• HABARI MPYA

    Sunday, October 04, 2015

    ETOILE WAINGIA FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO, ZAMALEK YAFA KIUME, EL HILAL NAYO NJE LIGI YA MABINGWA

    HATIMAYE Etoile du Sahel imetinga Fainali ya Kombe la Shirikisho, licha ya kufungwa mabao 3-0 usiku huu na Zamalek Uwanja wa Petro Sport mjini Cairo, Misri.
    Etoile inafuzu kwa ushindi wa jumla wa 5-4, baada ya awali kuibuka na ushindi wa 5-1 nyumbani, Uwanja wa Olimpiki mjini Sousse, Tunisia.
    Etoile iliyoitoa Yanga SC katika hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo, sasa itakutana na mshindi kati ya mabingwa watetezi, Al Ahly na Orlando Pirates katika fainali ya michuano ya mwaka huu. Ahly na Pirates zinamenyana usiku wa Jumapili mjini Cairo.
    Etoile ilishindwa kuutumia mwanya wa Zamalek kucheza pungufu ya mchezaji mmoja tangu dakika ya tano baada ya mchezaji wake, Ali Gabr kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kumpiga usoni Baghdad Bounedjah.
    Kocha Msaidizi wa Etoile, Ridha Jadi alipandishwa jukwaani baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kipindi cha kwanza.
    Mabao ya Zamalek yalifungwa na Mahmoud Kahraba mawili dakika ya 12 na 55 kwa penalty baada ya Ammar Jemal kuunawa mpira kwenye boksi na bao la tatu likafungwa na Mostafa Fathi aliyetokea benchi dakika ya 70. 
    Dakika tano baadaye, Marouane Tej wa Etoile akatolewa kwa kadi ya nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
    Etoile sasa wanasubiri mshindi kati ya Al Ahly na Orlando Pirates ya Afrika Kusini

    Ligi ya Mabingwa Afrika…
    Na katika mchezo wa marudiano wa Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, USM Alger ya Algeria imelazimishwa sare ya bila mabao na El Hilal ya Sudan kwenye Uwanja wa Omar Hamadi mjini Algiers.
    Pamoja na matokeo hayo, USM Alger inakwenda Fainali, kufuatia ushindi wa 2-0 katika mchezo wa kwanza nchini Sudan.
    Wababe hao wa Algeria watakutana na mshindi kati ya TP Mazembe ya DRC na El Merreikh ya Sudan wanaomenyana kesho mjini Lubumbashi. Mchezo wa kwanza, Merreikh walishinda 2-1 Khartoum. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ETOILE WAINGIA FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO, ZAMALEK YAFA KIUME, EL HILAL NAYO NJE LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top