguu.
  Viongozi wetu hawa tunawaombea mafanikio katika kutimiza majukumu yao.
  Ndugu wajumbe wenzangu wa Mkutano Mkuu, ninawapeni pole sana kwa usumbufu uliotokana na kuahirishwa Mkutano wetu wa tarehe 19-20 Desemba mwaka jana, hii ilitokana na sababu ambazo tulizieleza wakati huo. Ufumbuzi wa matatizo yetu na mamlaka za kodi unaendelea kutafutwa. Ninawashukuru sana kwa kuitikia wito wa Kamati yetu ya utendaji wa kuhudhuria mkutano mkuu  huu muhimu ulioitishwa kwa mujibu wa Katiba yetu.
  Ninaomba nichukue fursa hii kutoa taarifa ya mambo muhimu ambayo uongozi wetu umeyatekeleza kati ya kipindi tulichokutana mwezi Machi mwaka jana mjini Morogoro hadi sasa. Kama nilivyotoa  rai kwenye mkutano wetu wa Morogoro, ninaomba tuyapitie, tuyajadili na kuangalia wapi utekelezaji haukuwa mzuri ili changamoto hizo ziweze kufanyiwa kazi. Azma yetu ni kuhakikisha mpira wa Tanzania unakua na sisi tunafikia lengo la kutoa upinzani wa kutosha katika hatua za Kimataifa kuanzia ukanda wetu wa CECAFA, Afrika  na hatimae kung’ara duniani.
  1. Timu ya Taifa (Taifa Stars)
  Baada ya timu yetu ya Taifa , Taifa Stars kutofanya vizuri katika michuano ya COSAFA huko Afrika Kusini mwezi Mei mwaka jana na baadae kufanya vibaya katika  mchezo wa kwanza katika mtoano wa mashindano ya CHAN,Kamati  ya Utendaji ya TFF ilichukua maamuzi ya kusimamisha ajira ya kocha wa kigeni Martin Nooj na badala yake kuingia mkataba na makocha wazawa Boniface Charles Mkwasa akisaidiana na Hemed Morocco. Tangu walimu hawa wemechukua timu ya Taifa imeboreka na hadi sasa  tumefungwa mechi mbili tu za mashindano dhidi ya Algeria na Malawi ugenini, tumetoka sare mbili nyumbani dhidi ya Nigeria na Algeria na kuifunga Malawi nyumbani.
  Aidha timu ya Kilimanjaro Stars chini ya kocha Abdalla Kibadeni na msaidizi wake Juma Mgunda katika mashindano ya CECAFA Challenge katika mechi nne ilizocheza Ethiopia haikufungwa hata mechi moja katika “Open Play” ingawa ilitolewa kwa penati tano tano katika hatua ya nusu fainali. Kipindi chote ambacho tumekuwa na makocha wazawa kiwango cha Tanzania FIFA kimekuwa kikipanda mara zote. Tunawapongeza sana makocha wetu hawa na benchi la ufundi.
  Kwa sasa tunajiandaa na mechi  za kufuzu kucheza fainali za Afrika AFCON 2017 nchini Gabon. Mechi hizi ni dhidi ya Tchad tarehe 23/03/2015 ugenini Ndjadema na mechi ya marudiano  Dar es Salaam tarehe 28/03/2015. Imani yetu ni kuwa timu yetu itaendeleza wimbi la ushindi. Katika kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Nigeria Taifa stars iliweka kambi nchini Uturuki na pia timu iliweka kambi Afrika kusini kujiandaa na mechi dhidi ya Algeria. Kambi hizi zimesaidia sana kuimarisha timu yetu kabla ya mechi hizi kubwa mbili.
  2. Timu ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars.
  Timu yetu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars chini ya kocha Rogasian Kaijage ilifanikiwa kuitoa  Zambia na hivyo kufuzu kucheza fainali za michezo ya Afrika nchini Kongo Brazaville. Katika fainali hizi Tanzania ilifungwa na Ivory Coast na Nigeria na kutoka sare na Congo, hivyo kutolewa katika hatua za makundi. Uzoefu uliopatikana katika mashindano hayo umempa fursa kocha mpya wa Timu ya Twiga stars Bi Nasra kuweza kuunda kikosi kipya kichanga ambacho majuzi kilitoa changamoto kwa timu ya Zimbabwe, imani yetu ni kwamba hii timu itafanya vizuri mechi ya marudiano mjini Harare. Aidha timu ya Twiga stars ilipata mechi moja ya majaribio dhidi ya Malawi.
