• HABARI MPYA

    Thursday, October 29, 2015

    CAF YATISHIA KUIFUTA ZANZIBAR KIMATAIFA, NA ITALIFUTIA MBALI KOMBE LA MAPINDUZI IWAPO…

    Na Ameir Khalid, ZANZIBAR
    SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeagiza kufutwa kwa kesi dhidi ya uongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na kurejeshwa kwa uongozi halali wa chama hicho.
    CAF imeliandikia barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kulielekeza lihakikishe kesi dhidi ya viongozi wa ZFA inafutwa na wanarejeshwa madarakani, vinginevyo Zanzibar itafungiwa katika soka ya kimataifa.
    Barua ya CAF kwa TFF ambayo BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE imefanikiwa kuipata nakala yake, pia imesema kwamba iwapo agizo hilo litakiukwa, Zanzibar itatengwa na nchi zote wanachama wa CAF na FIFA.

    Rais wa TFF, Jamal Malinzi akiwa na Rais wa CAF, Issa Hayatou

    Maana yake hakuna timu ya nje ya nchi hiyo itakayokwenda kucheza michuano ya kila mwaka ya Mapinduzi visiwani humo na Zanzibar haitaruhusiwa kucheza Kombe la Challenge wala Kagame.
    Aidha, klabu za Zanzibar pia mwakani zitapoteza haki ya kucheza michuano ya Afrika, Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa.  
    Ikumbukwe Mahakama Kuu ya Zanzibar iliwaamuru viongozi wa juu wa ZFA kuondoka madarakani na kuagiza kuundwa Kamati ya muda kwa ajili ya kusimamia shughuli za chama hicho.
    Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mkusa Isaac Sepetu, wakati akisikiliza kesi inayowakabili viongozi hao, Rais wa ZFA Ravia Idarous, Makamu wake ofisi ya Pemba Ali Mohammed pamoja na Katibu Mkuu Kassim Haji Salum, alisema kwa mujibu wa katiba ya ZFA muda wao wa kukaa madarakani umemalizika hivyo wakae pembeni.
    Jaji Sepetu pia alitoa agizo la kuundwa kamati ya muda ya uongozi wa chama hicho ambacho mbali na kesi ya ubadhirifu wa fedha, inakabiliwa na kesi mbili za kukiuka katiba na kanuni za mashindano, zilizofunguliwa dhidi yake na klabu za Chuoni SC na Aluta.
    Baada ya amri hiyo ya Mahakama, Umoja wa Klabu za Soka Zanzibar uliteua kamati ya watu saba kuandaa uchaguzi mkuu wa chama hicho ili kupata viongozi wapya.
    Waliteuliwa ni Hussein Ali Ahmada anayekuwa Mwenyekiti ambapo Makamu wake atakuwa Omar Ahmed Awadh.
    Aidha, Hashim Salum Hashim anakuwa Katibu Mkuu akisaidiwa na Khamis Hamad, wakati Masoud Attai Masoud, Salum Hamdun na Ali Ussi Jongo wanakuwa wajumbe wa kamati hiyo.
    Jongo alisema miongoni mwa majukumu makubwa ya kamati hiyo ni kuzungumza na uongozi wa klabu za Chuoni SC na Aluta, kuziomba ziondoshe kesi walizoifungulia ZFA ili mpira uchezwe na ligi zianze.
    Aidha, alisema kazi nyengine ni kuandaa utaratibu wa kufanya uchaguzi mkuu wa chama hicho ambacho kwa muda sasa shughuli zake zimekwama kutokana na kuelemewa na mzigo wa kesi mahakamani.  

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CAF YATISHIA KUIFUTA ZANZIBAR KIMATAIFA, NA ITALIFUTIA MBALI KOMBE LA MAPINDUZI IWAPO… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top