• HABARI MPYA

  Tuesday, January 23, 2018

  MASHABIKI SIMBA BUKOBA WAMZAWADIA NDEMLA FEDHA NA MIKUNGU YA NDIZI

  Na Mwandishi Wetu, BUKOBA
  MASHABIKI wa Simba jana wamemzawadia kiungo wa timu hiyo, Said Ndemla fedha na mikungu ya ndizi, baada ya kazi nzuri akiisaidia timu kushinda 2-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
  Ndemla alicheza vizuri jana na kufunga bao la kwanza, wakati bao la pili lilifungwa na Nahodha na mshambuliaji John Raphael Bocco, yote kipindi cha pili.
  Baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, Ndemla aliwainua vitini mashabiki wa Simba SC dakika ya 69 kwa kufunga bao la kwanza akimalizia pasi ya kiungo wa pembeni, Shiza Kichuya.
  Mashabiki wa Simba wakimzawadia kiungo Said Ndemla baada ya mechi jana Uwanja wa Kaitaba
  Mpira uliozaa bao hilo ulitokana na makosa ya mshambuliaji wa Kagera Sugar, Atuepe Green aliyepiga bila uangalifu ukanaswa na Bocco aliyekimbia nao pembezoni mwa Uwanja kulia kabla ya kutia krosi iliyumkuta mshambuliaji Mganda Emmanuel Okiw aliyempasia kwa kichwa Kichuya ambaye naye alimpa Ndemla aliyefunga. 
  Baada ya hapo, Kagera Sugar waliokuwa wakicheza kwa kujihami kwa muda mrefu na kushambulia kwa kuvizia, wakaamua kufunguka moja kwa moja kusaka bao la kusawazisha.
  Lakini hiyo nayo iliwagharimu kufungwa bao la pili kwa shambulizi la kujibiwa, beki Shomary Kapombe akimlamba chenga beki wa Kagera Sugar, Adeyoum Ahmed na kutia krosi nzuri iliyomaliziwa na Bocco kuipatia Simba bao la pili.
  Ushindi huo unaifanya Simba SC irejee kileleni mwa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 32 baada ya kucheza mechi 14, ikifuatiwa na Azam FC pointi 30 na mabingwa watetezi, Yanga SC pointi 25.
  Na baada ya mchezo mashabiki walimkimbilia Ndemla na kumpa zawadi mbalimbali kila mmoja kwa uwezo wake, wengine fedha, wengine mikungu ya ndizi.  
  Ikumbukwe Mwenyekiti  wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameahidi kumnunulia gari Ndemla katika utaratibu wa kawaida aliojiwekea wa kuwazawadia gari wachezaji wanaojituma na wenye nidhamu kwenye timu.
  Ndemla atakuwa mchezaji wa pili Simba kuzawadiwa gari na Poppe baada ya beki, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kupewa gari aina ya Toyota Raum Septemba mwaka 2016.  
  Na Hans Poppe amesema amevutiwa na Ndemla kutokana na nidhamu yake na kujituma bila kukata tama wakati wote.
  “Ni mchezaji ambaye hana neno anapokuwa hapangwi, na akiinuliwa kuingia uwanjani wakati wowote huenda kufanya vizuri na kuisaidia timu. Kwa kweli huyu kijana ni mfano wa kuigwa kwe wenzake na anastahili zawadi hii,”amesema.
  Poppe amesema kwamba utamadunia wa kuwazawadia gari wachezaji wa klabu yake hiyo utaendelea na jukumu la kila mchezaji kuonyesha nidhamu na bidii kama Ndemla.   
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MASHABIKI SIMBA BUKOBA WAMZAWADIA NDEMLA FEDHA NA MIKUNGU YA NDIZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top