• HABARI MPYA

    Friday, December 29, 2017

    SIMBA YAMTEMA KWASI SAFARI YA MTWARA, AAMBIWA ATAANZIA MAPINDUZI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BEKI mpya wa kati wa Simba SC, Asante Kwasi raia wa Ghana hataweza kuanza kuichezea klabu hiyo kesho katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji Sunday Manara ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Kwasi aliyesajiliwa dirisha hili dogo kutoka Lipuli ya Iringa hajasafiri na timu kwenda Mtwara kwa ajili ya mchezo huo.
    Manara amesema kwamba Kwasi atajiunga na timu itaporejea kutoka Mtwara kwa safari ya Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.
    Simba imepangwa Kundi A kwenye Kombe la Mapinduzi pamoja na Azam FC, URA ya Uganda, Jamhuri na Mwenge wakati Kundi lina timu za Singida United, Yanga SC, Zimamoto, Mlandege, JKU na Taifa ya Jan’gombe.
    Asante Kwasi hajasafiri na Simba kwenda Mtwara kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ndanda FC kesho

    Michuano ya Mapinduzi inaanza leo kwa mechi kati ya Mlandege na JKU Saa 8:30 mchana, kabla ya Jamhuri kumenyana na Mwenge Saa 10:30 jioni na Zimamoto kupepetana na Taifa ya Jan’gombe Saa 2:15 usiku, zote zikichezwa Uwanja wa Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Mabingwa watetezi, Azam FC wataanza mashindano Jumapili kwa kumenyana na Mwenge Saa 10:30 jioni kabla ya Jamhuri kumenyana na URA  Saa 2:15 usiku, wakati vigogo Simba na Simba wao wataanza mashindano Janauri 2, 2018. 
    Simba wataanza na Mwenge Saa 10:30 jioni wakati Saa 2:15 usiku Yanga watapepetana na Mlandege, mechi ambazo zitatanguliwa na mchezo kati ya Singida United na Zimamoto.
    Simba watarudi uwanjani Januari 4 kumenyana na Jamhuri Saa 2:15 usiku, kabla ya kukutana na Azam Januari 6 na kuhitimisha mechi zake za Kundi A kwa kumenyana na URA Januari 8, 2018 Saa 10:30 jioni.
    Mechi za makundi zinatarajiwa kukamilishwa Januari 8, wakati Januari 9 itakuwa mapumziko na Nusu Fainali zitafuatia Januari 10, kabla ya kilele mashindano kwa mchezo mtamu wa fainali Januari 13, ambao utahudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi visiwani humo, Dk. Ali Mohammed Shein.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAMTEMA KWASI SAFARI YA MTWARA, AAMBIWA ATAANZIA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top