• HABARI MPYA

    Thursday, January 18, 2018

    SIMBA YAACHANA NA KOCHA WA MOHAMMED, YALETA MFARANSA MWINGINE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    UONGOZI wa Simba SC umeamua kuachana na kocha Hubert Velud na kumchukua Mfaransa mwenzake, Pierre Lechantre.
    Taarifa ya klabu ya Simba leo kwa vyombo vya Habari imesema kwamba, kocha huyo mzoefu ataanza kazi mara moja na atasaidiwa na kocha Mrundi, Masoud Juma ambaye amekuwa akiiongoza timu tangu Desemba mwaka jana alipoondolewa Mcameoon, Joseph Marius Omog.
    Taarifa hiyo imesema Lichantre amekuja na msaidizi mmoja, kocha wa viungo, Mtunisia Mohammed Aymen Hbibi na jioni ya leo ataishuhudia Simba ikicheza na Singida United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Pierre Lechantre amemzidi kete Mfaransa mwenzake, Hubert Velud kuchukua ajira Simba SC

    Pierre Lechantre aliyezaliwa Aprili 2, mwaka 1950 mjini Lille, Nord, Ufaransa ni kocha aliyeipa Cameroon ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2000 na kabla ya kuanza kufundisha alikuwa mchezani pia.
    Aprili 27 mwaka 2012, Lechantre alitambulishwa kuwa kocha Mkuu wa Senegal, lakini akashindwa kufikia makubaliano ya mwisho na Shirikisho la Soka la nchi hiyo.
    Akiwa mchezaji katika nafasi ya ushambuliaji, Lechantre amechezea klabu za Paris FC (1986–1989), Red Star 93 (1983–1986), Stade de Reims (1981–1983), Olympique de Marseille (1980–81), RC Lens (1979–80), Stade Lavallois (1976–1979), AS Monaco (1975–76), FC Sochaux (1970–1975) na Lille OSC (1964–1970).
    Na akiwa kocha amefundisha timu za taifa za Kongo (2016), Cameroon (1999-2001), klabu za Al-Ittihad Tripoli ya Libya kuanzia 2014 hadi 2015, Al Arabi ya Qatar kuanzia Machi hadi September 2013, CS Sfaxien ya Tunisia kuanzia Juni hadi Desemba 2010, Club Africain ya Tunisia kuanzia Juni 10 mwaka 2009 hadi Aprili 2010 na Al Rayyan ya Qatar.
    Amefundisha pia timu ya taifa ya Mali kuanzia Machi hadi Oktoba 2005, Al-Siliya Sports Club ya Qatar kuanzia Novemba 2003, Al-Ahli ya Jeddah kuanzia Agosti hadi Oktoba mwaka 2003, Qatar kuanzia Juni 2002, Le Perreux (1992–1995) na Paris FC (1987–1992).
    Amewahi pia kuwa Mshauri wa Ufundi wa Val de Marne kuanzia Julai 7 mwaka 1995 hadi Januari 1999.
    Na ujio wa kocha huyu unazima mpango wa kocha wa zamani wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Etoile du Sahel ya Tunisia, Mfaransa, Hubert Velud kujiunga na Simba.
    Habari za ndani zinasema kwamba, Velud ni pendekezo la Mjumbe Mteule wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Mohammed Nassor ‘Mohaamed Kigoma’ ambaye alipambana mno klabu imchukue mwalimu huyo, lakini akakutana na upinzani mkali kutoka kwa Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘’. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAACHANA NA KOCHA WA MOHAMMED, YALETA MFARANSA MWINGINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top