• HABARI MPYA

    Friday, October 30, 2015

    YANGA SC WAWAOMBA RADHI MASHABIKI, WASEMA HAWATARUDIA MAKOSA TENA

    MECHI ZIJAZO LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA
    Oktoba 31, 2015
    Simba SC Vs Majimaji FC
    Kagera Sugar Vs Yanga SC
    Mtibwa Sugar Vs Mwadui FC
    Prisons Vs Ndanda FC
    Coastal Union Vs Mbeya City
    Novemba 1, 2015
    African Sports Vs JKT Ruvu
    Azam FC Vs Toto Africans
    Novemba 2, 2015
    Mgambo Shooting Vs Stand United
    Wachezaji wa Yanga SC wamewaomba radhi mashabiki wao 

    Na Prince Akbar, TABORA
    NAHODHA wa Yanga SC, Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ amesema kwamba wanajutia makosa ya juzi kuwaruhusu Mwadui FC kusawazisha bao dakika za mwishoni na wanawaomba radhi mashabiki wa timu yao.
    Yanga SC ilikaribia kabisa kuvuna pointi tatu juzi Uwanja wa Kambarage Shinyanga baada ya kuongoza kwa 2-1 hadi dakika 87 Mwadui FC iliposawazisha.
    Na matokeo hayo, yanawashushia nafasi ya pili mabingwa hao watetezi katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wakizidiwa kwa pointi mbili na Azam FC ambayo jana iliichapa 4-2 JKT Ruvu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
    “Kwa kweli tunawaomba radhi sana mashabiki wetu kwa makosa ambayo tulifanya juzi, lakini huo ndiyo mpira, ila tutajitahidi tusirudie makosa kama haya,”amesema.
    Cannavaro amesema kuelekea mchezo wao wa kesho dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora watawafurahisha mashabiki wao.
    Amesema wanaamini mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwa sababu Kagera Sugar ni timu ngumu na japokuwa haina matokeo mazuri, lakini si timu ya kubeza.
    Pamoja na ukweli huo, Cannavaro amesema kwamba watajitahidi wavune pointi tatu katika mchezo huo ili kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa na kurejesha imani ya mashabiki.
    Akiwazungumzia Azam FC, Cannavaro amesema kwamba wanaongoza kwa pointi mbili na ligi bado ndefu na ngumu, hivyo anaamini na wao watateleza mbele ya safari Yanga itapita.
    Yanga SC iliwasili jana usiku Tabora na leo inatarajiwa kufanya mazoezi Uwanja wa Mwinyi kuelekea mchezo wa kesho.
    Kwa ujumla Ligi Kuu inaendelea mwishoni mwa wiki, Jumamosi Simba SC ikimenyana na Majimaji FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga SC na Kagera Sugar Uwanja wa Mwinyi, Tabora, Mtibwa Sugar na Mwadui FC Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, Prisons na Ndanda FC Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Coastal Union na Mbeya City Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    Mechi nyingine zitachezwa Jumapili, Azam FC na Toto Africans Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam wakati Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, African Sports itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu wakati Jumatatu, Mgambo Shooting itaikaribisha Stand United.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAWAOMBA RADHI MASHABIKI, WASEMA HAWATARUDIA MAKOSA TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top