• HABARI MPYA

    Tuesday, December 19, 2017

    AZAM FC KUMENYANA NA POLISI TANZANIA LEO USIKU CHAMAZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KATIKA kumalizia maandalizi yake katika kipindi hiki cha mapumziko ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kinatarajia kukipiga dhidi ya Polisi Tanzania kwenye mchezo wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Jumanne saa 1.00 usiku.
    Huo ni mchezo wa nne wa kirafiki kwa timu hiyo baada ya mapumziko hayo kupisha michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika jana Jumapili nchini Kenya, ilianza kwa kutoka sare na Friends Rangers (1-1) kabla ya kuzichapa Mvuvumwa (8-1) na Villa Squad (7-1).
    Akizungumzia programu ya mchezo huo dhidi ya timu hiyo ya polisi, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, alisema watautumia kama sehemu ya maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Area C United, Ligi Kuu na Kombe la Mapinduzi.
    Azam FC itafungua pazia la michuano ya Kombe la Shirikisho msimu huu kwa kukipiga dhidi ya timu hiyo kutoka mkoani Dodoma inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara (SDL), mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Jumamosi hii saa 10.00 jioni.
    Wakati huo huo: timu ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 13 (Azam U-13) imeibuka mabingwa ya michuano ya Kombe la Chipkizi kwa vijana wa umri huo baada ya kuichapa Express Academy kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya bao 1-1 Jumapili.
    Mashindano hayo yanaandaliwa na Future Stars Academy ya mkoani Arusha, ambapo Azam FC ndio mara ya kwanza kushiriki ikiwa na vikosi vipya ilivyoviunda hivi karibuni.
    Azam U-13 iliweza kufanya kweli na kupenya hadi robo fainali ikiifunga timu ya CTID bao 1-0, kisha nusu fainali ikaibugiza Moi Educational Centre ya Ghana mabao 5-0 kabla ya fainali kuifunga Express.
    Azam U-11 yenyewe haikufanikiwa kuingia robo fainali, lakini katika raundi za awali iliifunga Icons Football Academy ya Kenya (2-1) kabla ya kupoteza kwa bao 1-0 ilipocheza na Moi Educational Centre (1-0) na kutoka suluhu na Elite Soccer Academy.
    Mara baada ya michuano hiyo kumalizika, vikosi hivyo vya Azam FC vinatarajia kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho Jumatatu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC KUMENYANA NA POLISI TANZANIA LEO USIKU CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top