• HABARI MPYA

    Monday, October 19, 2015

    MAVUGO ‘WA SIMBA’ AGONGA ZOTE MBILI BURUNDI YABISHA HODI CHAN 2016

    TIMU ya Burundi imekuwa miongoni mwa nchi saba zilizoanza vyema mechi za kwanza za hatua ya mwisho ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) mwaka 2016 nchini Rwanda.
    Asante kwake mshambuliaji aliyetakiwa sana na Simba SC msimu huu, Laurent Mavugo aliyefunga mabao yote Burundi ikishinda 2-0 dhidi ya Ethiopia mjini Bujumbura na sasa Int’amba Murugamba wamejisogeza karibu na fainali za pili mfululizo za CHAN.
    Katika mechi hizo za mwishoni mwa wiki, Angola, Nigeria, Guinea, Niger, Uganda na Zambia nazo pia zimeanza vizuri michuano hiyo inayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
    Laurent Mavugo alikaribia kutua Simba SC ya Tanzania msimu huu

    Mechi tano zaidi zilitarajiwa kuchezwa usiku wa jana na jumla ya timu 16 zitacheza fainali za CHAN Rwanda kuanzia Januari hadi Februari. 
    Ikiwa imefuzu kwa mara ya kwanza mwaka jana na kushika nafasi ya tatu, Nigeria ilionekana kupania kurudia mafanikio hayo baada ya kuichapa 2-0 Burkina Faso mjini Port Harcourt, mabao ya Bature Yaro na Gbolahan Salami aliyemtungua kipa Mohammed Bailou kwa penalti.
    Uganda imejisogeza karibu na rekodi ya kucheza fainali tatu za CHAN baada ya kuichapa Sudan 2-0 mjini Kampala mabao yaFrank Kalanda na Farouk Miya katika mchezo ambao Hassan Dazo alitolewa kwa kadi nyekundu na kipa James Alitho akaokoa mkwaju wa penalti wa Mudather Eltaib.
    Zambia iliitandika Msumbiji 3-0 mjini Ndola, mabao ya Winston Kalengo na Conlyde Luchanga mawili. Angola imepata ushindi wa ugenini wa 2-0 mjini Johannesburg dhidi ya wenyeji Afrika Kusini mabao ya Mateus Da Costa na Manuel Afonso. Lakini Bafana Bafana iliathiriwa na kukosa wachezaji wake wa kikosi cha kwanza, kutokana na klabu kugoma kuwaachia kwa sababu michuano hiyo haipo katika kalenda ya FIFA.
    Guinea imeifunga Senegal 2-0, mabao ya Aboubacar Mouctar Sylla na Aboubacar Iyanga Sylla mchezo ambao ulichezwa Bamako nchini Mali, baada ya Conakry kutokana na hofu ya ugonjwa wa Ebola.
    Niger imeshinda 2-0 dhidi ya Togo mjini Niamey mabao ya Idrissa Halidou na Koffi Dan Kakowa, wakati mabingwa watetezi Libya watacheza ligi ndogo pamoja na Tunisia na Morocco wiki ijayo kuwania nafasi ya kucheza CHAN.
    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mabingwa wa CHAN ya kwanza mwaka 2009, wamefuzu bila jasho kufuatia wapinzani, Jamhuri ya Afrika ya Kati kujitoa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAVUGO ‘WA SIMBA’ AGONGA ZOTE MBILI BURUNDI YABISHA HODI CHAN 2016 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top