• HABARI MPYA

    Saturday, October 17, 2015

    YANGA SC NA AZAM FC NI ZAIDI YA MECHI, PATACHIMBIKA LEO

    REKODI YA YANGA NA AZM FC: 
    Oktoba 17, 2015
    Yanga SC Vs Azam (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    Agosti 22, 2015
    Yanga 0-0 Azam FC (Yanga ilishinda kwa penalti 8-7 Ngao ya Jamii)
    Julai 29, 2015
    Azam 0-0 Yanga SC (Azam ilishinda kwa penalti 5-3 Robo Fainali Kombe la Kagame)
    Mei 6, 2015
    Azam 2-1 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    Desemba 28, 2014
    Yanga SC 2-2 Azam (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    Septemba 14, 2014
    Yanga SC 3-0 Azam FC (Ngao ya Jamii)
    Machi 19, 2014; 
    Yanga SC 1-1 Azam FC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    Septemba 22, 2013; 
    Azam FC 3-2 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    Februari 23, 2013;  
    Yanga SC 1-0 Azam FC (Ngao ya Jamii)
    Novemba 4, 2012;  
    Azam FC 0-2 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    Machi 10, 2012; 
    Yanga SC 1-3 Azam FC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    January 07, 2012
    Azam FC 3-0 Yanga SC (Robo Fainali Kombe la Mapinduzi)
    Septemba 18, 2011;  
    Azam 1-0 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    Machi 30, 2011;  
    Yanga SC 2-1 Azam FC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    Oktoba 24, 2010; 
    Azam FC 0-0 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    Machi 7, 2010;  
    Yanga SC 2-1 Azam FC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    Oktoba 17, 2009; 
    Azam FC 1-1 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    Aprili 8, 2009;  
    Yanga SC 2-3 Azam FC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    Oktoba 15, 2008;  
    Azam FC 1-3 Yanga SC (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara)
    Nahodha wa Azam FC, John Bocco akimuacha chini beki wa Yanga SC, Kevin Yondan katika mchezo wa Ngao ya Jamii Julai mwaka huu 

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    INAPOWADIA mechi ya Simba na Yanga, hiyo ni ya wapinzani wa jadi katika soka ya Tanzania, lakini kwa sasa ‘Mechi Kubwa’ zaidi ni ile inayozikutanisha Azam FC na Yanga SC.
    Ni mechi ambayo inakutanisha washindani wa taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, timu ambazo zimekuwa zikiwakilisha nchi katika michuano ya Afrika kwa miaka mitatu mfululizo.
    Mechi ambayo inakutanisha timu zinazoaminika kuwa bora zaidi kwa sasa katika soka ya Tanzania na zinazoshikilia mataji.
    Mechi hiyo imewadia tena- na inapigwa leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, huo ukiwa mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Unazikutanisha timu ambazo zimeshinda mechi zake zote tano za awali za Ligi Kuu na zinafungana kwa pointi kileleni. Baada ya dakika 90 za mchezo huo, ama msimamo utabaki kama ilivyo iwapo zitatoka sare, au moja itapanda kileleni ikishinda.
    Azam FC wataingia uwanjani wakiwa na taji lao la ubingwa wa Klabu Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, wakati Yanga SC mabega yote yakuwa yamebeba mataji, kulia la Ligi Kuu na kushoto Ngao ya Jamii.
    Hilo ni pamoja la mabingwa- na ndiyo maana hiyo ni mechi kubwa zaidi katika soka ya Tanzania kwa sasa. 
    Kwa mwaka huu pekee hilo litakuwa pambano la nne kuzikutanisha timu hizo, baada ya awali kukutana mara tatu katika Ligi Kuu, Kombe la Kagame na Ngao ya Jamii, Azam FC ikishinda mara mbili, Yanga SC mara moja.
    Lakini ni Azam FC hadi sasa wanaoweza kutamba, baada ya kushinda mechi moja ndani ya muda wa kawaida wa mchezo, wakati nyingine walishinda kwa matuta kama Yanga. 
    Mei 6, mwaka huu katika mchezo wa kufunga dimba la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC walikabidhiwa Kombe lao wakitoka kuchapwa mabao 2-1 na Azam FC Uwanja wa Taifa.
    Julai 29, mwaka huu, timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake ikaendeleza ubabe wake kwa Yanga SC, baada ya kushinda kwa penalti 5-3 katika Robo Fainali ya Kombe la Kagame kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
    Agosti 22, mwaka huu, Yanga SC ikaanza kujiinua kwenye dimbwi la unyonge mbele ya Azam FC, baada ya kushinda kwa penalti 8-7 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 katika mchezo wa Ngao ya Jamii.
    Kocha wa Azam FC, Stewart John Hall na kocha wa Yanga SC, Mholanzi, Hans van der Pluijm wote wanauchukulia huo ni mchezo mgumu na wenye kutoa mwelekeo wa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu.
    Yanga SC wamerudia desturi yao ya kuweka kambi nje ya mji kuelekea mechi dhidi ya Azam FC na Simba SC pia, baada ya mapema wiki hii kuhamia Bagamoyo mkoani Pwani.
    Azam FC wanaojivunia hosteli na Uwanja wao wa Azam Complex, wao wameendelea kujichimbia Chamazi kwa maandalizi ya mchezo huo wiki yote hii.  
    Donald Ngoma wa Yanga SC (kulia) akimtoka Serge Wawa wa Azam FC

    TATHMINI YA MCHEZO
    Beki Serge Wawa Pascal raia wa Ivory Coast amejizolea sifa kemkem katika mechi mbili zilizopita, Kombe la Kagame na Ngao ya Jamii, kutokana na kuiongoza vizuri safu ya ulinzi ya Azam FC. 
    Na leo anatarajiwa kuendelea kuiongoza safu hiyo akishirikiana na Aishi Manula langoni, Shomary Kapombe kulia, Erasto Nyoni kushoto na Aggrey Morris katikati.
    Stewart anaweza kutumia viungo watatu leo, Himid Mao, Salum Abubakar na Mudathir Yahya au Jean Baptiste Mugiraneza, wakati safu ya ushambuliaji bali shaka ataanza na Farid Mussa, John Bocco na Kipre Herman Tchetche.
    Katika benchi wanatarajiwa kuwapo, Mwadini Ali, Said Mourad, David Mwantika, Racine Diouf, Didier Kavumbangu, Frank Domayo, Ramadhani Singano ‘Messi’ na Alan Wanga.   
    Kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ amekuwa katika kiwango kizuri siku za karibuni na leo anatarajiwa kuendelea kuanza Yanga SC, akisaidiwa na Mbuyu Twite kulia, Mwinyi Mngwali kushoto na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondan katikati.
    Pluijm naye pia anaweza kutumia viungo watatu leo, Said Juma Makapu, Salum Telelea na Thabani Kamusoko wakati safu ya ushambuliaji anaweza kuwaanzisha Simon Msuva, Donald Ngoma na Amisi Tambwe.
    Malimi Busungu pamoja na Deus Kaseke wanaweza kutokea benchi, ambako pia wanaweza kuwapo Mudathir Khamis, Juma Abdul, Vincent Bossou, Andrey Coutinho, Haruna Niyonzima na Godfrey Mwashiuya.   
    Je, ni nani ataibuka mbabe leo kati ya Azam FC na Yanga SC? Dakika 90 zitatoa jibu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC NA AZAM FC NI ZAIDI YA MECHI, PATACHIMBIKA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top