• HABARI MPYA

    Sunday, January 28, 2018

    OKWI MBILI, BOCCO MBILI…SIMBA YA MFARANSA YAUA 4-0

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA mpya wa Simba SC, Mfaransa Perre Lechantre ameanza vyema kibarua yake baada ya kuwaongoza Wekundu hao wa Msimbazi kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Maji Maji ya Songea mkoani Ruvuma katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ushindi huo, unaifanya Simba SC imalize duru la kwanza la Ligi Kuu na pointi 35 baada ya kucheza mechi 15, ikiwazidi kwa pointi saba mabingwa watetezi, Yanga walio nafasi ya tatu na pointi tano, Azam FC wanaoshika nafasi ya pili. 
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Erick Onoka wa Arusha, aliyesaidiwa na washika vibendera Mohammed Mkono wa Tanga na Anold Bugado wa Singida, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0, ambayo yote yalifungwa na Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’.
    Wafungaji wa mabao ya Simba leo, Emmanuel Okwi (kulia) na John Bocco (kushoto) wakishangilia na kiungo Said Ndemla baada ya bao la nne
    John Bocco akimuacha chini beki wa Maji Maji na huku akimburuza mwingine kabla ya kutoa pasi ya bao la mwisho 
    Emmanuel Okwi akimtoka kiungo wa Maji Maji Paul Maona kipindi cha kwanza 
    Kiungo Said Ndemla akimtoka kioungo wa Maji Maji, Yakubu Kibiga 
    Shiza Kichuya akipenyeza mpira mbele ya beki wa Maji Maji, Lucas Kikoti 

    Bocco alifunga bao la kwanza dakika ya 17 akimalizia mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kufuatia beki Mghana, Asante Kwasi kupiga tik tak kuunganisha kona ya winga Shiza Ramadhani Kichuya.
    Lakini benchi la wachezaji wa akiba wa Maji Maji wakiongozwa na kocha wao, Habib Kondo walilalamikia bao hilo na kumfuata mshika kibendera namba moja, Mohammed Mkono kumzonga wakidai Kwasi alicheza faulo wakati anapiga tik tak. Hata hivyo, refa Onoka alipuuza malalamiko hayo na mchezo ukaendelea. 
    Bocco aliye katika msimu wake wa kwanza Msimbazi tangu asajiliwe kutoka Azam FC alikocheza kwa miaka 10, aliwainua vitini wapenzi wa Simba kwa kufunga bao la pili dakika ya 26 kwa kichwa akimalizia ‘majaro’ ya kiungo Said Hamisi Ndemla.
    Bocco alikaribia kukamilisha hat trick dakika ya 37 baada ya pasi ya Okwi, lakini akapiga shuti lililookolewa na kipa Saleh Malande wa Maji Maji. Simba ilimpumzisha Jamal Mwambeleko dakika ya 41 nafasi yake kuchukuliwa na Muzamil Yassin. 
    Kipindi cha pili, Simba SC iliyoongozwa na kocha wake mpya, Mfaransa Pierre Lechantre kwa mara ya kwanza leo, ilikianza kwa mabadiliko, ikimpumzisha beki wa kati, Mganda  Juuko Murshid na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo wa ulinzi, Mghana James Kotei.
    Na dakika ya 52, Mganda Okwi akaifungia Simba bao la tatu akiunganisha vizuri kona ya Kichuya, lakini kipa Malande akapangua mpira na kumkuta tena Mganda huyo aliyefunga kiulaini.
    Okwi tena akafunga bao lake la 12 msimu huu, la pili kwake leo na la nne kwa Simba katika mchezo huo dakika ya 68 akimchambua kipa Malande baada ya pasi maridadi ya Bocco aliyefanya kazi kubwa kuambaa na mpira kutoka nyuma kabisa na mstari wa katikati wa uwanja na kwenda hadi ndani ya 18 na kumtengea Mganda huyo afunge.
    Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Jerson John Tegete alikaribia kuifungia bao la kufutia machozi Maji Maji baada ya kutokea benchi kipindi cha pili, kufuatia kup[okea pasi Six Mwesekaga, lakini pamoja na kupiga nje refa akamuambia alikuwa ameotea.
    Mchezo mwingine wa wa Ligi Kuu leo, Singida United wamekfunga 1-0 Tanzania Prisons Uwanja wa Namfua mkoani Singida, bao pekee la Sumbi Elinyesi dakika ya 90.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Asante Kwasi, Erasto Nyoni, Juuko Murshid/James Kotei dk46, Jonas Mkude, Jamal Mwambeleko/Muzamil Yassin dk41, Said Ndemla, Shiza Kichuya/Laudit Mavugo dk82, Emmanuel Okwi na John Bocco.
    Maji Maji FC; Saleh Malande, Lucas Kikoti, Mpoki Mwakinyuke, Kennedy Kipepe, Paul Maona/Alex Kondi dk58, Hassan Hamisi, Peter Mapunda/Jeryson Tegete dk65, Yakubu Kibiga, Geoffrey Mlawa/Geofrey Mlawa dk60, Marcel Boniventure na Jaffar Mohammed. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OKWI MBILI, BOCCO MBILI…SIMBA YA MFARANSA YAUA 4-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top