• HABARI MPYA

    Wednesday, October 28, 2015

    AKAUNTI YA KUPOKELEA CHEKI ZA WADHAMINI, YA MISHAHARA YA WACHEZAJI?

    JANA tumeripoti habari za kocha Mjerumani wa Toto Africans ya Mwanza, Martin Grelis kuachia ngazi katika timu hiyo kwa sababu mbalimbali ikiwemo wachezaji kutothaminiwa na uongozi mbovu wa timu.
    Katika barua yake ambayo BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE imefanikiwa kupata nakala yake, Grelis aliyeanza kazi Julai mwaka huu kwa kujitolea, amesema kwamba ameamua kuacha kazi baada ya kugundua hata wachezaji hawalipwi mishahara.
    Aidha, safari za ‘kigumu’ kwenda mikoa ya Tanga na Tabora katika mechi zao za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara nazo zimechangia kumfanya aachie ngazi, ingawa mwenendo wa timu si mbaya hadi sasa.

    “Kwa mwezi mzima tumefanya mazoezi ya uhakika mara saba tu, hali ambayo kocha yeyote hawezi kukubaliana nayo, nami kama kocha, imenilazimu kuchukua uamuzi huu ambao ungechukuliwa na kocha yeyote,”amesema.
    Aidha, Grelis amesema kwamba wachezaji kutothaminiwa na kwa ujumla uongozi mbovu wa timu, navyo vimemfanya ashindwe kabisa kuendelea na kazi katika timu hiyo ya Mtaa wa Kishamapanda, Mwanza.
    Hata hivyo, Grelis amesema anaamini kujiuzulu kwake kutaufanya uongozi ubadilike na kurekebisha mwenendo wake ndani ya timu, akiamini Toto ina wachezaji wazuri watakaoifanya timu iwe imara.
    “Naamini, Toto ni timu yenye wachezaji wazuri, ambao wataifanya timu iweze kushindana na timu bora na kudumu katika Ligi Kuu. Itakuwa majanga sana iwapo, uongozi utashindwa kuwatimizia wachezaji mahitaji yao, ili waweze kucheza vizuri,”amesema.
    Grelis anaiacha Toto ikiwa katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuvuna pointi 10 katika mechi nane.
    Mara ya mwisho, Grelis alikuwa kwenye benchi la Toto ikifungwa mabao 4-1 na Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na amesema matokeo hayo hayahusiani na kujiuzulu kwake.
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kiasi kikubwa limejikita kushughulikia kero na matatizo katika klabu kubwa pekee, Simba na Yanga, lakini linasahau lina wajibu huo kwa klabu zote wanachama wake.
    Ni kweli, kuna baadhi ya matatizo ni vigumu kuyajua hadi yafichuke yenyewe au kufichuliwa, kama hili la wachezaji wa Toto kutolipwa mishahara.
    Lakini TFF inaweza kuwa na kanuni madhubuti za sifa za kushiriki Ligi zake, kuanzia Ligi za mikoa, Daraja la Pili, Daraja la Kwanza na Ligi Kuu ambazo zinaweza kuepusha aina hii ya matatizo.
    Klabu ya Ligi Kuu kutokuwa na uwezo wa kulipa wachezaji wake ni matokeo ya udhaifu wa kanuni, ambazo unazipitisha kucheza Ligi.
    Miaka ya nyuma ilikuwa hatuwezi kustaajabu hata timu ya Ligi Kuu kuwa na seti moja tu ya jezi, na tena zisizotosheleza idadi ya wachezaji wa timu nzima.
    Lakini sasa ni zama nyingine, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ina wadhamini wawili, Vodacom na Azam TV- manaa yake klabu zinapata fedha za kutatua matatizo hayo madogo.
    Pamoja na hayo, udhaifu wa kanuni za Ligi Kuu bado unapitisha timu ambazo zinakwenda kufanya hata ligi yetu iwe dhaifu pia.
    Kama unakuwa na timu ambayo haijiwezi, itawezaje kwenda kucheza Ligi kwa ushindani na hapo huwezi kustaajabu kuona Toto imekuwa timu ya kupanda na kushuka, licha ya ukweli kwamba huibua vipaji vingi.
    Kocha Grelis ametufungua macho, binafsi siku zote nilikuwa ninajua Toto ni kati ya timu ambazo wachezaji wake wanalipwa kidogo, kumbe hawalipwi kabisa.
    Maana yake timu hiyo iliyopanda msimu huu haina uwezo wa kujiendesha- wakati kuna timu zilikosa nafasi ya kupanda Ligi Kuu zina uwezo wa kujiendesha.
    Mimi nadhani ni bora kuwa na Ligi ya timu nyingi za majeshi, lakini zina uwezo wa kujiendesha na kuhudumia wachezaji wake, kuliko kuwa na ligi yenye timu nyingi za mtaani, ambazo kumbe haziwezi hata kulipa wachezaji mishahara.
    Umefika wakati TFF iweke kanuni za kujijengea hadhi ligi zake kuanzia za mikoa, Daraja la Pili, Daraja la Kwanza na Ligi Kuu.
    Kwamba klabu ambayo inaingia kucheza Ligi ya Mkoa, akaunti yake iwe na kiasi fulani cha fedha, hali kadhalika kwa Daraja la Pili, Daraja la Kwanza na Ligi Kuu. Viwango vitofautiane kulingana na uzito wa Ligi.
    Lakini pia, TFF inaagiza klabu ziwe na Watendaji profesheno wa kuajiriwa- je Toto nao wana aina hiyo ya watu kwa maana ya Katibu Mtendaji, Mhasibu na Ofisa Habari.
    Tunapoambiwa watendaji wa kuajiriwa ni watu wa kuendesha ofisi ya klabu ambayo kwa sasa ni taasisi na si kitu cha kujifurahisha kama ‘Enzi za Mwalimu’, je utekelezaji wake ukoje?
    Tusiweke mbele misingi ya kulindana kwa maslahi binafsi tukasahau umuhimu wa kutunza rutuba za kustawisha soka yetu.
    Nina wasiwasi, kuna timu nyingine za Ligi Kuu hii ya msimu unaoendelea zina tatizo sawa na la Toto- sema halijafichuka tu, lakini kwa nini TFF ijiruhusu kuwa na timu za Ligi Kuu ambazo haziwezi kulipa wachezaji wake?
    Timu za Ligi Kuu zina akaunti za kupokelea cheki tu za Vodacom na Azam TV, ambazo mwisho wa siku fedha hizo huliwa na viongozi wanaoingia kuongoza klabu kwa maslahi binafsi, wakati wote akaunti hazina fedha. 
    Timu za Ligi Kuu kabla ya kusafiri zinatembeza ‘bakuli’ kwa wadau kuomba misaada, timu hazina utaratibu kwa mfano Grelis amesema Toto ilifanya mazoezi mara saba kwa mwezi mzima, inakuwaje timu ya Ligi Kuu hiyo?
    Wakati umefika TFF ianze kuzijengea hadhi ligi zake na si kufurahia kuwa na ligi nyingi, Ligi Kuu yenye timu nyingi, kumbe ni ligi dhaifu. Kwa leo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AKAUNTI YA KUPOKELEA CHEKI ZA WADHAMINI, YA MISHAHARA YA WACHEZAJI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top