• HABARI MPYA

    Thursday, December 28, 2017

    WALIOSAJILIWA DIRISHA DOGO HATIHATI KUCHEZA LIGI KUU…HADI SASA HAWANA LESENI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WACHEZAJI wapya waliosajiliwa dirisha dogo watarahusiwa kuanza kucheza mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wikiendi hii kwa utaratibu maalum waliopewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). 
    Na hiyo ni kutokana na wachezaji hao kutopatiwa leseni za klabu zao mpya baada ya mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ujulikanao kama TMS kukorofisha.
    Ofisa Habari Msaidizi wa TFF, Clifford Ndimbo ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online kwamba klabu zimepewa maelekezo ya kufuata ili ziweze kuwatimia wachezaji wao wapya iliyowaongeza dirisha dogo.
    Mrisho Ngassa hataruhusiwa kuichezea Ndanda FC dhidi ya Simba Jumamosi kama hajakamilisha taratibu zinazotakiwa na TFF
    “Kuna utaratibu maalum ambao klabu zimepewa zinatakiwa kuufuata ili ziweze kuwatumia wachezaji hao wapya,”amesema Ndimbo.
    Katika siku ya kufunga dirisha dogo la usajili Desemba 15, mwaka huu TMS ilifeli hali iliyosababisha klabu kushindwa kukamilisha usajili kwa wakati kupitia mfumo huo na Desemba 16 TFF ikaagiza klabu ziwasilishe moja kwa moja usajili wake makao makuu ya shirikisho, Uwanja wa Karume, Dar es Salaam. 
    Lakini Desemba 17 TFF ikasema TMS imefunguliwa tena baada ya marekebisho ya hitilafu zilizojitokeza kufuatia shirikisho hilo kuwasiliana na waendeshaji wa mfumo huo  walioko Tunis, Tunisia na kuzitaka klabu zitaendelea kusajili hadi Desemba 23 dirisha lilipofungwa tena.
    Hata hivyo, klabu hazikufanikiwa kukamilisha usajili ndani ya muda hadi kupewa mwongozo mwingine juu ya taratibu za kufuata ili ziruhusiwe kuwatumia wachezaji wake wapya. 
    Baada ya mapumziko ya wiki tatu kupisha michuano ya CECAFA Challenge iliyomalizika nchini Kenya wiki iliyopita kwa wenyeji, Harambee Stars kuwa mabingwa wakiwafunga Zanzibar katika fainali, Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea kesho kwa mchez mmoja tu, Azam FC wakiwakaribisha Stand United Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 1:00 usiku.
    Ligi itaendelea Jumamosi kwa mechi tatu zaidi, Lipuli wakiwakaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Samora, Iringa kuanzia Saa 8:00 mchana, Mtibwa Sugar wakiwakaribisha Maji Maji Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Ndanda FC wakiwakaribisha Simba SC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara zote zikianza saa 10:00 jioni.
    Jumapili, mabingwa watetezi, Yanga watakuwa wageni wa Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza saa 10:00 jioni na Njombe Mji FC wataikaribisha Singida United kuanzia saa 8:00 mchana Uwanja wa Saba Saba, Njombe.
    Mechi za kukamilisha mzunguko wa 12 zitachezwa mwaka mpya, Januari 1 Mbeya City wakiikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya  na Mwadui wakiikaribisha Ruvu Shooting zote kuanzia saa 10:00 jioni.
    Baada ya mechi hizo, Ligi Kuu itasimama tena kupisha mechi za Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na raundi ya tatu ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia kwenye mzunguko wa 13 wa ligi kuanzia Januari 13 na 17, 2018.
    Nickson Kibabage hataweza kuichezea Njombe Mji hadi taratibu zilizoelekezwa na TFF ziwe zimekamilishwa

    WALIORIPOTIWA KUTOKA NA KUINGIA KLABU MBALIMBALI LIGI KUU 
    AZAM FC;
    WALIOINGIA: Bernard Arthur kutoa Liberty Professional ya Ghana
    WALIOTOKA: Yahya Mohammed
    SIMBA SC;
    WALIOTOKA: Method Mwanjali, Jamal Mnyate (mkopo Lipuli)
    WALIOINGIA: Asante Kwasi 
    SINGIDA UNITED;
    WALIOINGIA: Malik Antri (Ghana), Lubinda Mundia (mkopo Res Arrows ya Zambia), Daniel Lyanga (Fanja ya Oman), Kambale Salita 'Papy Kambale' (Etincelles ya Rwanda), Issa Makamba, Assad Juma, Ally Ng’azi na Mohamed Abdallah wote huru waliokuwa Sereneti Boys
    WALIOTOKA: Elisha Muroiwa (Mkataba umesitishwa), Atupele Green, (Mkataba umesitishwa) na Pastory Athanas (Mkataba umesitishwa). Mohamed Titi (ametolewa kwa mkopo Njombe Mji) na Frank Zakaria (ametolewa kwa mkopo Stand United).
    YANGA SC;
    WALIOINGIA: Fiston 'Festo' Kayembe Kanku (Balende FC ya DRC) na Yohanna Nkomola (huru, alikuwa Serengeti Boys)
    WALIOTOKA: Hakuna
    MBEYA CITY;
    WALIOINGIA: George Mpole (Maji Maji) na Abubakar Shaaban (Amepandishwa)
    WALIOTOKA: Emmanuel Kakuti (Duchu) na Mrisho Ngassa (Kamaliza mkataba)
    LIPULI:
    WALIOINGIA: Jamal Mnyate (mkopo kutoka Simba SC), Alex Ntiri (Mghana kutoka Mbao FC), Adam Salamba (Stand United), Miraji Mwilenga (Mufindi United), Zawadi Mauya (Mufindi United), Steven Mganga (Pamba FC), Nelson Campbell (Huru) na Feisal Salum Abdallah (Huru.
    WALIOTOKA: Waziri Ramadhani, Mussa Ngunda, Machaku Salum, Melvin Alistoto, Ahmed Manzi na Dotto Kayombo.
    RUVU SHOOTING:
    WALIOINGIA: Rajab Zahir Mohamed (Huru), Hamisi Saleh Maulid (Huru), Adam Ibrahim Abdallah (Huru), Gideon Brown Benson (Huru) na Alinanuswe Martin Mwaisemba (Huru).
    WALIOTOKA: Hakuna 
    NJOMBE MJI FC:
    WALIOINGIA: Herelimana Lewi (Mukura Victory, Rwanda), Etienne Ngladjo (Sunrise FC, Rwanda), Mohammed Titi (mkopo kutoka Singida United), Nickson Kibabage (mkopo kutoka Mtibwa Sugar) na Muhsin Malima (mkopo kutoka Mtibwa Sugar).
    WALIOTOKA: Hakuna 
    MTIBWA SUGAR
    WALIOINGIA: Hakuna
    WALIOTOKA: Nickson Kibabage (mkopo Njombe Mji FC) na Muhsin Malima (mkopo Njombe Mji FC).
    STAND UNITED:
    WALIOINGIA: Frank Zakaria (mkopo kutoka Singida United).
    WALIOTOKA: Hakuna
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WALIOSAJILIWA DIRISHA DOGO HATIHATI KUCHEZA LIGI KUU…HADI SASA HAWANA LESENI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top