• HABARI MPYA

    Saturday, January 27, 2018

    NYOSSO APELEKWA KAMATI YA MAADILI KUCHUKULIWA HATUA ZA KINIDHAMU KWA KUMPIGA SHABIKI WA SIMBA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SUALA  le beki wa Kagera Sugar FC, Juma Said Nyosso kumpiga shabiki wa wapinzani, baada ya mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba SC limepelekwa Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumalizika, limepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
    Hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Bodi ya Ligi Kuu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kilichofanyika juzi kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Dar es Salaam.
    Katika mechi hiyo namba 112 ambayo Kagera Sugar ilifungwa 2-0, Nyoso alikamatwa na Polisi kwa kumpiga shabiki wa Simba baada ya mechi hiyo iliyochezwa Januari 22, 2018 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
    Juma Nyosso amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua za kinidhamu

    Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani katika mechi namba 95 dhidi ya Kagera Sugar iliyomalizika kwa sare ya 1-1 Januari 1, 2018 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu na Kamati iliiagiza Sekretarieti ya Bodi ya Ligi kutoa waraka kwa wamiliki wa viwanja kuhakikisha timu zinaingia uwanjani kwa kutumia milango rasmi tu.
    Kocha wa Mbeya City, Mrundi Ramadhani Nswazurimo amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa la kumkashifu mwamuzi Israel Mujuni Nkongo katika mechi namba 100 dhidi ya Tanzania Prisons ambayo timu yake ilichapwa 3-2.  Adhabu ambayo imezingatia Kanuni ya 40(11) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.
    Kocha Mwazurimo aliondolewa kwenye benchi (ordered off) na Mwamuzi baada ya kumtolea lugha ya kashfa katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 14, 2018 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
    Mbeya City nayo imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi kwa madai alikataa kutoa penalti kwa timu hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.
    Kamati imeteua wajumbe watatu kupitia mkanda wa mechi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine itachunguza kiwango cha uchezeshaji cha Mwamuzi wa mechi hiyo, Bw. Israel Nkongo na kuwasilisha taarifa yake kwa ajili ya hatua zaidi.
    Azam FC imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na kukataa wachezaji wake wakaguliwe ndani kwenye mechi namba 103 dhidi ya wenyeji Majimaji iliyomalizika kwa sare ya 1-1 Januari 18, Uwanja wa Majimaji mjini Songea kwa madai kuwa chumba kimepuliziwa dawa.
    Kitendo cha timu hiyo ni kinyume na Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, na adhabu dhidi yao imezingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu. Pia klabu hiyo imeandikiwa barua ya kutakiwa kuthibitisha madai yake kuwa chumba hicho kilikuwa kimepuliziwa dawa.
    Mtunza Vifaa wa Singida United FC, Mussa Rajab amefungiwa mwezi mmoja na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuingia uwanjani wakati wa mapumziko kumlalamikia mwamuzi katika mechi namba 104 dhidi ya wenyeji, Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kitendo alichofanya Mtunza Vifaa huyo katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 18, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kimekiuka Kanuni ya 14(10) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 41(2) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Viongozi.
    Stand United imepewa onyo kali kutokana na timu yake kuchelewa kwa dakika sita kwenye kikao cha maandalizi ya mechi na pia kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika tisa katika mechi namba 106 dhidi ya wenyeji Mbao FC timu hiyo ya Shinyanga ikishinda 1-0 Januari 20  Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
    Adhabu kwa klabu hiyo iliyokiuka Kanuni ya 14(2a) ya Ligi Kuu, imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NYOSSO APELEKWA KAMATI YA MAADILI KUCHUKULIWA HATUA ZA KINIDHAMU KWA KUMPIGA SHABIKI WA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top