• HABARI MPYA

    Thursday, December 28, 2017

    SI CHIRWA TU, HATA AJIB HATAKUWEPO YANGA NA MBAO MWANZA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC itaondoka kesho jioni kwa ndege ya Fast Jet kwenda Mwanza tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Mbao FC Jumapili Uwanja wa CCM Kirumba mjini humo.
    Lakini Yanga itaondoka bila washambuliaji wake wote vinara wa mabao msimu huu, Ibrahim Ajib na Mzambia Obrey Chirwa.
    Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo Ajib hatakwenda Mwanza kwa sababu anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano wakati Chirwa bado yupo kwao, Zambia kwa matatizo ya kifamilia.
    Katika mabao 17 ambayo Yanga imefunga kwenye Ligi Kuu msimu huu, 11 yanatoka kwa wawili hao, Chirwa akiwa amefunga sita na Ajib matano. 
    Pamoja na wawili hao, Yanga pia itaendelea kuwakosa wachezaji wake majeruhi Wazimbabwe, kiungo Thabani Scara Kamusoko na mshambuliaji Donald Dombo Ngoma pamoja na beki mzalendo, Kevin Patrick Yondan.
    Mshambuliaji Ibrahim Ajib hatakwenda Mwanza kwa sababu anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano

    Mkwasa amesema Chirwa anatarajiwa kurejea nchini kuanzia kesho na hawezi kujumuishwa kwenye msafara wa Mwanza wazi hatakuwa fiti. 
    Kwa ujumla Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea kesho baada ya mapumziko ya wiki tatu kupisha michuano ya CECAFA Challenge iliyomalizika nchini Kenya wiki iliyopita kwa wenyeji, Harambee Stars kuwa mabingwa wakiwafunga Zanzibar katika fainali.
    Kesho Azam FC watakuwa wenyeji wa Stand United Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 1:00 usiku na Jumamosi kutakuwa na mechi tatu, Lipuli na Tanzania Prisons Uwanja wa Samora, Iringa kuanzia Saa 8:00 mchana, Mtibwa Sugar na Maji Maji Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Ndanda FC na Simba SC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara zote zikianza saa 10:00 jioni.
    Jumapili, mabingwa watetezi, Yanga watakuwa wageni wa Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza saa 10:00 jioni na Njombe Mji FC wataikaribisha Singida United kuanzia saa 8:00 mchana Uwanja wa Saba Saba, Njombe.
    Mechi za kukamilisha mzunguko wa 12 zitachezwa mwaka mpya, Januari 1 Mbeya City wakiikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya  na Mwadui wakiikaribisha Ruvu Shooting zote kuanzia saa 10:00 jioni.
    Baada ya mechi hizo, Ligi Kuu itasimama tena kupisha mechi za Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na raundi ya tatu ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia kwenye mzunguko wa 13 wa ligi kuanzia Januari 13 na 17, 2018.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SI CHIRWA TU, HATA AJIB HATAKUWEPO YANGA NA MBAO MWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top