• HABARI MPYA

    Saturday, December 23, 2017

    WAKILI MGONGOLWA, PROFESA MGONGO FIMBO KUONGOZA KAMATI YA MABADILIKO YANGA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MWANASHERIA maarufu nchini, Alex Mgongolwa ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Mchakato wa Mabadiliko katika klabu ya Yanga.
    Uteuzi huo umetajwa Ijumaa na Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga katika mkutano wake na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga mjini Dar es Salaam.
    Sanga amesema Mgongolwa atakuwa pamoja na Makamu  Mwenyekiti, Profesa Mgongo Fimbo ambaye ni Mtaalam wa Katiba na Sheria za Ardhi, Mkuu wa zamani wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meckysadick na Wajumbe Mohamed Nyenge, ambaye ni Mchumi na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Fedha, George Fumbuka ambaye ni  Mshauri wa Masuala ya Uwekezaji na Felix Mlaki ambaye ni Mchumi na Mtaalam wa Masuala ya Fedha.
    Alex Mgongolwa (kushoto) akiwa na Mwanasheria mwenzake nguli, Imani Madega
    Yanga imeingia rasmi kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba kufuatia mahasimu wao, Simba kutangulia kwenye mfumo huo baada ya mkutano wao wa Desemba 3, mwaka huu kumpa zabuni mfanyabiashara Mohammed ‘Mo’ Dewji ya kuwekeza kwenye klabu hiyo.
    Katika mkutano huo uliofanyika ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uwekezaji ya Simba, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo alisema Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita.
    Hata hivyo, Serikali imeagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja na kusistiza lazima asilimia 51 ya hisa ziwe mali ya wanachama. 
    Yanga wao wansema Katiba yao ya mwaka 2010, Ibara 56 kipengele cha 3 kinajieleza kuwa wanachama wanatakiwa kumiliki asilimia 51 ya hisa wakati 49 inayobaki inaweza kwenda kwa Mwekezaji.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAKILI MGONGOLWA, PROFESA MGONGO FIMBO KUONGOZA KAMATI YA MABADILIKO YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top