  3. Udhamini na Michuano Mipya.
  Ninayo furaha kuwajulisha wajumbe wenzangu wa  mkutano mkuu kuwa katika kipindi hiki tumefanikiwa katika maeneo yafuatayo:
  3.1 Kufufuliwa Kombe la Shirikisho.
  Kwa kushirikiana na mdhamini Azam Sport Kombe la Shirikisho limefufuliwa na kuboreshwa. Kwa mwaka  huu tumeanza na timu 64 ambazo ni za ligi  Kuu (16), Ligi daraja la kwanza FDL (24) na Ligi daraja pili SDL (24). Ili  kupanua uwigo  wa ushiriki wa Mikoa kwa misimu ya usoni timu mabingwa wa mikoa (RCL) nazo zitashirikishwa katika mashindano haya ili kila mkoa wa Tanzania ushiriki katika mashindano haya. Kwa sasa mashindano haya yako hatua ya robo fainali na yana ushindani mkubwa. Inatia moyo kuwa mpaka hatua hii bado kuna timu moja ya ligi daraja la kwanza ya Geita Gold ambayo bado inapambana. Bingwa wa Kombe hili atawakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho la Afrika.
  3.2 Udhamini Ligi Daraja la Kwanza.
  Tumefanikiwa kupata udhamini wawili  kwa ligi daraja la kwanza FDL. Tumempata STARSTIMES ambaye ndiye mdhamini mkuu wa ligi na pia kampuni za Television ya  Sahara Media kupitia STAR TV imepewa haki za kuonyesha mechi hizi moja kwa moja. Haya ni mafanikio makubwa kwa ligi ya Daraja la kwanza kwani pia soko la wachezaji hawa litapanuka kwa kuwa wanaonekana moja kwa moja  na pia itakuza jina la ligi lenyewe. Changamoto ya vilabu kucheleweshewa malipo ya udhamini tumeliona na tunalifuatilia kwa karibu kupata ufumbuzi ili lisitokee tena.
  3.3 Mkataba wa Vodacom na Ligi Kuu.
  Kampuni ya Vodacom baada ya mzungumzo marefu tuliafikiana na kusaini mkataba mwingine wa miaka mitatu wa udhamini wa Ligi Kuu wenye  ongezeko la thamani ya udhamini kwa asilimia 40%. Jitihada zimefanyika kuvutia wadhamini wengine nao waje waongeze udhamini kwa ligi kuu.
  Tunashukuru mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF  umeitikia wito. Vilabu vya Ligi Kuu na ligi Daraja la Kwanza navyo vimeongeza jitihada za kupata wadhamini, tunayashukuru makampuni ya  madini ya ACACIA (Stand United)) na Geita Gold Mining (Geita Veterans) kwa kujitolea kusapoti mpira. Tunazidi kutoa wito kwa makampuni mengine yajitokeze kutoa udhamini ikiwa ni sehemu ya kutangaza biashara zao.
  3.4 Udhamini Tarajiwa.
  Tunatarajiwa kupata wadhamini kwa ajili ya Ligi Kuu ya vilabu vya wanawake (Women Premier League) pamoja na ligi ya vilabu vya Ligi Luu ya vijana chini ya umri miaka 20 (U20).
  Jambo hili likifanikiwa matumaini yetu ni kuwa tutaanzisha ligi mpya mbili, ya vilabu vya wanawake Women Premier League na ya vilabu vya Ligi Kuu kwa vijana umri chini ya miaka 20. Hii itasaidia sana kuinua kiwango cha mpira wetu kwa wanawake na wanaume.
  4. Soka la Vijana.
  4.1 Fainali za Afrika za vijana U17 mwaka 2017.
  Kikosi chetu cha Taifa cha vijana chini ya umri wa miaka 17 (U17) kinachojiandaa na hatua za mtoano mwezi juni, 2016 ilikuwa kifanye ziara ya kimichezo kwenda Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya. Lengo lilikuwa ni kukipatia kikosi hiki uzoefu wa kimataifa. Wakati tayari kikosi kimejiandaa na kukabidhiwa bendera, akaunti za TFF zilifungiwa na TRA na hivyo safari kuvunjika kwa ukosefu wa fedha. Pamoja na changamoto hiyo mpango mkakati umefanyika na sasa kikosi hiki kitacheza moja ya kirafiki ya kimataifa hapa Tanzania mwezi April na baadae kwa hisani ya Chama cha Mpira cha India timu itakwenda India kuweka kambi ya wiki tatu tayari kwa kuikabili Seychelles mwezi Juni. Tunakishukuru Chama cha Mpira cha India pamoja na serikali ya India kwa kutupatia sapoti hii.
