• HABARI MPYA

    Wednesday, October 25, 2017

    YANGA NAO WAAMUA KUANZISHA TIMU YA WANAWAKE

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    UONGOZI wa klabu ya Yanga, umeanzisha mchakato wa kuunda timu ya wanawake, ili iwanie kushiriki Ligi ya Taifa kuanzia msimu ujao.
    Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema leo katika mkutano na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam kwamba Katiba yao inawaruhusu kuwa na timu ya wanawake na wanaona sasa ni wakati mwafaka kuianzisha.
    “Hakuna tatizo kuwa na timu ya wanawake, Katiba yetu inaruhusu na kuanzia leo tunafungua milango kwa wachezaji wanaoona wana uwezo kuja kujiandikisha kwa ajili ya usaili,”alisema.
    Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jangwani 

    Mpango wa Yanga kuanzisha timu ya wanawake unakuja baada ya mahasimu wao wa jadi, Simba kuwatangulia kwa kuanzisha Simba Queens ambayo msimu huu ilishiriki mchujo wa kuwania kucheza Ligi ya Taifa na kufuzu. 
    Ligi ya Taifa ya Wanawake inayodhaminiwa na Azam TV, inatarajiwa kuanza Novemba 26, mwaka huu ikishirikisha timu 12 zitakazogawanywa katika makundi mawili, kila kundi litakuwa na timu sita zikiwemo mbili zilizopanda msimu huu, Simba Queens na Alliance Academy baada ya kushuka kwa Viva Queens ya Mtwara na Victoria Queens ya Kagera.
    Kundi A litakalotumia kituo cha Dar es Salaam litaundwa na timu za Mlandizi Queens ya Pwani, JKT Queens ya Kinondoni, Evegreen ya Temeke, Mburahati Queens, Simba Queens za Ilala na Fair Play ya Tanga.
    Kundi B Madadi amesema litakuwa na timu za Panama ya Iringa, Marsh Academy, Alliance za Mwanza, Kigoma Sisterz ya Kigoma, Bao Bab ya Dodoma na Majengo Queens ya Singida.
    Hatua ya kwanza itafikia tamati Desemba 9 na kila kundi litatoa timu nne ambazo zitafuzu hatua ya pili ya ligi hiyo, itakayojulikana kama Super 8, itakayonza Desemba 20 hadi Machi 28, mwakani.
    Bingwa mtetezi wa Ligi ya Taifa ya Wanawake ni Mlandizi Queens, ambayo ilibeba taji hilo Machi mwaka huu katika michuano iliyofanyika kwa mara ya kwanza Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA NAO WAAMUA KUANZISHA TIMU YA WANAWAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top