• HABARI MPYA

    Tuesday, January 30, 2018

    ROSTAND AIPELEKA YANGA 16 BORA KOMBE LA AZAM SPORTS FEDERATION

    Na Gwamaka Mwankota, MBEYA
    KIPA Mcameroon, Youthe Rostand leo ameibuka shujaa wa Yanga baada ya kupangua penalti tatu na kuiwezesha kuingia hatua ya 16 Bora ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa ushindi wa penalti 4-3 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
    Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Ihefu ya Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara ilikaribia kuimaliza Yanga ndani ya dakika 90, kama si bao la penalti la dakika ya mwisho la mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa.
    Ihefu walitangulia kwa bao la kujifunga la beki wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ dakika ya 36 katika juhudi za kuokoa shuti la Innocent Kapalata aliyepasiwa na Elias Salingo.
    Baada ya bao hilo, Yanga waliokuwa wakicheza taratibu walikuwa kama waliopigwa mshituko na kuamka kwa kuongeza kasi ya mashambulizi.
    Youthe Rostand leo amepangua penalti tatu na kuiwezesha Yanga kwenda 16 Bora ya Azam Sports Federation Cup  

    Lakini safu ya ulinzi ya Ihefu ikiongozwa na kipa wake hodari, Andrew Kayuni iliwazuia watoto wa kocha Mzambia, George Lwandamina kupata bao.
    Kipindi cha pili, Ihefu wakaamua kabisa kucheza kwa kujihami na huku wakipoteza muda kwa kujiangusha na kuchelewa kuanzisha mipira inapofuka upande wao.
    Lakini Yanga waliendelea kuwa wastahmilifu huku pia wakibadili mbinu moja baada ya nyingine katika jitihada za kusaka bao la kusawazisha.
    Hatimaye mpango wa kutafuta penalti wa Chirwa ukafanikiwa dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza kati ya sita baada ya kutimia dakika 90 za kawaida za mchezo, pale Mzambia huyo alipoingia kwenye boksi na kwenda chini kwa urahisi baada ya kubanwa na mabeki wawili wa Ihefu.
    Chirwa mwenyewe akaenda kufunga penalti hiyo na kuwainua kwa furaha mamia ya mashabiki wa Yanga waliokuwa wamenyong’onyea kwa pamoja na baridi ya Mbeya, lakini pia matokeo ya kuwa nyuma kwenye mchezo.
    Ukawadia muda wa matuta na kipa wa Ihefu Andrew Kayuni akawashitua Yanga baada ya kuokoa penalti ya kwanza ya Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi – lakini Nahodha Kevin Yondan akarejea kufunga ya pili, Hassan Kessy akafunga ya tatu, Gardiel Michael ya nne kabla ya Chirwa kughongesha mwanmba penalti ya tano na Raphael Daudi kufunga ya sita.
    Rostande alicheza penalti za Abubakar Kidungwe, Emmanuel Mamba na Richard Ngondya wakati za Andrew Kayuni, Mando Mkumbwa na Jonathan Mwaibindi zilimpita na kutinga nyavuni.
    Matokeo ya mechi nyingine ziliochezwa leo ya ASFC; Shupavu imefungwa nyumbani 5-0 na Azam FC Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Kariakoo United imefungwa 1-0 kwake na Mbao FC Uwanja wa Ilulu, Lindi, Mwadui FC imefungwa 2-1 nyumbani na Dodoma FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na Kagera Sugar pia imefungwa nyumbani 2-0 na Buseresere FC Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
    Mechi nyingine, Polisi Tanzania imeifunga Friends Rangers 2-1 Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Ndanda FC imeshinda kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1 na Biashara United ya Mara na JKT Tanzania imeifunga Polisi Dar 1-0 mjini Dar es Salaam.
    Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi kati ya Maji Maji FC na Ruvu Shooting Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, Tanzania Prisons na Burkina Faso Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Kiluvya United na JKT Oljoro Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Green Warriors na Singida United Uwanja w Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Pamba na Stand United Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na Njombe Mji na Rhino Rangers Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe. 
    Mchezo kati ya KMC na Toto Africans umesogezwa mbele hadi Januari 7 uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
    Kikosi cha Ihefu FC; Andrew Kayuni, Mando Mkumbwa, Elias Salingo, Alain Merere, Jonathan Mwaibindi, Ibrahim Kalenzo, Godfrey Kitengamlima, Innocent Kapalata/Abubakar Kidungwe dk80, Jose Kinyozi/Steven Kabume dk60, Richard Ngondya na Emmanuel Mamba.
    Yanga SC; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Andrew Vincent, Kelvin Yondan, Maka Edward/Raphael Daudi dk59, Juma Mahadhi/Emmanuel Martin dk65, Papy Kabamba Tshishimbi, Obrey Chirwa, Amissi Tambwe/Pius Buswita dk46 na Geoffrey Mwashiuya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ROSTAND AIPELEKA YANGA 16 BORA KOMBE LA AZAM SPORTS FEDERATION Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top