• HABARI MPYA

    Sunday, January 28, 2018

    VIONGOZI AZAM FC WASITHUBUTU KURUDIA KOSA KAMA LA JANA

    TIMU ya Azam FC jana imeshindwa kutumia vyema Uwanja wa nyumbani baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 28 baada ya kucheza mechi 15, ingawa inaendelea kukaa nafasi ya tatu, nyuma ya Azam FC inayobaki na pointi zake 30 nyuma ya vinara, Simba SC wenuye pointi 32.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Israel Mujuni Nkongo aliyeyesaidiwa na washika vibendera Soud Lila na Frank Komba, hadi mapumziko tayari Yanga walikuwa wamekwishatengeneza ushindi wao huo.
    Lakini ilibidi Yanga watoke nyuma baada ya mshambuliaji chipukizi, Shaaban Iddi Chilunda kutangulia kuifungia Azam FC bao la kuongoza dakika ya nne tu akimalizia krosi ya Mzimbabwe, Bruce Kangwa aliyemtoka beki Hassan Kessy pembeni na kuingia ndani.
    Mzambia Obrey Chirwa akaisawazishia Yanga dakika ya 30 baada ya kupokea pasi ya kiungo mshambuliaji, Ibrahim Ajib na kumpiga chenga kipa wa Azam, Mghana Razack Abalora aliyetoka bila maarifa ya ziada.
    Katika mastaajabu ya wengi, kocha wa Azam FC, Mromania Aristica Cioaba alimtoa mshambuliaji Mghana, Bernard Arthur aliyekuwa anacheza vizuri na kuwatia misukosuko mabeki wa Yanga, akamuingiza kiungo Salmin Hoza.
    Haikuwa ajabu Yanga walipouteka mchezo kwa kasi na mashambulizi mfululizo hadi wakafanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na beki Gardiel Michael Mbaga aliye katika msimu wake wa kwanza  Jangwani tangu asajiliwe kutoka Azam aliyefunga kwa shuti la umbali wa mita 30 baada ya pasi ya Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi.
    Ushangiliaji wa Gardiel kana kwamba alijua ndio bao la ushindi, lakini ulitosha kupeleka ujumbe kwa viongozi wa Azam FC kwamba walikosea kumuacha.
    Kipindi cha pili mchezo ulinoga zaidi, Azam FC wakisaka bao la kusawazisha na Yanga ambayo leo iliongozwa na kocha wake, Mzambia George Lwandamina ikitafuta bao la pili.
    Cioaba akasahihisha makosa yake baada ua kurudisha mshambuliaji uwanjani na kutoa kiungo, akimuingiza Mbaraka Yussuf kwenda kuchukua nafasi ya Stephan Kingue Mpondo.    
    Azam FC ilipata pigo dakika ya 79 baada ya kiungo wake, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu kufuatia kumchezea rafu beki wa Yanga, Hassan Kessy. Sure boy alionyeshwa kadi ya kwanza ya njano dakika ya 22 alipomchezea Emmanuel Martin.
    Kutoka hapo, Yanga wakauteka kabisa mchezo, lakini wakaishia kukosa mabao ya wazi tu.
    Ikumbukwe siku mbili kabla ya mechi hiyo, uongozi wa Azam FC uliandika barua Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) ikielezea kutokuwa na imani na mwamuzi Nkongo.
    “Kama klabu, itakumbukwa kuwa mechi zetu ambazo mwamuzi huyu (Nkongo) amekuwa akizichezesha zimekuwa na malalamiko mengi na utata mwingi juu ya maamuzi ya uwanjani,” ilisema moja ya nukuu kwenye barua hiyo.
    Barua hiyo iliendelea kueleza kwamba moja ya sababu nyingine ya kumlalamikia mwamuzi huyo na kukosa imani naye, ni kitendo chake cha kuzua utata mkubwa kwenye mchezo aliochezesha mkoani Mbeya wiki moja iliyopita kati ya Tanzania Prisons na Mbeya City kutokana na uamuzi wake.
    Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohamed, aliyeandika barua hiyo na kutuma nakala kwa Kamati ya Waamuzi, TFF na Yanga, ameweka wazi kuwa kwa kuzingatia uzito wa mchezo huo wameiomba bodi hiyo kubadilisha mwamuzi kwa kumpanga mwingine.
    Aidha katika barua hiyo, Mohamed ameongeza kuwa kutokana na timu zote mbili kutoka katika mkoa wa Dar es Salaam, ameiomba bodi hiyo kumpanga mwamuzi ambaye atatoka nje ya mkoa huo.
    Pamoja na kuandika barua kwenda Bodi ya Ligi, Azam FC walitoa taarifa kwa vyombo vya Habari na viongozi wake wakahojiwa na vituo vya Redio na Televisheni wakimkataa hadhari refa Nkongo.
    Ukweli ni kwamba kitendo kilichofanywa na viongozi wa Azam FC kwanza hakikuwa cha kiungwana na zaidi kililenga kumvuruga refa huyo mteule kuelekea mchezo wa jana.
    Lakini bahati mbaya kikasababisha athari zaidi ndani ya timu yao wenyewe, Azam FC kwa wachezaji kuingia uwanjani wakiamini refa ni adui yao.
    Hali hiyi iliwaingiza kwenye mtego wa kufanya makosa mengi ya utovu wa nidhamu, ambayo matokeo yake yaliigharimu timu, ikiwemo kiungo Salum Abubakar ‘Sur Boy ’kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
    Kama kulikuwa kuna malalamiko ya msingi dhidi ya refa, Azam wangeweza kuyawasilisha kimaandishi bila kuvujisha kwenye vyombo vya habari na mambo yangeshughulikiwa kiofisi.
    Pamoja na makosa ya benchi la Ufundi katika mchezo wa jana, lakini bado uongozi kwa mamalamiko ya wazi dhidi ya refa Nkongo yalichangia kuwapoteza malengo wachezaji wa Azam FC.
    Na maana yake, kwa kipigo cha jana viongozi wa Azam FC nao hawawezi kukwepa lawama.  
    Waswahili wanasema maji yakishamwagika hayazoleki, Azam imekwishapoteza mchezo na sasa inapaswa kuelekeza nguvu zake katika michezo ijayo - lakini wajue hawpaswi kurudia kufanuya koasa ka la jana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VIONGOZI AZAM FC WASITHUBUTU KURUDIA KOSA KAMA LA JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top