• HABARI MPYA

    Monday, December 18, 2017

    TFF YASOGEZA MBELE DIRISHA DOGO LA USAJILI HADI DESEMBA 23

    Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
    DIRISHA dogo la usajili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara sasa litafungwa Desemba 23, mwaka huu badala ya Desemba 15 kama  ilivyo kawaida.
    Ofsa wa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba, hiyo imetokana na hitilafu zilizotokea siku ya mwisho ya usajili usiku wa Desemba 15, mwaka huu baada ya kufeli kwa mtandao wa mfumo wa usajili hali iliyosababisha klabu kushindwa kukamilisha zoezi hilo kwa wakati kupitia mfumo huo.
    Na Lucas amesema wakati huu ambao jitihada za kurekebisha mfumo huo maarufu kama TMS zinaendelea, TFF imeziagiza klabu kuwasilisha nyaraka za usajili wa dirisha dogo moja kwa moja katika ofisi za Makao Makuu ya shirikisho hilo, Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
    Beki Mghana wa Lipuli, Asante Kwasi (kulia) akikabiliana na mshambuliaji Mrundi wa Simba, Laudit Mavugo

    “TFF imetoa muda hadi Jumamosi Desemba 23, 2017 kwa klabu kuwasilisha nyaraka hizo za usajili wa dirisha dogo. TFF inasisitiza vilabu vyote kuzingatia kusajili kwa wakati pale inapotokea dirisha la usajili limefunguliwa,” amesema Lucas.
    Ofisa huyo amesema kwamba TFF inaendelea na jitihada za kuwasiliana na Mwendeshaji wa mfumo huo waliokasimiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) walioko Tunis, Tunisia ili kutatua tatizo hilo la kimtandao  haraka iwezekanavyo ili kuweza kukamilisha usajili wa dirisha dogo. 
    Katika mawasiliano na kampuni hiyo, FIFA na CAF wamekuwa wakipewa Taarifa ya kila hatua inayochukuliwa na TFF.
    Wakati huo huo: Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliyosimama kupisha michuano ya Kombe la Challenge inaendelea mwishoni mwa mwezi huu kwa mechi za raundi ya 12 zitakazochezwa kati ya Desemba 29 na 31 mwaka huu, na Januari mosi mwakani.
    Vilevile mechi 16 kati ya 152 zilizobaki za Ligi hiyo zitachezwa kuanzia saa 8 kamili mchana. Kwa mujibu wa Kanuni ya 14 (45) ya Ligi Kuu, mchezo wowote wa Ligi Kuu unatakiwa kuchezwa kati ya saa 8 kamili mchana, na saa 4 kamili usiku.
    Uamuzi huo umefanywa ili kuongeza mechi ambazo zinataoneshwa moja kwa moja (live) na mdhamini wa matangazo, hatua ambayo itaisaidia Bodi ya Ligi kufuatilia kwa karibu uchezeshaji wa waamuzi na pia kutoa nafasi kwa wadhamini wa Ligi pamoja na wa klabu kuonekana zaidi (mileage).
    Hivyo, mechi 102 kati ya 152 zitaoneshwa moja kwa moja ikiwemo zile zinazofanyika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambazo kwa kawaida zinachezwa kuanzia saa 1 kamili usiku. 
    Mechi za raundi ya 12 ni Desemba 29; Azam vs Stand United (saa 1 usiku), Desemba 30; Lipuli vs Tanzania Prisons (saa 8 mchana), Mtibwa Sugar vs Majimaji (saa 10 jioni), Ndanda vs Simba (saa 10 jioni), Desemba 31; Njombe Mji vs Singida United (saa 8 mchana), Mbao vs Yanga (saa 10 jioni), Januari 1; Mbeya City vs Kagera Sugar (saa 10 jioni), na Mwadui vs Ruvu Shooting (saa 10 jioni).
    Baada ya raundi ya 12, Ligi Kuu ya Vodacom itapisha mechi za Kombe la Mapinduzi na raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia raundi ya 13 itakayofanyika kati ya Januari 13 na 17, 2018.
    Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL), itaingia raundi ya 10 Desemba 30 kwa mechi za Kundi A na C, wakati mechi za Kundi B zitafanyika Desemba 31.
    Ligi Daraja la Pili (SDL) itaanza hatua ya pili Desemba 29 kwa Kundi B, C na D wakati mechi za Kundi A zitafanyika kuanzia Desemba 30, 2017.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YASOGEZA MBELE DIRISHA DOGO LA USAJILI HADI DESEMBA 23 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top