• HABARI MPYA

    Saturday, October 17, 2015

    KIPRE TCHETCHE, AISHI MANULA WAINUSURU AZAM FC KUZAMA KWA YANGA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    AZAM FC na Yanga SC zimetoshana nguvu, baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Matokeo hayo yanaifanya Yanga SC iendelee kuongoza ligi kwa wastani wa mabao, ikiwa ina pointi 16 sawa na Azam FC baada ya kila timu kucheza mechi sita.
    Mchezo huo uliochezeshwa refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga, hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa Zimbabawe, Donald Ngoma dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 45 za kipindi cha kwanza.
    Kipre Tchetche akishangilia baada ya kuifungia Azam FC bao la kusawazisha

    Ngoma alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi ya Malimi Busungu, ambaye naye alipokea mpira mrefu wa beki wa kulia, Juma Abdul, Yanga SC ikitoka kushambuliwa.
    Yanga SC ilistahili kumaliza kipindi hicho wakiwa wako mbele, kwani waliwazidi wapinzani wao katika kumiliki mpira.
    Lakini katika utengenezaji wa nafasi timu zote zililingana, Yanga SC wakipoteza nafasi mbili za wazi kama Azam FC.
    Kipa wa Azam FC, Aishi Manula alidaka shuti la Busungu dakika ya sita na dakika ya 33, Kelvin Yondan alimhadaa vizuri beki wa Azam FC, Serge Wawa Pascal, lakini Manula akaokoa. 
    Mshambuliaji Mkenya wa Azam FC, alijaribu kuunganisha kwa kichwa ha mkizi krosi ya John Bocco, lakini mpira ukaenda nje dakika ya 19 na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliingia vizuri kwenye eneo kla hatari la Yanga SC, lakini Mwinyi Hajji Mngwali akatokea na kuokoa.  
    Kipindi cha pili, Azam FC walibadilika na kuanza kucheza kwa kujiamini na mambo yalikuwa mazuri zaidi upande wao, baada ya mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche kuingia kuchukua nafasi ya Allan Wanga.
    Na ni Kipre Tchetche huyo huyo aliyekwenda kuisawazishia bao Azam FC dakika ya 82 akimchambua vizuri ‘Tanzania One’, Ally Mustafa ‘Barthez’ baada ya kupokea pasi ya Farid Mussa.
    Wachezaji wa Yanga SC wakimpongeza Ngoma (katikati) baada ya kufunga bao la kuongoza


    Kipa wa Azam FC, Aishi Manula akiokoa mpira juu ya kichwa cha Amissi Tambwe wa Yanga
    Mshambuliaji wa Azam FC, Alan Wanga akipiga kichwa cha mkizi eki dhidi ya beki wa Yanga SC, Nadir Haroub 'Cannavaro'


    Yanga SC walihamishia kambi kwenye lango la Azam FC kusaka bao la ushindi na wakafanikiwa kupata penalti dakika ya 88, lakini mkwaju wa Mzimbabwe Thabani Kamusoko ukapanguliwa na kipa Aishi Manula.
    Hata hivyo, penalti hiyo ilionekana kuwa ya utata, kwani Simon Msuva alimtoka beki, David Mwantika akamchambua kipa Aishi Manula lakini mpira ukaenda juu kidogo ya lango la Azam FC na kutuama kwenye nyavu za juu.
    Katika mastaajabu ya wengi, Refa Kambuzi akaamuru mkwaju wa penalti, ambao wachezaji wa Azam FC walipingana naye kwa dakika zaidi ya moja, kabla ya kukubali kwa shingo upande na Aishi akainusuru timu yake kuzama. 
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Kevin Yondan, Nadir Cannavaro, Mbuyu Twite/Said Juma ‘Makapu’ dk78, Salum Telela/Deus Kaseke dk89, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Malimi Busungu/Simon Msuva dk56. 
    Azam FC; Aishi Manula, Aggrey Morris, David Mwantika, Serge Wawa Pascal, Shomary Kapombe, Farid Mussa Shah Malik, Kipre Balou/Frank Domayo dk69, Himidi Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk57, Allan Wanga/Kipre Tchetche dk63 na John Bocco.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPRE TCHETCHE, AISHI MANULA WAINUSURU AZAM FC KUZAMA KWA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top