• HABARI MPYA

    Friday, October 30, 2015

    KIBADENI ALALAMIKA USAJILI MBOVU CHANZO CHA MATATIZO JKT RUVU, AAHIDI KUBOMOA KIKOSI DESEMBA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA mpya wa JKT Ruvu, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ amesema kwamba kufanya vibaya kwa timu hiyo msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ni matokeo ya usajili mbovu. 
    Kibadeni jana aliiongoza JKT katika mchezo wa pili bila ushindi tangu arithi mikoba ya Freddy Felix Minziro aliyefukuzwa kwa matokeo mabaya. Na jana imefungwa 4-2 na Azam FC Uwanja wa Karume, Dar es Salaam ikitoka kutoa sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE jana, Kibadeni alisema kwamba kufanya vibaya kunatokana na udhaifu katika safu ya kiungo na ushambuliaji.
    Kocha Kibadeni (kushoto) akiwa na Msaidizi wake, Mrage Kabange

    ”Kwa sasa bado nina wakati mgumu, kwanza ukiangalia wachezaji nilionao, wote wanafanana kwa viwango, pia kukosekana kwa mshambuliaji makini kunaifanya timu ikose matokeo mazuri,”alisema.
    Kibadeni amesema anatarajia kufanya marekebisho ndani ya kikosi cha timu hiyo katika kipindi cha dirisha dogo la usajili Desemba.
    “Licha ya kutaka kufanya mabadiliko kipindi cha usajili wa dirisha dogo, nitalazimika kuwapeleka wachezaji wengi kwa mkopo ili apate nafasi ya kusajili wachezaji ambao naitawahitaji,” alisema. 
    “Ukiangalia timu hii, tayari imekemalisha idadi ya usajili wa wachezaji 30, hali hiyo itanilazimu kuondoa wachezaji waende kwa mkopo au kutumia vijana kutoka kikosi cha pili, ili tunusuru timu isishuke daraja,”alisema.
    JKT Ruvu imecheza mechi ya tisa jana ikifungwa saba na sare mbili, kati ya hizo mechi saba chini ya Minziro na mbili chini ya Kibaden aliyetoa sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar na kufungwa 4-2 na Azam jana.
    Na ndiyo inashika mkia katika Ligi Kuu ikiwa na pointi mbili, ikizidiwa moja na African Sports na tatu na Kagera Sugar. Timu nyingine zilizo katika hali mbaya ni Coastal Union yenye pointi sita, Ndanda pointi saba na Mbeya City pointi nane.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIBADENI ALALAMIKA USAJILI MBOVU CHANZO CHA MATATIZO JKT RUVU, AAHIDI KUBOMOA KIKOSI DESEMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top