• HABARI MPYA

    Saturday, September 14, 2019

    SWEDI NKWABI ANG’ATUKA SIMBA SC NA KUSEMA; “KWA NDANI SI SHWARI, MUDA UTAONGEA”

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Bodi ya klabu ya Simba SC, Swedy Mkwabi ameamua kujiuzulu wadhifa huo miezi 10 na ushei tu tangu achaguliwe.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online mchana huu, Mkwabi amesema kwamba ameamua kujiuzulu kwa sababu mambo si shwari ndani ya klabu na wakati ukifika kila kitu kitakuwa bayana.
    “Vizuri nje, lakini ndani siyo vizuri kihivyo, lakini tusiseme mengi, muda utaongea mimi nimeamua tu kukaa pembeni,”alisema Mkwabi baada ya kuulizwa sababu ya kujiuliza wakati ilikuwa inaonekana wanakwenda vizuri.
    Swedy Mkwabi amejiuzulu Uenyekiti wa Bodi ya Simba SC miezi 10 na ushei tu tangu achaguliwe 

    Kuhusu kuwaacha njia panda wanachama wa Simba walimuamini na kumpa ushindi wa kishindo Novemba 5, mwaka jana, Mkwabi amesema; “Ndiyo maana tumechaguliwa sita na uchaguzi mwingine utafanyika,”.
    Taarifa ya klabu leo imesema kwamba Mkwabi ameiandikia Bodi ya Wakurugenzi kupitia Mwenyekiti wa Bodi, Mohammed ‘Mo’ Dewji akisema sababu kuu ya kijiuzulu nafasi hiyo ni kuhitaji muda zaidi kusimamia shughuli zake binafsi.
    “Bodi ya Wakurugenzi na Sekretarieti ya Simba inamtakia kila la heri katika shughuli zake, na tunatumaini kwamba ataendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za klabu kama ilivyokuwa awali kabla kupata nafasi hiyo,”.
    Na taarifa hiyo imesema kwamba Utaratibu wa kumpata Mwenyekiti mpya utatangazwa baadae. 
    Nkwabi alipita bila kupingwa Novemba 5, mwaka 2018 katika uchaguzi uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere mjini Dar es Salaam, akiwa mgombea pekee baada ya gwiji wa klabu, Mtemi Ramadhani kujitoa dakika za mwishoni.
    Katika nafasi za Ujumbe waliochaguliwa ni Hussein Kitta Mlinga, Dk. Zawadi Ally Kadunda, Suleiman Haroub Said, Mwina Mohammed Kaduguda na Asha Ramadhani Baraka.
    Uchaguzi wa Simba SC ulifuatia uongozi uliopita ulioingia madarakani Juni 30, mwaka 2014 chini ya Rais, Evans Elieza Aveva, Makamu wa Rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Wajumbe Iddi Kajuna, Said Tully, Collins Frisch, Ally Suru na Jasmine Badour kumaliza muda wake.
    Lakini Aveva na Kaburu hawakufanikiwa kumalizia muda wao madarakani, kufuatia kuwekwa rumande katika gereza la Keko tangu Juni 29, mwaka 2017 kwa tuhuma za kughushi nyaraka, kesi ambayo bado inaendelea katika Mahakama ya Kisutu mjini Dar es Salaam.
    Na Julai 1, mwaka huo, Kamati ya Utendaji iliwateua Salum Abdallah ‘Try Again’ na Iddi Kajuna kukaimu nafasi za Aveva na Kaburu na hao ndiyo waliosimamia mchakato mzima wa mabadiliko ya klabu kuelekea uchaguzi uliomuweka madarakani Mkwabi na wenzake.
    Lakini taarifa za ndani za klabu zinasema Mkwabi hakuwa na maelewano mazuri na Mwenyekiti wa Bodi ya klabu, mfanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini ambaye ameshinda zabuni ya kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SWEDI NKWABI ANG’ATUKA SIMBA SC NA KUSEMA; “KWA NDANI SI SHWARI, MUDA UTAONGEA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top