• HABARI MPYA

  Sunday, January 14, 2018

  PRISONS YAITANDIKA MBEYA CITY 3-2 SOKOINE, REFA NKONGO ASINDIKIZWA NA POLISI…MASHABIKI WATAWANYWA KWA MABOMU YA MACHOZI

  Na Mwandishi Wetu, MBEYA
  REFA Israel Mujuni Nkongo amesindikizwa na Polisi Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya baada ya mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Tanzania Prisons na Mbeya City leo.
  Prisons wameibuka na ushindi wa 3-2, lakini wachezaji wa Mbeya City walimvamia refa Nkongo mwishoni mwa mchezo wakimlalamikia kuwanyima penalti ya dakika ya mwisho baada ya kuonekana kama Jumanne Elfadhil aliunawa mpira.
  Lakini Nkongo alishikilia msimamo wake wa kutotoa penalti na kusababisha kuzongwa zaidi na wachezaji wa Prisons kabla ya Polisi kuingia na kumtoa.
  Ukabaki ugomvi baina ya wachezaji wa timu zote mbili uliomuhusisha pia na kocha wa Prisons, Mohammed Abdallah, ambao baadaye ukawahusisha na mashabiki pia.
  Polisi wakalazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya mashabiki waliokuwa wanafanya vurugu ndani na nje ya Uwanja wa Sokoine.
  Katika mchezo huo uliodumu kwa dakika 98 pamoja na za nyongeza, mabao ya Prisons yalifungwa na Salum Bosco dakika ya 12, Jumanne Elfadhil kwa penalti dakika ya 66 na Mohamed Rashid dakika ya 89, wakati ya Mbeya City yamefungwa na John Kabanda dakika ya 31 na Babu Ally Seif dakika ya 90 na ushei. 
  Kwa ushindi huo, Prisons inafikisha pointi 21 sawa na mabingwa watetezi, Yanga SC walio nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kucheza mechi 13, wakati Mbeya City inabaki na pointi zake 12 katika nafasi ya pili kwenye ligi ya timu 16.
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa Njombe Mji kuikaribisha Kagera Sugar FC Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe na Janauri 17 Yanga SC watakuwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mzunguko wa 13 utahitimishwa kwa michezo miwili Januri 18, Simba wakiikaribisha Singida United Uwanja wa Taifa na Maji Maji wakiwa wenyeji wa Azam FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PRISONS YAITANDIKA MBEYA CITY 3-2 SOKOINE, REFA NKONGO ASINDIKIZWA NA POLISI…MASHABIKI WATAWANYWA KWA MABOMU YA MACHOZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top