• HABARI MPYA

  Wednesday, April 11, 2018

  YANGA SC YAANZA KUJITOA MBIO ZA UBINGWA, YATOKA SARE 1-1 NA SINGIDA UNITED TAIFA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MATUMAINI ya Yanga SC kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara yameanza kutoweka taratibu baada ya leo kulazimisha sare ya 1-1 na Singida United Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Sare hiyo inaiongezea Yanga pointi moja tu na kufikisha 47 baada ya kucheza mechi 22, ikizidiwa pointi tano na vinara, Simba SC wenye pointi 52 za mechi 22 pia.  
  Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Jacob Adongo wa Mara aliyesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Janeth Balama wa Iringa , Singida waliishitua Yanga kwa bao la mapema tu dakika ya kwanza, lililofungwa Mkongo, Kambale Salita.
  Wachezaji wa Singida, Kennedy Wilson (kushoto) na Mudathir Yahya wakishirikiana na kumpokonya mpira mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa aliyeanguka chini
  Mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu akimtoka beki wa Singida Miraj Adam
  Beki wa Yanga, Hassan Kessy (kushoto) akijaribu kumpita Kambale Salita wa Singida United
  Winga wa Yanga, Yussuf Mhilu (kushoto) akiria krosi mbele ya beki wa Singida United, Malik Antiri
  Kiungo wa Yanga, Raphael Daudi akimpita Kambale Salita wa Singida United

  Yanga SC walizinduka na kujaribu kusukuma mashambulizi langoni mwa Singida United, lakini washambuliaji wake, Ibrahim Ajib, Mzambia Obrey Chirwa na Yussuf Mhilu walipoteza nafasi za kufunga.  
  Singida United ilipata pigo dakika ya 37 baada ya kipa wake, Ally Mustafa ‘Barthez’ kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo. Nafasi yake ikichukuliwa na Peter Manyika Jr.
  Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm akafanya mabadiliko mengine ya lazima dakika ya 40 baada ya beki wake Mganda, Shafiq Batambuze kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na Salum Chukwu.
  Yanga ikatumia mwanya huo kupata bao la kusawazisha lililofungwa na beki Mzanzibari, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ dakika ya 45 kwa kichwa akimalizia kona iliyopigwa na Mwinyi Hajji Mngwali.
  Kipindi cha pili, Yanga walikianza vizuri na kutawala mchezo, lakini mipango yao ikaishia kwenye kushambulia tu na si kufunga, huku Chirwa akipoteza nafasi nzuri zaidi ya kufunga dakika ya 85 ya mchezo huo kwa kupiga juu baada pasi nzuri ya Yussuf Mhilu.
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mchezo mmoja, Simba SC wakiwakaribisha Mbeya City Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. 
  Sare hii inakuja siku moja baada ya kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina kuondoka jana kwenda Zambia na habari zinasema anarejea klabu yake, Zesco United ya kwao.
  Lwandamina ambaye mkataba wake unamalizika Juni mwaka huu, alijiunga na Yanga Novemba mwaka 2016 akichukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm na katika kipindi hicho ameiongoza timu katika michezo 77 ya mashindano yote akitoa sare 18, kushinda 45 kati ya hizo mbili kwa penalti baada ya sare ndani ya muda wa kawaida na kufungwa 14, tano kwa penalti baada ya sare katika muda wa kawaida.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Maji Maji imeshinda 3-1 dhidi ya Stand United Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mbao FC imeshinda 2-1 dhidi ya Njombe Mji FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Mwadui FC imeshinda 2-1 dhidi ya Lipuli FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na Tanzania Prisons imelazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Youthe Rostand, Hassan Kessy, Mwinyi Mngwali, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Kelvin Yondan, Papy Tshishimbi, Yussuf Mhilu, Pius Buswita/Juma Mahadhi dk73, Obrey Chirwa, Raphael Daud na Ibrahim Ajibu/Geoffrey Mwashiuya. 
  Singida United: Ally Mustafa ‘Barthez’/Peter Manyika dk37, Miraji Adam, Shafiq Batambuze/Salum Chukwu dk40, Kennedy Juma, Malik Antiri, Mudathir Yahaya, Deus Kaseke, Kenny Ally, Kambale Salita, Nizar Khalifan/Yussuf Kagoma dk69 na Kiggi Masaki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAANZA KUJITOA MBIO ZA UBINGWA, YATOKA SARE 1-1 NA SINGIDA UNITED TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top