  4.2 Fainali za Afrika U17 mwaka 2019.
  Maandalizi ya fainali hizi ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji yanaendelea vizuri na vikao na Wizara tayari vimeanza kwa ajili ya kufanya maandalizi muhimu ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo. Pia maandalizi ya timu itakayoshiriki fainali hizi yameanza kwa vijana umri chini ya miaka 13 (U13) kujumuisha pamoja katika shule ya Alliance mjini Mwanza. Mwalimu Kim Poulsen tumemleta mahsusi ili pamoja na majukumu mengine, atuandalie kikosi cha ushindi cha vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019.   Imani yetu ni kuwa Tanzania tutafanikiwa kuandaa mashindano mazuri mwaka 2019 na pia kunyakua kombe hili.
  4.3 Mashindano ya Olimpiki Tokyo 2020
  Tumedhamiria kushiriki fainali za Olimpiki Tokyo mwaka 2020. Ili kufanikisha lengo hili zoezi la kuwapata vijana wenye umri stahiki (waliozaliwa mwaka 1997 na kuendelea) limeanza. Chini ya uangalizi wa Kocha Poulsen tunaamini tutaweza kujenga kikosi imara cha kufaulu kushiriki fainali hizi.
  Kwa kuweza kujenga vikosi imara vya U17 mwaka huu na mwaka 2019 na pia kuwa na timu nzuri ya Olimpiki Tokyo 2020 imani yetu ni kuwa hiki kizazi tunachokijenga na kukikuza ifikapo  mwaka 2026 kitaweza kutuvusha tucheza fainali za kombe la dunia inshallah.
  4.4  Vituo vya mikoa vya kukuza na kuendeleza vipaji.
  Kama nilivyoainisha kwenye mkutano wa mwezi Machi mjini Morogoro, azma ya  TFF ni kuhakikisha kuwa kila chama cha mpira wa miguu cha mkoa kinakuwa na kituo mama cha kukuza na kuendeleza vipaji vya mpira. Mkataba wa mfano (template) umekwisha pelekwa mikoani ili vyama vya mikoa kama havina vituo vyake basi viingie mkataba wa ushirikiano na kituo kimoja kwa lengo la kukifanya kiwe kituo mama cha Mkoa. Kupita vituo hivi TFF itaweza kuratibu shughuli za maendeleo ya mpira wa vijana katika mikoa yetu na  kuongeza nguvu kwa kuvipatia vifaa na walimu.
  Mipira 5000, koni 3000, na beeps 2000 tayari vimeagizwa toka nje ya nchi kwa kutumia vyanzo vya fedha vya TFF yenyewe bila kuomba msaada kwa ajili ya kuendeleza program hii. Tayari kila mkoa una mwalimu angalau mmoja aliyefanya kozi ya FIFA ya ukocha  isipokuwa mikoa miwili tu Manyara na Njombe. Hivyo mtaji wa kutosha tunao wa kuanzisha vituo hivi. Shime viongozi wenzangu wa mikoa tujidhatiti tuweke nguvu katika uwanzilishaji na uendelezaji wa vituo hivi ambavyo vitakuwa chachu kuu ya kutoa wachezaji wa Taifa wa kike na wa kiume.
  Imani yetu ni kuwa vituo hivi vikiimarika vitakuwa ni chachu ya kuendeleza vituo vingine ambavyo vitamilikiwa na vyama vya mpira vya wilaya, vilabu, taasisi binafsi, mashule nk. Kwa utaratibu baadae tutaweza kuwa tunaratibu mashindano kati ya vituo hivyo ngazi ya wilaya, mikoa, kanda na hatimae Taifa ili tuweze kutafuta wachezaji bora wa kuimarisha timu zetu na hatimae kuwa na timu za kuleta mafanikio Kimataifa kwa siku zijazo.
  Tunashukuru tumeweza kupata ardhi yetu wenyewe katika mikoa ya Tanga na Manyara. Ninarudia kutoa wito kwa viongozi wote wa mikoa tuzidi kukamata ardhi mikoani kwetu ili hatimae tuweze kujenga vituo vya kukuza na kuendeleza vipaji, centres of excellency.
  5. Kozi mbali mbali.
  Kwa kushirikiana na CAF na FIFA Shirikisho letu limeandaa kuratibu na kutoa kozi mbali mbali za waamuzi na makocha katika ngazi mbali mbali. Jitihada kubwa zimefanyika kuhakikisha mikoa iliyokuwa na hazina ndogo ya makocha na waamuzi inapewa fursa ya kuratibu kozi hizi. Tunashukuru viongozi wote wa mikoa na wilaya ambao tumeshirikiana nao kutimiza azma hii. Juhudi zinaendelea ili tuweze kupata kupata makocha, waamuzi, madaktari wa michezo na watawala bora na wengi zaidi. Ninatoa rai kwa wakinamama wazidi kujiunga katika kozi hizi maana wana umuhimu wa kipekee katika maendeleo ya mpira hasa wa wanawake.
