• HABARI MPYA

    Sunday, December 24, 2017

    YANGA SC YASONGA MBELE AZAM SPORTS FEDERATION CUP, YAWAPIGA 2-0 WATOTO WA TEMEKE

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MABAO ya dakika za lala salama ya kiungo Pius Buswita na mshambuliaji Amissi Tambwe yameipa ushindi wa 2-0 Yanga SC dhidi ya Reha ya Temeke na kusonga mbele hatua ya 32 Bora ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
    Baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, Reha wakicheza kwa kujihami zaidi na kufanya mashambulizi ya kushitukiza, Yanga walibadili maarifa kipindi cha pili na kuanza kushambulia kwa nguvu zaidi.
    Lakini bado Reha iliyokuwa chini ya kocha Ivo Mapunda, kipa wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ilikuwa ngumu kufungika, mlinda mlango wake, Idrisa Ramadhani akidaka kwa ustadi wa hali ya juu.
    Wafungaji wa mabao Yanga; Pius Buswita akimpongeza Amissi Tambwe baada ya kufunga bao la pili
    Kipa wa Reha FC, Idrissa Ramadhani akidaka mpira mbele ya winga wa Yanga, Emmanuel Martin
    Kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi akimiliki mpira mbele ya mchzaji wa Reha
    Beki wa Reha, Ambele Daudi akiokoa mbele ya Amissi Tambwe wa Yanga
    Beki wa Yanga, Gardiel Michael akiwatoka wachezaji wa Reha

    Kocha Msaidizi wa Yanga, Nsajigwa Shadrack akafanya mabadiliko, akimpumzisha Emmanuel Martin na kumuingiza kinda Said Mussa ‘Ronaldo’ aliyekuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kilichoshiriki fainali za Afrika nchini Gabon Mei mwaka huu.
    Na ni huyo Said Ronaldo aliyekwenda kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji wa Yanga akishirikiana na Yussuf Mhilu, Tambwe na Buswita hata yakapatikana mabao mawili ya haraka haraka.  
    Kiungo aliyesajiliwa kutoka Mbao FC ya Mwanza, Buswita aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 82 kwa shuti kali baada ya kupokea pasi nzuri ya Tambwe kufuatia kazi nzuri ya kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi. 
    Buswita naye akamsetia Tambwe kufunga bao la pili dakika ya 84 baada ya kumtangulizia mpira kwa mbele na Mrundi huyo akamchambua kipa mgumu kufungika wa Reha, Idrisa.
    Baada ya bao hilo, Reha wakaonekana kabisa kukubali matokeo na Yanga wakaanza kucheza kwa uhuru uwanjani, wakigongeana pasi za kuwaburudisha mashabiki wao.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Youth Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Nadir Haroub, Andrew Vincent, Papy Tshishimbi, Yusuph Mhilu, Raphael Daud, Amis Tambwe, Pius Buswita na Emmanuel Martin/Said Mussa dk69.
    Reha FC; Idrisa Ramadhan, Brian Khiza, Japhary Athuman, Abdul Hassan, Ambele Daud, Zuberi Makame, RajabuMohamed, Silvanus Sostenes/Mohamed Abdallah dk58, Bazo Sentumbi/Mohammed Hassan dk64, Salum Athuman na Idrisa Omary
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YASONGA MBELE AZAM SPORTS FEDERATION CUP, YAWAPIGA 2-0 WATOTO WA TEMEKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top