• HABARI MPYA

    Wednesday, October 07, 2015

    TAIFA STARS KUFUTA GUNDU LA MWAKA LEO? YAMENYANA NA MALAWI IKIWA HAIJASHINDA MECHI HATA MOJA MWAKA HUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TANZANIA leo wanaikaribisha Malawi katika mchezo wa kwanza wa kuwania kupangwa kwenye makundi ya kugombea tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
    Taifa Stars inakutana na Malawi leo, ikitoka kucheza mechi 11 bila kushinda. Mara ya mwisho Taifa Stars ilishinda 4-1 dhidi ya Benin Oktoba 12, mwaka jana Dar es Salaam na tangu hapo imekuwa ikichezea vichapo mfulilizo na kutoa sare.
    Stars inacheza na Malawi siku moja baada ya kocha Mzalendo, Charles Boniface Mkwasa kusaini Mkataba wa mwaka mmoja na nusu, akirithi mikoba ya Mholanzi, Mart Nooij.
    Kikosi cha Taifa Stars kilichotoa sare ya bila kufungana na Nigeria Septemba 5, mwaka huu Dar es Salaam

    MATOKEO YA MECHI 11 ZILIZOPITA ZA TAIFA STARS

    Nov 16, 2014: Swaziland 1-1 Tanzania
    Machi 29, 2015: Tanzania 1-1 Malawi
    Mei 18, 2015: Tanzania 0-1 Swaziland
    Mei 20, 2015: Madagascar 2-0 Tanzania
    Mei 22, 15: Lesotho 1-0 Tanzania
    Juni 7, 2015: Rwanda 2-0 Tanzania
    Juni 14, 2015: Misri 3-0 Tanzania
    Juni 20, 2015: Tanzania 0-3 Uganda
    Julai 4, 2015: Uganda 1-1 Tanzania
    Agosti 28, 2015: Tanzania 1-2 Libya
    Septemba 5, 2015: Tanzania 0-0 Nigeria

    Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema jana kwamba Mkwasa amesaini Mkataba wa kudumu Taifa Stars, sawa na wa mtangulizi wake, Mholanzi Mart Nooij.   
    Malinzi alimteua Mkwasa kukaimu Ukocha Mkuu Taifa Stars kwa miezi mitatu tangu Julai na akasema kwa kuanzia atakuwa anachukua mshahara alikuwa analipwa Nooij.
    Nooij aliyekuwa analipwa dola za Kimarekani 12,500 (zaidi ya Sh. Milioni 25) kwa mwezi, alifukuzwa mwishoni mwa Juni baada ya Taifa Stars kufungwa mabao 3-0 na Uganda Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika mechi ya kufuzu CHAN.
    Mkwasa aliwateua Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ kuwa Mshauri wa Ufundi, Hemed Morocco kuwa Kocha Msaidizi na Manyika Peter kuwa kocha wa makipa wakichukua nafasi za Salum Mayanga na Patrick Mwangata.
    Aidha, Omar Kapilima aliteuliwa kuwa Meneja na Hussein Swedi ‘Gaga’ kuwa mtunza vifaa vya timu- kukamilisha sura mpya kabisa ya benchi la Ufundi la Taifa Stars.
    Na tangu hapo timu imecheza mechi tatu bila ushindi ikitoa sare ya 1-1 na Uganda mjini Kampala kufuzu CHAN, ikifungwa 2-1 na Libya mchezo wa kirafiki mjini Kartepe, Uturuki na kutoa sare ya 0-0 na Nigeria.
    Hayo yalikuwa mabadiliko makubwa kutoka kwenye timu kufungwa mechi tano mfululizo na kwa ujumla kucheza mechi 11 bila ushindi chini ya Nooij.
    Taifa Stars watasafiri Ijumaa asubuhi kwenda Malawi kurudiana nao Jumapili mjini Blantyire na mshindi wa jumla ataingia kwenye Raundi ya pili ya kufuzu ambako atamenyana na Algeria.
    Atakayefuzu mtihani wa Algeria, atakuwa amefanikiwa kupangwa kwenye Kundi la kuwania tiketi ya kwenda Urusi mwaka 2018.
    Wachezaji wote wanaocheza nje, Mrisho Ngassa wa Free State Stars ya Afrika Kusini, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya DRC wapo kambini.
    Watatu hao wamekuja wakiwa katika kiwango kizuri, Ngassa akitoka kuisaidia klabu yake kufuzu Robo Fainali ya Kombe la Telkom Knockout na akina Samata na Ulimwengi wakitoka kuisaidia Mazembe kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Kila la heri Taifa Stars. Mungu ibariki Tanzania. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS KUFUTA GUNDU LA MWAKA LEO? YAMENYANA NA MALAWI IKIWA HAIJASHINDA MECHI HATA MOJA MWAKA HUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top