• HABARI MPYA

    Sunday, October 04, 2015

    MKWASA ANGEKUWA KAMA MIDDENDORP, TUNGEONA MABADILIKO TAIFA STARS

    KOCHA mpya wa Free State Stars ya Afrika Kusini, Mjerumani Ernst Middendorp aliyerithi mikoba ya Mmalawi, Kinnah Phiri sasa anamtumia Mrisho Khalfan Ngassa kama kiungo mchezeshaji.
    Lakini Free State, chini ya Koch Phiri ilimsajili Ngassa kama mshambuliaji, baada ya kuvutiwa na rekodi yake ya mabao Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita akiibuka mfungaji bora.
    Lakini baada ya kurithi mikoba ya Phiri aliyefukuzwa kutokana na timu kufungwa mechi tatu zote za mwanzo Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini, Middendorp akaanza kuwatathmini kwa kina wachezaji.

    Aliwaagiza wachezaji wote waliokwenda kuchezea timu zao za taifa, warejee na video zao, ili awaone walivyozichezea nchi zao katika mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.
    Ngassa alichezeshwa nafasi ya kiungo mchezeshaji katika mchezo wa Tanzania dhidi ya Nigeria na akafanya kazi nzuri, akikaribia kufunga mara mbili.
    Baada ya Middendorp kumuona Ngassa alivyocheza vizuri katika eneo hilo, naye akaamua tangu hapo kumtumia katika nafasi hiyo pia Free State.
    Ngassa amekuwa mpishi mzuri wa mabao ya FS tangu hapo, ikishinda mechi mbili na kutoa sare moja chini ya Mjerumani huyo.  
    Hii ndiyo namna ya kocha makini anavyofanya kazi zake- hawasubiri wachezaji mazoezini tu, anawafuatilia kwa kina hata wanapokuwa kwenye majukumu ya kimataifa.
    Na hata kocha wa timu ya taifa anaweza kuwafuatilia wachezaji katika klabu zao, si kuwasubiri mazozini- huko kunaitwa kufanya kwa mazoea.
    Turudi katika utendaji wa kocha wetu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa- vipi utendaji wake?
    Akiwa kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mkwasa pia ni Kocha Msaidizi wa klabu bingwa nchini, Yanga SC- maana yake anapomaliza tu majukumu ya kitaifa, anarudi kwenye kazi za klabu.
    Huwezi kuona ni saa ngapi Mkwasa anapata muda wa kujishughulisha na Taifa Stars baada ya kumaliza mchezo mmoja.
    Yaani Mkwasa anarejea kwenye kazi za Taifa Stars pale anapoita wachezaji kwa ajili ya kambi ya mchezo unaofuata- mfano kwa sasa akiwaandaa kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Malawi kufuzu Kombe la Dunia.
    Katikati hapa Mkwasa baada ya mchezo na Nigeria amefanya nini kwa ajili ya Taifa Stars zaidi ya kuwajibika kwa mwajiri wake, Yanga SC na haishangazi hata kikosini hakuna mabadiliko.
    Sishawishiki kuamini wachezaji wote aliowaita Mkwasa katika kambi ya kujiandaa na Malawi ni ambao walifanya vizuri katika kipindi hiki- hapana.
    Kuna wachezaji katika klabu zao tu walikuwa hawachezi, mfano huyo Juma Abdul wa Yanga anayofundisha yeye mwenyewe, unawezaje kumlinganisha kiwango chake cha sasa na mtu ambaye amecheza mechi zote za klabu tangu kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu?
    Lakini pia kuna wachezaji ambao mwezi uliopita hawakufanya vizuri katika Ligi Kuu, mfano Rashid Mandawa wa Mwadui FC, lakini ‘Master’ Mkwasa amemchukua, huku ambao wamefanya vizuri kama Elias Maguri wa Stand United akiachwa.
    Inafahamika wachezaji wa kikosi cha kwanza cha timu hawabadilishwi mara kwa mara, lakini nao wanahitaji changamoto ya wachezaji ambao wanasubiri.
    Wakati Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaanza, kwenye benchi mshambuliaji wa akiba ni Mandawa ambaye hajatisha mwezi uliopita katika Ligi Kuu.
    Wazi hapa hata matumaini ya wananchi kwa timu yao yanakuwa madogo kuelekea mchezo huo na Malawi. Naamini juu ya uwezo wa Mkwasa kuanzia kwenye uteuzi wa wachezaji hadi kufundisha, lakini siamini kama kwa sasa anapata fursa ya kutosha kwa ajili ya kazi za Taifa Stars.
    Na hilo liko wazi, kwa sababu amebanwa na majukumu ya mwajiri wake, Yanga SC. Mkwasa anahitaji muda wa kufanya kazi za timu ya taifa kila siku na hapo ndipo atakapoweza kupanua wigo wake fikra na mipango yake.
    Kwa nini tukatae Mkwasa mwezi wote uliopita hajawaona wachezaji wa timu nyingne za Ligi Kuu, zaidi ya wale wa timu yake na zile nne alizokutana nazo katika Ligi Kuu kabla ya kutaja kikosi, Coastal Union, Prisons, JKT Ruvu na Simba SC.
    Na hata alipokutana na timu hizo sitaki kuamini alikuwa ana muda wa kumuangalia mchezaji wa timu pinzani, zaidi ya kuuangalia mchezo na kufikiria namna ya kuisaidia Yanga yake ishinde.
    Tumekwishajiridhisha Mkwasa ni kocha bora na mwenye sifa za kuwa kocha wa Taifa Stars, sasa vyema utaratibu ufanyike awe kocha wa timu ya taifa tu.
    Kocha Mkuu wa timu ya taifa ni ambaye anatakiwa kuwa bosi wa makocha wengine wote wa timu za vijana na kufanya nao kazi kwa ukaribu, kwa sababu huko ndiko kwenye daraja la kupandishia wahezaji timu ya wakubwa.  
    Anatakiwa afuatilie Ligi Kuu na hata Ligi Daraja la Kwanza kwa ujumla kutafuta wachezaji- je Mkwasa anapata fursa hiyo? Tusidanganyane. Haipati.
    Zama za timu za taifa kuazima makocha wa klabu zilishapitwa na wakati siku nyingi- lakini ajabu sasa timu zote za taifa nchini, ukiondoa ya wanawake inayofundishwa na Rogasian Kaijage hazina makocha rasmi.
    Bakari Shime, kocha wa timu za vijana huyo ni kocha wa Mgambo JKT, sasa kwa namna hii tunajiweka katika fungu gani kama si la wababaishaji?
    TFF, wanatakiwa kulitazama kwa kina hili na kuhakikisha timu za taifa zinakuwa na walimu wake maalum, wasio na majukumu mengine yoyote, popote. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKWASA ANGEKUWA KAMA MIDDENDORP, TUNGEONA MABADILIKO TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top