• HABARI MPYA

    Wednesday, October 07, 2015

    NSSF SASA IZIGEUKIE SIMBA NA YANGA, ZINATIA AIBU KWA MWELI!

    MWAKA juzi Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Crescentius John Magori alikutana na wachezaji wa klabu za Simba na Yanga SC za Dar es Salaam kuwaelimisha umuhimu wa kumiliki nyumba zao.
    Inafahamika, NSSF ina miradi ya kujenga nyumba na kuwakopesha wananchi katika mtindo wa kulipa kidogo kidogo kila mwezi.
    Tayari wananchi wengi sasa Tanzania wanaishi katika nyumba zao kutokana na miradi hiyo ya NSSF.
    Tunafahamu maisha ya wanamichezo wengi nchini huwa magumu baada ya kustaafu, kwa sababu ya maslahi madogo na gharama kubwa za maisha.
    Katika mshahara wake mdogo anaopata mchezaji wa Tanzania analazimika kulipa kodi kubwa za nyumba za Dar es Salaam, kusaidia ndugu na jamaa na kukidhi mahitaji yake mengine muhimu.

    Lakini kama atafanikiwa kupata nyumba ya mkopo ya NSSF mapema na badala ya kulipa kodi akaanza kulipa malimbikizo ya deni lake, kwa kiasi kikubwa itampunguzia mzigo katika maisha yake. 
    Niwapongeze NSSF kwa kuwafikiria wanamichezo, lakini hii isiishie kwa wachezaji wa Yanga SC, au kwa timu kubwa pekee.
    Hata wachezaji wa Azam FC, Ndanda, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Polisi, Coastal, JKT Ruvu nao wanastahili tahfifu hii katika maisha yao.
    Kwa ujumla, wanamichezo wote, wa michezo yote wanastahili elimu hii, ili nao wajue umuhimu wa kumiliki nyumba zao.
    Mpango huu wa NSSF kwa wachezaji umenifanya nifikirie mbali zaidi- hilo ni shirika lililojijengea uwezo mkubwa kutokana na uongozi bora chini ya Mkurugenzi wake Mkuu, Dk Ramadhani Dau. 
    Mafanikio ya NSSF chini ya Dk Dau na watendaji wake wengine mahiri katika shirika hilo kama Magori, wakati wote huwa yananifanya nijiulize- kama mashirika yote ya umma yangekuwa na watu wa aina hiyo, nchi hii leo ingekuwa mbali kiasi gani kimaendeleo?
    Simba SC na mahasimu wao Yanga ni klabu kongwe zenye mashabiki wengi nchini, ambazo kwa ujumla ndizo zimeshikilia soka ya Tanzania.
    Kwa miaka mingi sasa klabu hizo zinahangaika kuweza kumiliki viwanja vyao, lakini zinashindwa. Zinashindwa kwa mengi, kikubwa ni hazina uwezo wa kufanya miradi hiyo na mbaya zaidi zimekosa mipango hata ya muda mrefu ili kutekeleza hilo.
    Kilichobaki ni propaganda tu za kuwaweka sawa wanachama watulie siku ziende- lakini utekelezaji limeku3a jambo gumu kwa miaka sasa.
    Kama nilivyosema, NSSF ni shirika lenye uwezo mkubwa- naamini kabisa wakiamua, wanaweza kuzisaidia Simba na Yanga kutimiza ndoto za kuwa na viwanja vyao.
    Hizi klabu zinakopesheka, kwa sababu zinaweza kulipa tu kupitia wapenzi na wanachama wake, lakini bado kwa mapato ya kwenye mechi, Simba na Yanga zina uwezo wa kulipa si chini ya Sh. Milioni 10 kila mwezi.  
    Ni mipango tu, ambayo ndiyo inakosekana  kwa sasa ndani ya Simba na Yanga SC- lakini kama wasomi wa NSSF wakiketi meza moja na viongozi wa klabu hizo, naamini unaweza kuibuliwa mpango mmoja mkubwa na wa kihistoria.
    Simba na Yanga zinaweza kujiwekea utaratibu wa kucheza mechi moja kila mwezi na mapato yote yakaenda kwenye mfuko wa deni la NSSF.
    Ninaamini, wachezaji wa Simba na Yanga SC hawakuomba kikao na NSSF, bali shirika hilo lenyewe katika mkakati wa mradi wake liliwafikia wachezaji wa klabu hiyo.
    Hivyo basi, kwa dhamira nyingine nzuri kabisa- upo uwezekano wa NSSF kukutana na viongozi wakuu wa Simba na Yanga kujadili nao namna ya kuzisaidia klabu hizo siku moja zitimize ndoto za kumliki viwanja vyake na majengo ya kisasa. 
    Kama NSSF sasa wapo katika mchakao wa kujenga akademi ya kisasa eneo la Mwasonga, Kigamboni, Dar es Salaam- kwa nini washindwe kuzisaidia Simba na Yanga kuwa na majengo ya kisasa na viwanja pia? Ninaamini inawezekana, kwa dhamira ile ile nzuri ya kusaidia maendeleo ya michezo nchini. Siku njema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NSSF SASA IZIGEUKIE SIMBA NA YANGA, ZINATIA AIBU KWA MWELI! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top