• HABARI MPYA

  Thursday, January 18, 2018

  OKWI ATOKEA BENCHI NA KUPIGA MBILI SIMBA SC IKIICHAPA SINGIDA UNITED 4-0

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Mganda Emmanuel Arnord Okwi ametokea benchi na kufunga mabao mawili Simba SC ikishinda 4-0 dhidi ya Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Matokeo hayo yanaifanya Simba SC ifikishe pointi 29, baada ya kucheza mechi 13, ikiwazidi pointi saba mabingwa watetezi, Yanga SC na pointi mbili Azam FC wenye 27 katika nafasi ya pili, wakati Mtibwa Sugar sasa ni ya tatu kwa pointi zae 24 baada ya timu zote kucheza mechi 13.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Jacob Adongo wa Mara, aliyesaidiwa na Mohammed Mkono wa Tanga na Gasper Ketto wa Arusha hadi mapumziko Simba SC walikuwa wanaongoza kwa mabao 2-0.
  Emmanuel Okwi akishangilia baada ya kufunga mabao maiwli leo Simba ikishinda 4-0 
  Emmanuel Okwi akifumua shuti kuifungia Simba bao la tatu leo
  Beki Mghana, Asante Kwasi akimtungua kipa wa Singida United, Peter Manyika
  Mfungaji wa bao la kwanza la Simba, Shiza Kichuya akimtoka mchezaji wa Singida leo
  Mshambuliaji anayechezeshwa kama beki kwa sasa, Mghana, Nicholas Gyan (kulia)

  Kiungo Shiza Ramadhani Kichuya alianza kuifungia Simba SC dakika ya tatu akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo mkongwe Mwinyi Kazimoto, kufuatia John Raphael Bocco kuangushwa nje kidogo ya boksi. 
  Singida wakacharuka na kuanza kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Simba kusaka bao la kusawazisha, lakini ngome ya Wekundu wa Msimbazi ikiongozwa na Erasto Edward Nyoni ilikuwa imara kuondosha hatari zote. 
  Beki Mghana, Asante Kwasi akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 25 akimvisha kanzu kipa Peter Manyika aliyetoka langoni bila hesabu nzuri baada ya pasi ndefu ya kiungo Said Ndemla aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Kazimoto.
  Bao hilo lilionekana kuwachanganya Singida United wanaofundishwa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm na kuwaruhusu Simba kutawala zaidi mchezo huo.
  Kipindi cha pili, mashabiki wa Simba SC wakaripuka kwa shangwe baada ya kumuona kocha wao mpya, Mfaransa Pierre Lechantre aliyeongozana na msaidizi wakea, kocha wa viungo, Mmorocco Mohammed Aymen Hbibi jukwaa kuu.
  Kocha huyo amekuja kusaini mkataba wa kuifundisha Simba kuchukua nafasi ya Mcameroon, Joseph Marius Omog aliyeondolewa Desemba na atafanya kazi na Mrundi, Masudi Juma ambaye amekuwa akiiongoza tangu kipindi chote hiki.
  Okwi akatokea benchi dakika ya 65 kuchukua nafasi ya kiungo Muzamil Yassin na akafunga mabao mawili ndani ya dakika saba.
  Alifunga bao la tatu dakika ya 75 akimalizia pasi ya Shiza Kichuya na la nne dakika ya 82 akimalizia pasi ya Ndemla. Alifunga mabao hayo, baada ya kumsetia pasi nzuri Kichuya, akapiga nje akiwa ndani ya sita.
  Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Juuko Murshid, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, James Kotei/Mohammed Ibrahim dk88, Mwinyi Kazimoto/Said Ndemla dk22, John Bocco, Shiza Kichuyana Muzamil Yassin/Emmanuel Okwi dk65.
  Singida United; Peter Manyika, Michael Rusheshangoga, Shafiq Batambuze, Kennedy Wilson, Malik Antiri, Mudathir Yahya, Deus Kaseke, Tafadzwa Kutinyu/Yussuf Kagoma79, Lubinda Mundia/Kenny Ally76, Kambale Salita Gentil na Kiggi Makassy/Salum Chukwu dk62. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OKWI ATOKEA BENCHI NA KUPIGA MBILI SIMBA SC IKIICHAPA SINGIDA UNITED 4-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top