• HABARI MPYA

  Sunday, October 01, 2017

  SIMBA YAREJEA KILELENI LIGI KUU, YAWAPIGA STAND 2-1 KAMBARAGE

  Na Rehema Lucas, SHINYANGA
  SIMBA SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Stand United Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga jioni ya leo. 
  Ushindi huo umeifanya Simba ifikishe pointi 11 baada ya kucheza mechi tano, ikishinda tatu na kutoa sare mbili – sasa ikilingana kwa pointi na Mtibwa Sugar na Azam FC, lakini Wekundu wa Msimbazi wanapanda kileleni kwa wastani wao mzuri wa mabao. 
  Kero kubwa ilijitokeza mapema tu kwenye mchezo huo kutokana na timu zote kuvaa jezi zinazokaribia kufanana, Simba nyekundu na Stand za rangi ya chungwa. Kwa kawaida jezi za ugenini za Simba ni nyeupe. 
  Laudit Mavugo ametokea benchi leo na kuifungia bao la pili Simba PICHA YA MAKTABA
  Simba walipata bao la kwanza dakika ya 17 kupitia kwa winga wake machachari, Shiza Ramadhani Kichuya aliyefumua shuti kali kutoka umbali wa mita 20 baada ya kutengewa mpira na mshambuliaji John Raphael Bocco kufuatia pasi ya juu ya beki Erasto Nyoni.
  Bao hilo lilidumu hadi mapumziko na kipindi cha pili kocha Mcameroon wa Simba, Joseph Marius Omog akaanza na mabadiliko akimpumzisha Mganda, Emmanuel Okwi na kumuingiza mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo.
  Mabadiliko hayo yaliisaidia Simba kupata bao la pili lililofungwa na huyo huyo Mavugo dakika ya 47 baada ya kuwatoka mabeki wa Stand United kufuatia pasi ya Niyonzima na kumchambua kipa Mganda, Frank Muwonge.
  Stand United wakaamua kutoka kwenda kushambulia moja kwa moja na kufanikiwa kupata bao lao pekee hii leo, lililofungwa na mshambuliaji Mzimbabwe, Mtasa Munashe anayecheza kwa mkopo kutoka Singida United dakika ya 52.
  Beki Ally Shomary aliunawa mpira kwenye boksi na refa Suleiman Kinugani wa Kagera akatenga penalti, ambayo ilikwenda kupigwa na Munashe, lakini kipa namba moja Tanzania, Aishi Manula akapangua na mpira kumrudia Mzimbabwe huyo aliyefanikiwa kuusukuma nyavuni kwa shuti la chini chini.  
  Kinugani akakataa bao la Simba lililofungwa na Mavugo tena dakika ya 56 kwa kichwa kufuatia kona ya Haruna Niyonzima kuleta piga nikupige kwenye lango la Stand United, akidai Mrundi huyo alikuwa ameotea. Wachezaji wa Simba walimzoga refa kwa muda kablaya kuendelea na mchezo.
  Method Mwanjali akanawa mpira nje kidogo ya boksi, lakini Stand United wakashindwa kuitumia vizuri nafasi hiyo. Dakika tano za mwisho, lango la Simba lilikuwa kwenye misukosuko ya mashambulizi ya Stand na ashukuriwe kipa Aishi Manula aliyeokoa mfululizo hadi akaumia na kulala chini kutibiwa kwa takriban dakika moja.
  Kikosi cha Stand United kilikuwa; Frank Muwonge, Ally Ally, Aaron Lulambo, Hamad Kibopile, Jisend Maganda, Rajab Rashid, Kitoba Emmanuel/Sixtus Sabile dk76, Mageta Milambo/Kisatya Sahani dk69, Adam Salamaba, Mtasa Munashe na John Lwitiko. 
  Simba SC; Aishi Manula, Ally Shomary, Erasto Nyoni, Salim Mbonde, Method Mwanjali, James Kotei, Haruna Niyonzima/Jonas Mkude dk85, Muzamil Yassin/Said Ndemla dk68, John Bocco, Emmanuel Okwi/Laudit Mavugo dk46 na Shiza Kichuya.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YAREJEA KILELENI LIGI KUU, YAWAPIGA STAND 2-1 KAMBARAGE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top