  6.  Vilabu.
  Pamoja na jitihada za kutafuta wadhamini wa mashindano mbalimbali yanayohusisha vilabu, jitihada pia zinaendelea kufanyika kuhakikisha vilabu vyetu vinaimarisha utawala bora. Kufuatia CAF na FIFA kuanzisha utaratibu wa kutoa leseni kwa vilabu (Club Licencing) jitihada sasa zinafanyika kuhakikisha vilabu vinaelimishwa kwa kina juu ya mahitaji ya leseni hizi. Katika utaratibu wa leseni za vilabu, vilabu vyetu sasa vitalazimika kuwa na ofisi,  kuwaajiri watendaji wakiwemo makatibu na watunza kumbukumbu za mahesabu, kuwa na maeneo ya kufanya mazoezi, kuwa na program ya maendeleo ya mpira wa vijana, kuajiri walimu wenye sifa nk. Tunaamini utaratibu wa leseni za vilabu ukitekelezwa ipasavyo uendeshaji wa vilabu vyetu utaboreshwa na hivyo kuongeza tija kwa vilabu vyetu.
  7.   Kitega uchumi Karume.
  Jitihada za kuendeleza kiwanja chetu uwanja wa Karume, kama tulivyoahidi, zinaendelea. Tayari tumekwisha malizia kujenga chumba ambacho kitakuwa ni duka la TFF la kuuzia vifaa vya michezo na pia ujenzi wa chumba kingine utakapowekwa mgahawa unaendelea. Kwa sasa tunashugulikia kupata mashine ya TRA ya tozo ya kodi (EFD machine) ili tuweze kufungua duka letu la vifaa vya michezo.
  8.  Tiketi za Elektroniki.
  Kutokana na matatizo yaliyojitokeza matumzi ya tiketi ya elektronik yalisimamishwa na mmiliki wa uwanja wa Taifa ambaye ni Serikali. Baada ya mazungumzo na mwenye mkataba  ambaye ni Benki ya CRDB ilikubaliwa apatikane mshauri mtaalam wa kupitia mfumo mzima na kupendekeza marekebisho. Baada ya tenda kutangazwa mtaalam amepatikana na sasa anasubiriwa aanze kazi hiyo. Lengo ni kuhakikisha utaratibu wa tiketi za elektronik unaanza kutumika msimu ujao wa ligi.
  9.  Mfuko wa maendeleo ya mpira (Football Development Fund).
  Baada ya mfuko huu kuanzishwa kikatiba katika mkutano mkuu uliopita, kamati ya utendaji ya TFF iliteua wajumbe wa kamisheni ya uendeshaji wa mfuko  huu chini ya mwenyekiti Ndugu Tido Mhando. Lengo la mfuko huu kama ilivyoanishwa ni kuwa chanzo kikuu cha kupata rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa  miguu nchini mwetu. Ninaomba tuwaunge mkono na kuwapa ushirikiano watendaji wa mfuko huu huku tukitambua kuwa maendeleo ya mpira wa miguu yanahitaji rasilimali nyingi.
  PONGEZI MAALUM
  Ninaomba nichukue fursa hii kumpongeza tena Bwana Gianni Infantino kwa kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa FIFA. TFF tulishiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uchaguzi huu. Tunaamini chini ya uongozi wake mabadiliko makubwa chanya yatatelezwa katika mpira wetu.
  Aidha nirudie tena kumpongeza kijana wetu Mbwana Samatta kwa kuteuliwa kuwa mwanamichezo bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani ya bara letu na pia kwa kufanikiwa kupata fursa ya kucheza katika ligi kuu ya Ubelgiji. Tunazidi kumuombea na kumtakia mafanikio.
  Ndugu wajumbe wa Mkutano Mkuu baada ya kuyasema haya ninaomba nirudie kuwashukuru wote kwa kuhudhuria kwenu mkutano huu, ninaomba Mola aubariki Mkutano wetu ili tutakayojadili na kukubaliana yawe ni ya kheri na yajenge mpira wetu. Ahsanteni sana,".
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MALINZI AUAMBIA MKUTANO MKUU TFF; "TUMEIWEKA PAZURI SOKA YA TANZANIA" Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top