• HABARI MPYA

    Saturday, October 10, 2015

    YANGA SC: BOSSOU NA COUTINHO WOTE NI WACHEZAJI WA KOCHA, UONGOZI HAUHUSIKI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    UONGOZI wa Yanga SC umesema kwamba beki Mtogo, Vincent Bossou na kiungo Mbrazil, Andrey Coutinho wote wamesajiliwa kwa mapendekezo ya kocha wao Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORT- ONLINE jana mjini Dar es Salaam, Katibu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha amesema kwamba wachezaji wote hao ni pendekezo la kocha.
    Dk. Tiboroha amesema kwamba wakati klabu inamrejesha Pluijm Januari mwaka huu, alikuta Wabrazil wawili, wote viungo Emerson de Oliveira Neves Roque na Coutinho naye akaamua kuacha mmoja na kubaki na mmoja.
    Vincent Bossou (katikati) amecheza mechi moja tu dhidi ya Mbeya City, tena ya kirafiki kwa dakika 45 tangu amesajiliwa Yanga SC Agosti

    “Na ndipo aliamua abaki na Coutinho. Na hata katika usajili wa msimu huu, kocha aliafiki aachwe beki Zuttah (Joseph) wa Ghana, ili abaki Coutinho. Sasa kwa nini hamtumii, sisi hatuwezi kumuingilia katika programu zake,”amesema.
    Aidha, Katibu huyo amesema kwamba alipoletwa beki Bossou alipelekwa kwenye kambi ya Tukuyu Mbeya kwa majaribio ya wiki mbili na kocha akaridhishwa na uwezo wake na kuagiza asajiliwe.
    “Lakini bado uongozi unanyooshewa kidole juu ya usajili wa hawa wachezaji. Mimi nadhani Waandishi wa Habari bora wakamuulize kocha, tena anaweza akawapa sababu nzuri tu,”.
    “Sisi tulimuuliza, akasema ana wachezaji wengi na wote wazuri, kila mmoja atacheza wakati ukifika. Akatupa mfano Busungu (Malimi), naye alikuwa anakaa benchi, lakini baada ya kuingia katika mechi na Simba na kufunga bao na kuseti lingine, mechi iliyofuata alianza. Na labda mechi ijayo pia ataanza,”amesema Tiboroha.
    Katibu huyo amesema uongozi hauwezi kumuingilia kocha katika upangaji wa timu na hususan wakati ambao timu inacheza vizuri na kushinda.
    Andrey Coutinho alikuwa ana wakati mzuri chini ya kocha Mbrazil mwenake, Marcio Maximo kabla ya kuanza kusugua benchi chini ya Mholanzi, Plujm

    “Watu watakuona chizi, kuhoji kocha kwa nini hampangi nani wakati timu inashinda kila mechi na kucheza soka ya kuvutia. Mimi nadhani tuwe na subira,”amesema.
    Vincent Bossou amecheza mechi moja tu dhidi ya Mbeya City, tena ya kirafiki kwa dakika 45 tangu amesajiliwa Yanga SC Agosti, mwaka huu, wakati Coutinho alikuwa ana wakati mzuri chini ya kocha aliyemsajili, Mbrazil mwenzake, Marcio Maximo kabla ya kuanza kusota benchi chini ya Pluijm.
    Winga huyo Mbrazil hadi sasa ameichezea Yanga SC jumla ya mechi 35 na kufunga mabao saba, nyingi akitokea benchi kipindi cha pili mwishoni.  
    Yanga SC kwa sasa wanaendelea na mazoezi mjini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, Oktoba 17, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC: BOSSOU NA COUTINHO WOTE NI WACHEZAJI WA KOCHA, UONGOZI HAUHUSIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top