• HABARI MPYA

    Thursday, April 05, 2018

    CAF YATHIBITISHIA ADHABU YA YONDAN NA KUFUNGIA MWINGINE YANGA MECHI NA WELAITA DITCHA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeithibitishia klabu ya Yanga kuwa beki wake tegemeo, Kelvin Yondan alionyeshwa kadi kwenye mechi zote mbili dhidi ya Township Rollers ya Botswana na hatacheza Jumamosi dhidi ya Welaita Ditcha ya Ethiopia.
    CAF juzi iliitumia barua ya tahadhari Yanga kutowatumia wachezaji wake wanne, Nahodha Yondan, viungo Said Juma ‘Makapu’ na Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi na mshambuliaji Mzambia Obey Chirwa katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Welaita Ditcha ya Ethiopia.  
    Yanga watakuwa wenyeji wa Waleita Ditcha ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    CAF imeithibitishia Yanga kuwa Kelvin Yondan alionyeshwa kadi kwenye mechi zote mbili dhidi ya Township Rollers  

    Lakini benchi la Ufundi la Yanga lilisema halina kumbukumbu za Yondan kuonyeshwa kadi mbili za njano na kulazimika kuomba ufafanuzi CAF ambao wamepewa tayari na kujiridhisha, hivyo beki huyo wa zamani wa Simba kuondolewa kwenye programu za mchezo huo. 
    Pamoja na wachezaji hao wanne, Kocha Msaidizi wa Yanga, Mzambia Noel Mwandila naye hatatakiwa kukaa kwenye benchi, ingawa hapo CAF imejichanganya, kwani aliyeondolewa uwanjani mjini Gaborone ni Kocha Msaidizi mwingine, Nsajigwa Shadrack.   
    Wapinzani wa Yanga, Welaita Ditcha nao watawakosa wachezaji wao wawili, Teklu Tefesse Kumma na Eshetu Mena Medelecho baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano kila mmoja katika mechi zao mbili zilizopita dhidi ya Zamalek ya Misri.
    Yanga imeweka kambi mjini Morogoro tangu juzi kujiandaa na mchezo huo na inatarajiwa kurejea mjini Dar es Salaam leo kwa maandalizi ya ‘mwisho mwisho’.
    Yanga wataingia kwenye mchezo wa Jumamosi wakitoka kutolewa na Singida United katika Robo Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 Jumapili Uwanja wa Namfua mjini Singida.
    Na Yanga waliingia kwenye mchezo huo wakitoka kutolewa kwenye hatua ya 32 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya 2-1 waliyofungwa na Township Rollers ya Botswana Machi 6 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam kabla sare ya 0-0 kwenye mechi ya marudiano mjini Gaborone nchini Botswana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CAF YATHIBITISHIA ADHABU YA YONDAN NA KUFUNGIA MWINGINE YANGA MECHI NA WELAITA DITCHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top