• HABARI MPYA

    Tuesday, October 24, 2017

    SIMBA NA YANGA TATU ZA MWISHO KUCHEZWA SHAMBA LA BIBI ‘HAKUPIGWA MTU’

    MECHI TANO ZA MWISHO KABLA YA SIMBA 
    NA YANGA KUHAMIA UWANJA MPYA WA TAIFA
    Tarehe Matokeo Uwanja
    26/03/2006  Simba 0-0 Yanga Uhuru
    29/10/2006 Simba 0-0 Yanga Uhuru
    08/07/2007 Simba 1-1 Yanga (Pen5-4) Jamburi/Moro
    24/10/2007 Simba 1-0 Yanga  Jamhuri/Moro
    27/04/ 2008 Simba 0-0 Yanga Uhuru
    26/10/ 2008 Yanga 1-0 Simba Taifa

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    IMETHIBITISHWA mchezo wa mahasimu wa jadi, Simba na Yanga utafanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam Oktoba 28, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza baada ya miaka tisa.
    Mara ya mwisho, mahasimu hao wa jadi katika soka ya Tanzania kucheza Uwanja wa Uhuru ilikuwa ni Aprili 27, mwaka 2008 katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu, uliomalizika kwa sare ya 0-0.
    Mchezo uliotangulia wa msimu huo wa 2007/2008 ulichezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na bao pekee la Ulimboka Alfred Mwakingwe liliisambaratisha Yanga 1-0.
    Kipa Ivo Mapunda na mabeki Nsajigwa Shadrack, Edwin Mukenya na Amir Maftah walisimamishwa baada ya mchezo huo kwa tuhuma za kuhujumu timu.
    Baadaye wote walisamehewa, kasoro Mukenya aliyeondolewa moja kwa moja kwenye timu kufuatia pia mkataba wake kumalizika. 
    Kwa ujumla Simba na Yanga zilicheza mara tatu mfululizo Uwanja wa Uhuru bila kufungana, mechi nyingine zikiwa ni za Machi 26 na Oktoba 29, zote mwaka 2006.
    Timu ya mwisho kushangilia ushindi katika mechi ya Ligi Kuu ya mahasimu Uwanja wa Uhuru ilikuwa ni Simba, ambayo iliilaza Yanga 1-0 Septemba 18, mwaka 2004, bao pekee la Athumani Machuppa dakika ya 82, baada ya kumpiga chenga kali beki Samson Mwamanda.
    Ingawa Nusu Fainali ya Kombe la Tusker Agosti 15, mwaka 2006 inabaki kuwa mechi ya mwisho ya mahasimu wa jadi kutoa mshindi Uwanja wa Uhuru, baada ya Simba kushinda kwa penalti 7-6, kufuatia sare ya 1-1, Credo Mwaipopo akiisawazishia Yanga dakika ya 90 baada ya Emanuel Gabriel kutangulia kuwafungia Wekundu wa Msimbazi dakika ya 69. 
    Ukarabati wa mara kwa mara Uwanja wa Uhuru ulikuwa ukizisukumia nje ya Dar es Salaam mechi za mahasimu hao wa jadi na Julai 8, mwaka 2007 zilikutana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro katika fainali ya Ligi Ndogo. 
    Dakika 120 zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1, Moses Odhiambo akitangulia kuifungia Simba kwa penalti dakika ya pili, kabla ya Said Maulid ‘SMG’ kuisawazishia Yanga dakika ya 55, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti, ambako Simba ilishinda kwa penalti 5-4.
    Mchezo wa kwanza kufanyika Uwanja wa Uhuru, Yanga ikaifunga Simba baada ya muda mrefu, Oktoba 26, mwaka 2008 wakishinda 1-0, bao pekee la mshambuliaji Ben Mwalala aliyemalizia krosi ya Mkenya mwenzake, Boniphace Ambani dakika ya 15. 
    Baada ya miaka tisa, watani wa jadi wanarudi ‘Shamba la Bibi’ wakiwa na kumbukumbu ya kucheza mechi tatu mfululizo bila kutikisa nyavu. Je, Jumamosi itakuaje? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA YANGA TATU ZA MWISHO KUCHEZWA SHAMBA LA BIBI ‘HAKUPIGWA MTU’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top