• HABARI MPYA

    Sunday, December 24, 2017

    OMOG ANAWAACHIA SIMBA MATATIZO YAO NA MASUDI JUMA WAO

    KOCHA Mcameroon, Joseph Marius Omog jana amehitimisha miezi yake 17 ya kufanya kazi Simba baada ya jana kuondolewa kufuatia timu kuvuliwa ubingwa wa michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) katika hatua ya 64 Bora kwa kufungwa kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 na Green Warriors juzi  Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Aliyekuwa kocha Msaidizi, Mrundi Masudi Juma sasa ataiongoza timu kuelekea mwishoni mwa msimu. Omog amefukuzwa siku mbili tu tangu arejee nchini kutoka kwao, Cameroon alipokwenda kwa mapumziko na kuelekea mchezo wa juzi, timu iliandaliwa na Msaidizi wake, Juma.
    Lakini kumekuwa na tetesi za Omog kuondolewa kwa miezi miwili sasa na hata wakati Masudi Juma anawasili miezi miwili iliyopita ilielezwa anakuja kuwa Kocha Mkuu. 
    Mcameroon huyo aliyeirejesha Simba kwenye michuano ya Afrika 2018 baada ya miaka mitatu kufuatia kuipa Kombe la ASFC Mei mwaka huu ikiifunga Mbao FC 2-1 kwenye fainali Dodoma, alijiunga na klabu hiyo Julai 1, mwaka 2016, baada ya awali kufundisha klabu ya Azam FC na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2014.  
    Omog anaondoka Simba SC baada ya mechi 79, akiipa taji moja la ASFC Mei mwaka huu na hajafungwa mechi hata moja dhidi ya mahasimu, Yanga. 
    Katika mechi zake 79 tangu aanze kazi Msimbazi Julai mwaka jana, Omog ameshinda 53, kafungwa 10 na kutoa sare 16 na kati ya hizo amekutana na Yanga mara tano, mara tatu katika Ligi Kuu akishinda 2-1 Februari 26 mwaka jana (2016), sare mbili 1-1 zote Oktoba 1, 2016 na Oktoba 28, mwaka huu (2017).
    Mechi nyingine zote alishinda kwa matuta; kwanza ya Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 Januari 10, 2017 na nyingine ya Ngao ya Jamii kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 Agosti 23, mwaka huu.
    Historia inajirudia kwa Omog kufukuzwa nchini, baada ya awali pia kufukuzwa Azam FC ambao nao aliwapa taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na bila shaka anapata somo lingine zuri kuhusu soka ya nchi hii.
    Kwa Omog hata kuingia kwenye msimu wa pili Simba SC ni jambo ambalo halikutarajiwa, kwa sababu si kawaida kwa timu hiyo kuishi japo kwa msimu mzima na kocha mmoja katika miaka ya karibuni.
    Imekuwa vigumu kwa viongozi wa Simba miaka ya karibuni kujua wanahitaji nini kwa walimu na hata wachezaji, maana mara kadhaa imeacha makocha na wachezaji bora na kuangukia kwa wasiofaa.
    Haiyumkiniki lawama za Simba kutolewa katika mchezo wa juzi zimuangukie Omog – wakati hakuwepo nchini kwenye matayarisho ya mchezo wenyewe na alirejea siku mbili kabla ya mechi hiyo.
    Lakini pia mastaajabu kama hayo hutokea katika soka, timu kubwa yenye wachezaji wakubwa na nyota kutolewa kwenye mashindano na timu ndogo ya wachezaji wa kawaida.
    Ni Desemba 20 mwaka huu Manchester United ilipotolewa katika Robo Fainali ya Kombe la Ligi England na timu ya Daraja la Kwanza, Bristol City Uwanja wa Ashton Gate kwa kipgo cha 2-1. Huwezi kuifananisha Bristol na United kwa chochote kuanzia uwekezaji na hata uwezo wa wachezaji na benchi la Ufundi.
    Lakini United wametupwa nje, wamefunga ukurasa na kusonga mbele kwenye michuano mingine, huku Simba wanamtoa kafara Omog.
    Mchezo wa juzi achilia mbali Simba walicheza nyuma ya bahati yao, wachezaji wake nyota akina Shiza Kichuya, John Bocco, Muzamil Yassin, Said Ndemla, Jonas Mkude wakipoteza nafasi kadhaa za wazi – lakini pia kuna wachezaji wengine nyota kama Waghana, James Kotei, Nicholas Gyan, Mrundi Laudit Mavugo na Mganda Emmanuel Okwi hawakuwepo kabisa na sababu hazijulikani.
    Omog ameendeleza rekodi yake nzuri ya kushinda mataji katika kila timu – lakini pia anaondoka Simba kwa heshima ya kutofungwa na watani wa jadi, Yanga kitu ambacho nadhani hakikuwapendeza viongozi wa Simba chini ya Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘Try Again’ na sasa wanataka kujaribu matokeo tofauti.
    Omog anaondoka na kumbukumbu zake nzuri tu kwenye soka ya Tanzania, kushinda mataji yote makubwa, Ligi Kuu na ASFC na pia kutamba katika mechi za watani – na anawaachia Simba matatizo yao na ni juu yao na Masudi Juma wao. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OMOG ANAWAACHIA SIMBA MATATIZO YAO NA MASUDI JUMA WAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top