• HABARI MPYA

    Saturday, April 07, 2018

    KILA LA HERI YANGA SC MECHI NA WAHABESHIN LEO TAIFA…NI USHINDI TU, TENA ULE UNAOITWA MNONO KAZI IKAWE NYEPESI ETHIOPIA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC inateremka Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam leo kumenyana na Welaita Ditcha ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania tiketi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Katika mchezo wa leo, Yanga itawakosa wachezaji wake wanne tegemeo wote wa kikosi cha kwanza, mabeki Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, kiungo Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi na mshambuliaji Obrey Chirwa ambao wote walionyeshwa kadi za njano katika mechi mbili zilizopita za nyumbani na ugenini dhidi ya Township Rollers ya Botswana.
    Lakini hapana shaka, kocha Mzambia George Lwandamina amejipanga kuingiza timu bila wanne hao kwenye mchezo wa leo, ingawa kukosekana kwa sentahafu Yondan kunatarajiwa kuiyumbisha safu ya ulinzi ya Yanga, ingawa Andrew Vincent ‘Dante’ na Nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wapo.
    Mungu ibariki Yanga SC ishinde mechi ya leo na kujiweka kwenye nafasi nzuri kuelekea kwenye mchezo wa marudiano wiki ijayo Ethiopia

    Welaita Ditcha nao watawakosa wachezaji wao wawili, Teklu Tefesse Kumma na Eshetu Mena Medelecho baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano kila mmoja katika mechi zao mbili zilizopita dhidi ya Zamalek ya Misri, wakati kocha Msaidizi wa Yanga, Mzambia Noel Mwandila naye hataruhusiwa kukaa benchi leo, ingawa aloiyetolewa Gaborone alikuwa Kocha Msaidizi mwingine, Nsajigwa Shadrack.
    Yanga ilirejea Dar es Salaam jana ikitokea mjini Morogoro ambako iliweka kambi tangu Jumatatu, siku moja tu baada ya kutolewa na Singida United katika Robo Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 juzi Uwanja wa Namfua mjini Singida.
    Kocha Lwandamina safari hii anataka matokeo mazuri katika mchezo wa nyumbani kwenye michuano ya Afrika, baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa matokeo mabaya ya nyumbani.
    Yanga SC ilifungwa 2-1 na Township Rollers ya Botswana Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam Machi 6 katika mchezo wa kwanza wa 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya kwenda kupata sare ya 0-0 kwenye mechi ya marudiano mjini Gaborone nchini Botswana.
    Na sasa baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa, Yanga itamenyana na Welayta Dicha ya Ethiopia katika mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, mechi ya kwanza ikifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi wiki hii na marudiano Addis Ababa kati ya Aprili 17 na 18, mwaka huu.
    Hii ni mara ya pili mwaka huu kwa Welayta Dicha kuja Tanzania. baada ya Februari kuja kucheza na na Zimamoto ya Zanzibar na kushinda kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Ethiopia.
    Welayta Dicha imefika hatua hii baada ya kuitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 3-3, kila timu ikishinda 2-1 nyumbani kwake.
    Katika Raundi ya Awali ambayo Yanga SC iliitoa Saint Louis Suns United ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Dar es Salaam na sare ya 1-1 Mahe, Welayta Dicha iliitoa Zimamoto ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Erthiopia.
    Huu ni mwaka wa tatu mfululizo, Yanga inaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na mara ya nne kwa ujumla kihiostoria.
    Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2007 ilipotolewa na na El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-0 iliyofungwa Khartoum baada ya sare ya 0-0 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Iliingia kwenye kapu hilo baada ya kutolewa na  Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao 3-0 iliyofungwa mjini Tunis, baada ya sare 0-0 Mwanza.
    Mwaka pekee Yanga ilifuzu hatua ya makundi Kombe la Shrikisho Afrika baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa ni 2016, ilipoitoa Sagrada Esperança ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 1-0 Angola.
    Hiyo ilikuwa baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kwenda kufungwa 2-1 Alexandria.
    Katika hatua ya makundi, Yanga ilipangwa Kundi moja na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), MO Bejaia ya Algeria na Medeama SC ya Ghana. 
    Yanga ilishinda mechi moja tu dhidi ya MO Bejaia 1-0 na sare ya 1-1 na Medeama Dar es Salaam huku mechi nyingine zote nne ikifungwa, zikiwemo mbili za nyumbani na ugenini na TP Mazembe.
    Mwaka jana pia Yanga baada ya kutolewa na Zanaco ya Zambia kwa mabao ya ugenini, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na 0-0 Lusaka, ikaenda kutolewa na MC Alger ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye mchujo wa kuwania tiketi ya hatua ya makundi Kombe la Shirikisho, ikishinda 1-0 Dar es Sakaam na kufungwa 4-0 Algiers.
    Mshindi wa jumla atajihakikishia kitita cha dola za Kimarekani, 550,000 zaidi ya Sh. Bilioni 1.1 za Tanzania ambazo zinaweza kuongezeka kama timu ikiingua Nusu Fainali na kuwa dola 800,000 (zaidi ya Sh. Bilioni 1.6), Dola Milioni 1.2 (zaidi ya Sh. Bilioni 2.5) kwa nafasi ya pili na Dola Milioni 2.5 (zaidi ya Sh. Bilioni 5) kwa kuchukua Kombe.
    Matokeo mazuri zaidi kwa timu za Tanzania katika michuano hii ni mwaka 1993, Simba SC ilipofika fainali katika mfumo wa zamani wa mtoano mwanzo hadi mwisho na kufungwa na Stella Abidjan kwa mabao 2-0 Dar es Salaam baada ya sare ya 0-0 nchini Ivory Coast.
    Kila la heri Yanga SC. Mungu ijaalie Yanga SC ishinde mechi ya leo na kujiweka kwenye nafasi nzuri kuelekea kwenye mchezo wa marudiano wiki ijayo Ethiopia. Mungu ibariki Tanzania. Amin.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA LA HERI YANGA SC MECHI NA WAHABESHIN LEO TAIFA…NI USHINDI TU, TENA ULE UNAOITWA MNONO KAZI IKAWE NYEPESI ETHIOPIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top