• HABARI MPYA

    Thursday, January 18, 2018

    AZAM FC YALAZIMISHWA SARE NA MAJI MAJI SONGEA, 1-1

    Na Mwandishi Wetu, SONGEA
    KLABU ya Azam FC, imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Maji Maji katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara  uliofanyika leo mchana kwenye Uwanja wa Majimaji, mjini Songea, Ruvuma.
    Sare hiyo inaifanya Azam FC kufikisha pointi 27 na kukaa kileleni kwa muda kwenye msimamo wa ligi ikiisubiri Simba ambayo kama itapata ushindi jioni ya leo itarejea kileleni kwa pointi 29.
    Azam FC ndiyo iliyoanza kuliona lango la Majimaji dakika ya 30 kupitia bao safi la winga Joseph Mahundi, aliyeunganisha kiustadi pasi safi ya mshambuliaji Yahya Zayed, bao lililodumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.
    Kiungo wa Azam FC, Frank Domayo akimtoka mchezaji wa Maji Maji leo

    Kipindi cha pili Azam FC iliwaingiza nyota kadhaa kwenye dakika tofauti wakiingia viungo Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na mshambuliaji Shaaban Idd, ikiwatoa Bernard Arthur, Salmin Hoza na Idd Kipagwile, mabadiliko ambayo yaliongeza kasi ya mashambulizi wakati timu hiyo ilipokuwa ikishambulia.
    Dakika ya 73 Majimaji iliweza kusawazisha bao hilo kupitia kwa Marcel Boniventure, aliyepiga mpira wa moja kwa moja wa kona uliojaa wavuni na kufanya matokeo kuisha kwa sare hiyo.
    Kama Azam FC ingekuwa makini ingeweza kujipatia mabao mengine kupitia nafasi walizopoteza kwenye mchezo huo, kipindi cha kwanza kupitia kwa Bernard Arthur, kipindi cha pili ikipoteza nyingine kwa washambuliaji wake Yahya Zayd, Shaaban Idd na beki Yakubu Mohammed.
    Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuelekea mkoani Mbeya kesho Ijumaa asubuhi tayari kabisa kwenda kucheza na Tanzania Prisons, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Sokoine Jumapili hii.
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa: Razak Abalora, Himid Mao (C), Bruce Kangwa, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue, Joseph Mahundi, Salmin Hoza/Shaaban dk 78, Bernard Arthur/Domayo dk 47, Yahya Zayd, Idd Kipagwile/Salum dk 61
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YALAZIMISHWA SARE NA MAJI MAJI SONGEA, 1-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top