• HABARI MPYA

    Sunday, April 08, 2018

    YANGA WASIBWETEKE NA USHINDI WA JANA, BADO WANA KAZI YA KWENDA KUFANYA HAWASSA APRILI 18

    TIMU ya Yanga SC jana imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wolaita Ditcha ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kupigania tiketi hiyo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kwa ushindi huo uliotokana na mabao ya Raphael Daudi kipindi cha kwanza na Emmanuel Martin kipindi cha pili, unamaanisha Yanga SC watahitaji kwenda kulazimisha sare ugenini wiki ijayo, au kutofungwa zaidi ya tofauti ya bao moja ili kwenda hatua ya makundi.
    Daudi aliye katika msimu wake wa kwanza Yanga SC baada ya kusajiliwa kutoka Mbeya City leo alichezeshwa katika nafasi ya ushambuliaji badala ya sehemu yake ya kiungo na akafunga dakika ya kwanza tu akimalizia krosi ya beki wa kushoto Mwinyi Hajji Mngwali. 

    Bao hilo la mapema liliwajengea hali ya kujiamini wachezaji wa Yanga na kupeleka mashambulizi zaidi mfululizo langoni mwa Wolaita Dictha, lakini wakaishia kukosa mabao ya wazi.
    Lakini baadaye Wolaita wakatulia na kuanza kucheza mpira wao mzuri wa kupasiana kuanzia kwenye eneo lao hadi la wapinzani na kulitia misukosuko lango la Yanga.
    Sifa zimuendee kipa Mcameroon, Youthe Rostand Jehu aliyefanya kazi nzuri leo pamoja na mabeki wake, Andrew Vincent ‘Dante’ na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.
    Kipindi cha pili, Yanga walikianza vizuri tena na kufanikiwa kupata bao la mapema, safari hiyo winga Emmanuel Joseph Martin kumalizia kwa kichwa krosi ya kiungo wa pembeni, Yussuf Mhilu kufunga bao la pili dakika ya 54.  
    Lilikuwa bao ambalo lilizidi kuwajengea hali ya kujiamini Yanga na kuwakatisha tamaa Ditcha, hivyo mabingwa hao wa Tanzania kuzidi kuutawala mchezo, lakini wakashindwa tu kuongeza bao.
    Pamoja na hayo, Wolaita Ditcha ikiongozwa na mshambuliaji wake, Mtogo Arafat Djako ilikaribia kufunga mara mbili, kama si juhudi za kipa Rostande kuokoa michomo miwili ya hatari.
    Yanga ilipata pigo dakika ya 74, baada ya beki wake, Andrew Vincent Chikupe ‘Dante’ kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Nahodha na mkongwe, Nadri Haroub ‘Cannavaro’ aliyekwenda kumalizia vizuri akicheza na Mzanzibari mwenzake, Abdallah Shaibu ‘Ninja’.
    Timu hizo zitarudiana na Jumatano ijayo, Aprili 18 Uwanja wa Hawassa mjini Hawassa, Ethiopia na mshindi wa jumla ataingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na kuzawadiwa kitita cha sola za Kimarekani 550,000 zaidi ya Sh. Bilioni 1.1.
    Wolaita Dicha walikuwa wanacheza kwa mara ya pili kwa ardhi ya Tanzania jana, baada ya Februari kuja kucheza na na Zimamoto ya Zanzibar na kushinda kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Ethiopia.
    Ikumbukwe Welayta Dicha imefika hatua hii baada ya kuitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 3-3, kila timu ikishinda 2-1 nyumbani kwake.
    Katika Raundi ya Awali ambayo Yanga SC iliitoa Saint Louis Suns United ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Dar es Salaam na sare ya 1-1 Mahe, Welayta Dicha iliitoa Zimamoto ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Erthiopia.
    Huu ni mwaka wa tatu mfululizo, Yanga inaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na mara ya nne kwa ujumla kihiostoria.
    Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2007 ilipotolewa na na El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-0 iliyofungwa Khartoum baada ya sare ya 0-0 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Iliingia kwenye kapu hilo baada ya kutolewa na  Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao 3-0 iliyofungwa mjini Tunis, baada ya sare 0-0 Mwanza.
    Mwaka pekee Yanga ilifuzu hatua ya makundi Kombe la Shrikisho Afrika baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa ni 2016, ilipoitoa Sagrada Esperança ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 1-0 Angola.
    Hiyo ilikuwa baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kwenda kufungwa 2-1 Alexandria.
    Katika hatua ya makundi, Yanga ilipangwa Kundi moja na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), MO Bejaia ya Algeria na Medeama SC ya Ghana. 
    Yanga ilishinda mechi moja tu dhidi ya MO Bejaia 1-0 na sare ya 1-1 na Medeama Dar es Salaam huku mechi nyingine zote nne ikifungwa, zikiwemo mbili za nyumbani na ugenini na TP Mazembe.
    Mwaka jana pia Yanga baada ya kutolewa na Zanaco ya Zambia kwa mabao ya ugenini, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na 0-0 Lusaka, ikaenda kutolewa na MC Alger ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye mchujo wa kuwania tiketi ya hatua ya makundi Kombe la Shirikisho, ikishinda 1-0 Dar es Sakaam na kufungwa 4-0 Algiers.
    Mshindi wa jumla atajihakikishia kitita cha dola za Kimarekani, 550,000 zaidi ya Sh. Bilioni 1.1 za Tanzania ambazo zinaweza kuongezeka kama timu ikiingua Nusu Fainali na kuwa dola 800,000 (zaidi ya Sh. Bilioni 1.6), Dola Milioni 1.2 (zaidi ya Sh. Bilioni 2.5) kwa nafasi ya pili na Dola Milioni 2.5 (zaidi ya Sh. Bilioni 5) kwa kuchukua Kombe.
    Matokeo ya jana ni mazuri upande wa Yanga, na mazuri zaidi kwa msimu huu kwenye michuano ya Afrika, kwani hata kwenye Ligi ya Mabingwa pamoja na kukutana na timu hafifu katika hatua ya mwanzo lakini haikuwa kupata ushindi mzuri.
    Lakini pamoja na hayo, Yanga hawatakiwi kubweteka kwa matokeo haya, kwani tumeona historia ya Wolaita Ditcha ni timu ya mipango sana ambayo hesabu zake wakati wote zimekuwa kusonga mbele na imefanikiwa kufika hadi hatua hii.
    Yanga wanatakiwa kwenda kuulinda ushindi wao kwa kujiwekea malengo ya kwenda kushinda na mechi ya ugenini pia – jambo ambalo linawezekana, kwani mabingwa hao wa Tanzania hawajapoteza mechi ya ugenini msimu huu.
    Akiwa Mkufunzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), George Lwandamina ni kocha mkubwa na mwenye uzoefu wa kutosha baada ya awali kuiongoza timu ya taifa ya Zambia na Zesco United ya kwao hadi kufika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa, hivyo anajua kwamba bado ana kazi ya kufanya kwenye mechi ya marudiano Hawassa. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WASIBWETEKE NA USHINDI WA JANA, BADO WANA KAZI YA KWENDA KUFANYA HAWASSA APRILI 18 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top