• HABARI MPYA

  Thursday, April 12, 2018

  SIMBA SC YAANZA KUVUTA HEWA YA UBINGWA, YAITANDIKA 3-1 MBEYA CITY NA KUWAACHIA VUMBI YANGA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imeongeza kasi kulikimbilia taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.
  Ushindi huo unawafanya Wekundu hao wa Msimbazi wafikishe pointi 55 baada ya kucheza mechi 23, moja zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 47 katika nafasi ya pili.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hance Mabena wa Tanga aliyesaidiwa na Jesse Erasmo wa Morogoro na Rashid Zongo wa Iringa, hadi mapumziko Simba SC walikuwa tayari wamekwishavuna ushindi huo wa mabao 3-1.
  Emmanuel Okwi akishangilia baada ya kufunga bao la kwanza leo 
  John Bocco (kulia) akiondoka na mpira baada ya pasi ya Shomary Kapombe (kushoto) wakiwaacha chini wachezaji wa Mbeya City 
  Emmanuel Okwi akijaribu kuwapita wachezaji wa Mbeya City
  Mshambuliaji kutoka Ghana, Nicholas Gyan anayetumika kama beki kwa sasa akitafuta maarifa ya kumpita beki wa Mbeya City, Rajab Isihaka  
  Mshambuliaji wa Mbeya City, Frank Ikobela akiwa juu kupiga mpira kichwa dhidi ya beki wa Simba, Shomary Kapombe 

  Nyota Mganda, Emmanuel Arnold Okwi alianza kuwainua vitini mashabiki wa SImba SC dakika ya 20 baada ya kukutana na mpira uliookolewa na kipa wa Mbeya City, Mmalawi Owen Chaima kufuatia shuti la Nahodha, mshambuliaji John Raphael Bocco. 

  Beki Mghana, Asante Kwasi akaifungia bao la pili Simba SC dakika ya 36 akitumia bega lake kumalizia krasi ya winga Shiza Ramadhani Kichuya, bao ambalo hata hivyo lililalamikiwa na wachezaji wa Mbeya City wakidai alifunga kwa mkono.
  Juhudi za Mbeya City ya kocha Mrundi, Ramadhani Nswazurimo zilizaa matunda dakika ya 37 baada ya kufanikiwa kupata bao leo pekee lililofungwa na mshambuliaji wake, Frank Ikobela aliyeunganisha kwa kichwa kona ya Danny Joram.
  Hata hivyo, Nahodha mshambuliaji John Raphael Bocco akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 38 akimalizia krosi ya beki Shomary Kapombe kutoka upande wa kulia. 
  Kipindi cha pili timu zote zilishambuliana kwa zamu, Mbeya City wakianza vizuri dakika ya 20 za mwanzo kabla ya Simba SC ya kocha Mfaransa, Pierre Lechantre kutulia na kuanza kujibu mashambulizi.
  Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, bao pekee la Kelvin Sabato dakika ya 22 limetosha kuipa ushindi wa 1-0 Mtibwa Sugar dhidi ya Ndanda FC jioni ya leo Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro. 
  Mechi nyingine kati ya wenyeji, Ruvu Shooting na Azam FC iliyopangwa kufanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani imeahirishwa hadi kesho Saa 10:00 jioni tena kutokana na maji mengi kutuwama uwanjani baada ya mvua kubwa iliyonyesha leo.
  Kikosi cha Simba SC Kilikuwa: Aishi Manula, Nicholas Gyan/James Kotei dk87, Asante Kwasi/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk72, Juuko Murshid, Yussuf Mlipili, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi, John Bocco/Laudit Mavudo dk79 na Shiza Kichuya.
  Mbeya City: Owen Chaima, Rajabu Isihaka, Majaliwa Shaaban, Ally Lundenga, Haruna Shamte, Eliud Ambokile, Danny Joram/Mohammed Samatta dk61, Victor Hangaya/Geoffrey Muller dk76, Baab Ally Seif na Frank Ikobela.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAANZA KUVUTA HEWA YA UBINGWA, YAITANDIKA 3-1 MBEYA CITY NA KUWAACHIA VUMBI YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top