• HABARI MPYA

  Sunday, January 21, 2018

  YANGA SC YAILAZA 1-0 RUVU, AZAM YAIPIGA 2-0 PRISONS MBEYA…SIMBA WANA KAZI KAGERA KESHO KAITABA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  BAO pekee la kiungo Pius Charles Buswita leo limeipa Yanga SC ushindi mwembaba wa 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Buswita aliye katika msimu wake wa kwanza Jangwani tangu asajiliwe kutoka Mbao FC ya Mwanza, alifunga bao hilo dakika ya 45 na ushei kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo mshambuliaji, Ibrahim Ajib Migomba. 
  Lakini Yanga walimaliza kipindi cha kwanza wanaongoza kwa bao 1-0 wakitoka kuchezewa zaidi mpira na wapinzani wao hao, ambao walikuwa wenyeji kwenye mchezo wa leo. 
  Dakika moja kabla ya Buswita kufunga, Ayoub Kitala aliikosesha Ruvu bao la wazi baada ya kupigwa juu ya lango akiwa anatazamana na lango la Yanga kufuatia kupokea krosi ya Abdulrahman Mussa aliyewachambua mabeki wa Yanga.
  Mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajib (kushoto) akimpita beki wa Ruvu Shooting, Mau Bofu

  Wachezaji wa Yanga wakimpongeza mfungaji wa bao lao pekee leo, Pius Buswita (wa pili kulia)

  Kiungo wa Yanga, Pius Buswita akipasua katikati ya wachezaji wa Ruvu Shooting  

  Beki wa Yanga, Hassan Kessy akimtoka beki wa Ruvu Shooting, Mau Bofu

  Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe akitafuta maarifa ya kumpita beki wa Ruvu Shooting, Damas Makwaya 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Florentina Zabron kutoka Dodoma aliyesaidiwa na Rashid Zongo wa Iringa na Michael Mkongwa kutoka Njombe, Yanga walikianza vizuri kipindi cha pili na kiungo aliyechezeshwa kama sentahafu leo, Said Juma ‘Makapu’ aliunganishia kwenye nyavu za nje kwa kichwa kona ya Ajib.
  Buswita akapiga shuti la umbali wa mita 20 dakika ya 62 baada ya kupokea pasi ya kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi, lakini likaenda nje. 
  Almanusra Issa Kanduru aisawazishie Ruvu dakika ya 64 baada ya kuwachambua vyema mabeki wa Yanga na kumpiga chenga kipa Mcameroon, Youthe Rostand lakini akachelewa kufunga hadi beki Hassan Kessy akatokea na kuokoa bao la wazi.
  Jamal Soud aliyeingia kuchukua nafasi ya Adam Ibrahim naye alikaribia kuipatia bao Ruvu bao la kusawazisha kwa shuti la mbali dakika ya 79, lakini mpira ukatoka nje.
  Juma Mahadhi naye aliyeingia kuchukua nafasi ya Amissi Tambwe kipindi cha pili, akapoteza nafasi nzuri ya kjfunga baada ya kuingiziwa krosi safi na Emmanuel Martin, lakini akapiga nje.
  Yanga inafikisha pointi 25, baada ya kucheza mechi 14 na kupanda hadi nafasi ya tatu, nyuma ya Simba SC yenye pointi 29 na Azam FC pointi 30. 
  Mzunguko wa 14 wa Ligi Kuu utakamilishwa kesho kwa mechi mbili, Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Sugar wataikaribisha Simba SC na Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, Maji Maji watakuwa wenyeji wa Singida United.  
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Azam FC imeshinda 2-0 dhidi ya wenyeji, Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya mabao yake yakifungwa na Yahya Zayed dakika ya 24 na Paul Peter dakika ya 82, wakati Mwadui FC imelazimishwa sare ya 1-1 na Ndanda FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga wageni wakitangulia kwa bao la John George dakika ya 43 kabla ya Awadh Juma kuwasawazishia wenyeji dakika ya 48.
  Kikosi kamili cha Yanga leo kilikuwa; Youthe Rostand, Hassan Kessy Mwinyi Hajji Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’, Said Juma ‘Makapu’, Papy Kabamba Tshishimbi, Pius Buswita, Raphael Daudi/Pato Ngonyani dk86, Amissi Tambwe/Juma Mahadhi dk69, Yohanna Nkomola/Emmanuel Martin dk28 na Ibrahim Ajib.
  Ruvu Shooting; Abdallah Rashid, George Amani, Mau Bofu, Damas Makwaya, Rajab Zahir, Baraka Mtui, Abdulrhaman Mussa, Adam Ibrahim/Jamal Soud dk46, Issa Kanduru, Shaaban Msala, Ayoub Kitala/Fully Zully Maganga dk49.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAILAZA 1-0 RUVU, AZAM YAIPIGA 2-0 PRISONS MBEYA…SIMBA WANA KAZI KAGERA KESHO KAITABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top