• HABARI MPYA

    Saturday, December 23, 2017

    LWANDAMINA, LUCAS WA TFF WAFIWA NA WATOTO WAO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mzambia wa Yanga, George Lwandamina ataendelea kuwa kwao, Lusaka kwa muda mrefu kufuatia kufiwa na mtoto wake wa tatu, Mofya Lwandamina ambaye anatarajiwa kuzikwa Jumanne.
    Lwandamina ameithibitishia Bin Zubeiry Sports – Online leo taarifa za msiba wa mwanawe huyo, ambao utamfanya aendelee kukosekana kazini.
    “Ni kweli nimefiwa na motto wangu wa tatu, na hapa nipo kwenye msiba,”amesema Lwandamina alipozungumza kwa simu mchana huu kutoka Zambia.
    Ikumbukwe Lwandamina aliondoka Dar es Salaam wiki iliyopita kwenda nyumbani kwa ajili ya kuhudhuria mahafali ya mwanawe wa kike, Nasanta Lwandamina aliyehitimu Stashahada ya Afya ya Jamii katika Chuo Kikuu cha NRDC.
    Pole kocha George Lwandamina kwa kufiwa na mwanao. Mungu ampumzishe kwa amani

    Wakati anajiandaa kurejea nyumbani baada ya hafla ya binti yake kuhitimu masomo NRDC, Lwandamina anakutwa na msiba na mwanawe.
    Ikumbukwe Yanga SC kesho wanatarajiwa kuteremka kwenye Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam kumenyana na  Reha FC katika hatua ya 64 Bora ya Azam Sports federations Cup (ASFC).
    Ni jana tu, mahasimu wao, Simba SC wamevuliwa ubingwa wa michuano hiyo baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 na timu ya Green Warriors ya Mwenge, inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Wakati huo huo: Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas naye amefiwa na mwanawe mdogo jana. 
    Lucas amesema katika taarifa yake fupi leo; “Ni kweli nimefiwa na mtoto wa kike.  Alizaliwa jana Desemba 22, 2017. Aliishi kwa muda mchache kabla ya mauti kumfika jana saa 4:00 asubuhi. Nikafanya mazishi jana saa 11 jioni,”. 
    Lucas amesema mkewe ameruhusiwa mchana  huu kutoka hospitali na anaendelea vema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LWANDAMINA, LUCAS WA TFF WAFIWA NA WATOTO WAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top