• HABARI MPYA

    Thursday, April 05, 2018

    MMOJA AONGEZWA KESI YA AVEVA NA KABURU IKIAHIRISHWA HADI APRILI 12

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KESI inayowakabili viongozi wakuu wa Simba SC, Rais Evans Elieza Aveva na Makamu wake, Geoffrey Hiriki Nyange ‘Kaburu imeahirishwa tena hadi Aprili 12, mwaka huu ili kuupa fursa upande wa mashtaka kufanya mabadiliko ya jalada kwa kuongeza mshitakiwa mmoja.
    Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu Jijini Dar es Salaam leo, Thomas Simba, Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leornad Swai alisema kesi hiyo ilifikishwa kwa ajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali baada ya upelelezi kukamilika.
    Hata hivyo, wakili Swai akaiomba mahakama hiyo ahirisho fupi ili kutoa fursa ya mabadiliko hati ya mashitaka kwa kuongeza mshitakiwa mmoja, ombi ambalo lilikubaliwa na sasa kesi hiyo itasikilizwa tena Aprili 12, mwaka huu.
    Evans Aveva na Geoffrey Nyange ‘Kaburu wakati wanawasili mahakamani leo kabla ya kesi yao kuahirishwa hadi Aprili 12, mwaka huu 

    Kwa pamoja, Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashitaka matano ya uhujumu uchumi, ikiwamo kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na utakatishaji wa fedha ambazo ni dola za Kimarekani 300,000, zaidi ya Sh. Milioni 600 za Tanzania.
    Aveva leo alifika mahakamani baada ya kulazwa kwa muda mrefu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu, ingawa alikuwa hajiwezi kiasi cha kushikiliwa mkono na mshitakiwa mwenzake, Kaburu kumsaidia kutembea.
    Aveva na Kaburu walipelekwa mahabusu, gereza la Keko, Dar es Salaam Juni 29, mwaka huu kufuatia kusomewa mashitaka matano Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam.
    Wawili hao walifikishwa mahakamani mapema asubuhi ya Juni 29, mwaka huu na kusomewa mashitaka hayo matano mchana wake, ambayo ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodai kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni Rais Aveva na Makamu wake, Kaburu kiasi cha dola za Kimarekani 300,000.
    Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwenye benki ya CRDB tawi la Azikiwe mjini Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sharia, ambapo inadaiwa Rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.
    Shitaka la nne ni Kaburu kutakatisha fedha dola 300,000 na kuziweka kwenye benki ya  Barclays tawi la Mikocheni mjini Dar es Salaam, na la tano ni kutakatisha likimhusu tena, Makamu wa Rais, Kaburu aliyemsadia Aveva kutakatisha fedha katika Barclays baada ya kughushi nyaraka.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MMOJA AONGEZWA KESI YA AVEVA NA KABURU IKIAHIRISHWA HADI APRILI 12 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top