• HABARI MPYA

    Wednesday, January 31, 2018

    ‘MWENYEKITI YANGA’ AFUNGIWA MWAKA MZIMA KWA KUIKASHIFU TFF

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia kutojihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa mwaka mmoja Mwenyekiti wa klabu ya Abajalo FC ya Sinza, Edgar Chibula na kumpiga faini ya Sh. Milioni 3 kwa kosa la kulikashifu, kulidhalilisha na kulivunjia heshima shirikisho hilo kwenye vyombo vya habari, kinyume na kifungu cha 50 (1), (2) na (6) cha katiba ya TFF toleo la 2015. 
    Hatua hiyo imechukuliwa katika kikao chake Kamati ya Maadili ya TFF cha Januari 28, 2018 kupitia shauri la Chibula lililofikishwa kwenye kamati hiyo na Sektretarieti ya shirikisho.
    Chibura alikuwa mpinzani wa Yussuf Manji kwenye uchaguzi wa klabu ya Yanga Julai mwaka 2012 katika nafasi ya Uenyekiti na akaangushwa vibaya. Manji alishinda kwa kishindo akipata 1876, sawa na asilimia 97 akifuatiwa kwa mbali na John Jembele aliyepata kura 40 sawa na asilimia 2.6 wakati Chibura alishika mkia baada ya kuambuliwa kura 4, sawa na asilimia 0.24 ndipo akaenda kuibukia Abajalo.
    TFF ya Wallace Karia na Michael Wambura haina masihara; inafungia tu

    Taarifa ya Kamati leo kwa vyombo vya Habari imesema; “Edgar Chibula Mwenyekiti wa Klabu ya Abajalo FC lililosikilizwa mbele ya Kamati alishtakiwa kwa kosa la kuongea maneno ya kuikashifu, kuidhalilisha na kuivunjia heshima TFF katika vyombo vya habari ikiwa ni kinyume na kifungu cha 50(1), (2) na (6) cha katiba ya TFF toleo la 2015,Vilevile ni kinyume na kanuni ya 15 na 16 ya kanuni za maadili ya TFF toleo la 2013,”.
    “Chibula akiwa Mwenyekiti wa klabu ya Abajalo FC na mjumbe wa Bodi ya Ligi aliongea maneno ya kuikashifu, kuidhalilisha na kuivunjia heshima TFF katika vyombo vya habari,Akiwa mmoja wa viongozi wa juu wa mchezo wa mpira hapa nchini hakupaswa kuongea maneno ya kukashfu taasisi anayoiongoza, kwa kufanya hivyo amevunja kanuni ya uwajibikaji wa pamoja na utunzaji wa siri za taasisi,”.
    “Kwenye shauri hilo, mtuhumiwa hakuweza kuhudhuria na badala yake alileta utetezi wake kwa njia ya maandishi ambao unakubalika kikanuni. Sekretarieti ya TFF iliwasilisha ushahidi wa sauti (audio clip) ya mahojiano aliyofanya na kituo kimoja cha redio ambapo kwenye mahojiano hayo mtuhumiwa alisikika akitamka maneno hayo yasiyo na afya kwa maendeleo ya mpira wetu,”.
    “Pia Sekretarieti ya TFF imewasilisha barua ya utetezi kutoka kwa mtuhumiwa ambapo alikiri kuongea na vyombo vya habari baada ya kufanya kila njia ya kuwasiliana na uongozi wa TFF bila mafanikio. Hata hivyo Kamati haikupata nakala ya mawasialiano hayo kutoka kwa mtuhumiwa. Aidha katika barua hiyo mtuhumiwa aliandika maneno yenye kukera na ya kichonganishi,”.
    “Baada ya Kamati kupitia shauri hili imeridhika pasipo na shaka tuhuma dhidi ya mtuhumiwa, kitendo cha kumhusisha mdhamini kwa kuishutumu taasisi inayoongoza mpira ni uchonganishi na ni hatari kwa maendeleo ya mpira; kinaweza kuwaogopesha wadhamini wengine ambao wana nia ya kuwekeza katika mpira,Mtuhumiwa hakuwa na ushahidi wowote uliombatana na tuhuma hizo zinazoweza kudidimiza jitihada za kuinua mchezo wa mpira nchini,”.
    “Kamati imemtia hatiani Edgar Chibula kwa kosa la kuongea maneno ya kuikashifu, kuidhalilisha na kuivunjia heshima TFF katika vyombo vya habari ikiwa ni kinyume na kifungu cha 50 (1), (2) na (6) cha katiba ya TFF toleo la 2015. Hivyo Kamati inamuhukumu kifungo cha kutojihusisha na shughuli za mpira kwa kipindi cha mwaka mmoja (1) na faini ya shilingi milioni tatu (sh.3,000,000) chini ya kifungu cha 73(4) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013,”.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ‘MWENYEKITI YANGA’ AFUNGIWA MWAKA MZIMA KWA KUIKASHIFU TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top