• HABARI MPYA

  Wednesday, April 04, 2018

  LWANDAMINA AFURAHIA MAANDALIZI YA YANGA KUELEKEA MECHI NA WAHABESHI JUMAMOSI TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa Yanga, Mzambia George Lwandamina anafurahishwa na maendeleo ya timu yake kuelekea mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Waleita Ditcha ya Ethiopia Jumamosi.
  Yanga imeweka kambi mjini Morogoro kujiandaa na mchezo dhidi ya Welaita Ditcha Jumamosi Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na kuelekea mchezo huo, Lwandamina amesema maandalizi yanaendelea vizuri.
  “Maandalizi yanaendelea vizuri,”amesema Lwandamina leo kwa simu kutoka Morogoro alipoulizwa na Bin Zubeiry Sports – Online juu ya maandalizi kuelekea mchezo huo.
  GL amesema kwamba wachezaji wake wote wameelekeza fikra zao vizuri kabisa kwenye mchezo huo na kikubwa wanaendelea kufanyia kazi mapungufu ambayo yamekuwa yakijitokeza kwenye mechi zilizopita.
  George Lwandamina anafurahishwa na maendeleo ya Yanga kuelekea mchezo na Waleita Ditcha ya Ethiopia Jumamosi

  Yanga inatarajiwa kurejea mjini Dar es Salaam kesho kwa maandalizi ya ‘mwisho mwisho’ ya mchezo huo dhidi ya Ditcha.
  Yanga wataingia kwenye mchezo wa Jumamosi wakitoka kutolewa na Singida United katika Robo Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 Jumapili Uwanja wa Namfua mjini Singida.
  Na Yanga waliingia kwenye mchezo huo wakitoka kutolewa kwenye hatua ya 32 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya 2-1 waliyofungwa na Township Rollers ya Botswana Machi 6 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam kabla sare ya 0-0 kwenye mechi ya marudiano mjini Gaborone nchini Botswana.
  Na sasa baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa, Yanga itamenyana na Welayta Dicha ya Ethiopia katika mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, mechi ya kwanza ikifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi wiki hii na marudiano Addis Ababa kati ya Aprili 17 na 18, mwaka huu.
  Welayta Dicha watarajiwa kuwasili Dar es Salaam leo, hii ikiwa mara ya pili mwaka huu wanakuja Tanzania baada ya Februari kuja kucheza na na Zimamoto ya Zanzibar na kushinda kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Ethiopia.
  Welayta Dicha imefika hatua hii baada ya kuitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 3-3, kila timu ikishinda 2-1 nyumbani kwake.
  Katika Raundi ya Awali ambayo Yanga SC iliitoa Saint Louis Suns United ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Dar es Salaam na sare ya 1-1 Mahe, Welayta Dicha iliitoa Zimamoto ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Erthiopia.
  Huu ni mwaka wa tatu mfululizo, Yanga inaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na mara ya nne kwa ujumla kihiostoria.
  Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2007 ilipotolewa na na El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-0 iliyofungwa Khartoum baada ya sare ya 0-0 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Iliingia kwenye kapu hilo baada ya kutolewa na  Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao 3-0 iliyofungwa mjini Tunis, baada ya sare 0-0 Mwanza.
  Mwaka pekee Yanga ilifuzu hatua ya makundi Kombe la Shrikisho Afrika baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa ni 2016, ilipoitoa Sagrada Esperança ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 1-0 Angola.
  Hiyo ilikuwa baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kwenda kufungwa 2-1 Alexandria.
  Katika hatua ya makundi, Yanga ilipangwa Kundi moja na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), MO Bejaia ya Algeria na Medeama SC ya Ghana. 
  Yanga ilishinda mechi moja tu dhidi ya MO Bejaia 1-0 na sare ya 1-1 na Medeama Dar es Salaam huku mechi nyingine zote nne ikifungwa, zikiwemo mbili za nyumbani na ugenini na TP Mazembe.
  Mwaka jana pia Yanga baada ya kutolewa na Zanaco ya Zambia kwa mabao ya ugenini, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na 0-0 Lusaka, ikaenda kutolewa na MC Alger ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye mchujo wa kuwania tiketi ya hatua ya makundi Kombe la Shirikisho, ikishinda 1-0 Dar es Sakaam na kufungwa 4-0 Algiers.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LWANDAMINA AFURAHIA MAANDALIZI YA YANGA KUELEKEA MECHI NA WAHABESHI JUMAMOSI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top